Nchi kukumbwa na janga la ukosefu wa chakula

KENYA inakabiliwa na hatari ya upungufu mkubwa wa chakula huku wakulima katika maeneo yanayolisha taifa wakisita kupanda tena zao hilo baada ya ukame kuangamiza mazao ya awali.
Hofu hiyo inatanda licha ya serikali kutumia mabilioni ya fedha kupunguza gharama ya mbolea na mbegu katika juhudi za kuwashawishi wakulima kurejea mashambani msimu huu.
Katika maeneo ya North Rift, yanayojulikana kama ghala la chakula la Kenya, hali ya kusubiri na kuona imetawala.
Wakulima wengi wanahofia kupanda tena mahindi baada ya kupata hasara kutokana na ukame na magonjwa ya mimea.
Serikali imepunguza bei ya mbolea ya ruzuku kutoka Sh2,500 hadi Sh2,000 kwa gunia la kilo 50, huku ikigharamia nusu ya bei ya mbegu bora za mahindi.
Hatua hiyo imeshusha bei ya mbegu kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo.
Lakini kwa wakulima wengi, punguzo hilo halitoshi kuondoa hofu ya kupata hasara nyingine.
William Kosgei, mkulima kutoka Ziwa, Uasin Gishu, alisema gharama za kilimo ni zaidi ya mbolea na mbegu.
“Kilimo si suala la kupunguza tu gharama ya mbolea na mbegu za mahindi. Bado kuna gharama kubwa za mafuta ya trekta kutayarisha mashamba, dawa za kuua magugu na mishahara ya wafanyakazi. Aidha, hali ya hewa isiyotabirika inafanya kuwa hatari kupanda zao lile lile kwa mara ya pili katika msimu mmoja,” alisema.
Kwa miaka mingi, wakulima wa mahindi North Rift wamezoea kupanda zao hilo mara moja kwa mwaka.
Sasa wengi wao wanaombwa kupanda tena baada ya zao lao kuharibiwa na ukame mkali na milipuko ya magonjwa.
Hii imezua swali kubwa kuhusu iwapo wakulima wako tayari kuhatarisha mtaji wao tena.
Mkurugenzi wa Chama cha Wakulima Kenya (KFA), Kipkorir Menjo, alisema hofu imeenea miongoni mwa wakulima.
“Kuna mashaka makubwa miongoni mwa wakulima kuhusu iwapo wapande tena au wasubiri msimu ujao. Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha hali ya hewa kutotabirika na wakulima wanaogopa kupata hasara nyingine kutokana na majanga ya kiasili,” alisema.
Bw Menjo alisema wakulima wengi bado wanahangaika kulipa mikopo waliyochukua kufadhili mazao yaliyoharibiwa.
“Wakulima waliopata mikopo ya mamilioni ya shilingi kutoka taasisi kama Agricultural Finance Corporation (AFC) sasa wanakabiliwa na changamoto ya kulipa madeni hayo huku wakihitajika kuwekeza katika zao jingine,” alisema.
Hali hiyo inaweka shinikizo zaidi kwa sekta ya kilimo ambayo tayari inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uasin Gishu na Trans Nzoia, ambazo ni miongoni mwa kaunti muhimu katika uzalishaji wa mahindi, zimeathiriwa na ukame, na hivyo kuongeza hofu kuhusu uzalishaji wa chakula katika msimu unaokuja.
Serikali, hata hivyo, imeamua kuongeza ruzuku kwa matumaini ya kuzuia wakulima kuacha kilimo.
Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo Mutahi Kagwe alisema bei ya gunia la kilo 50 la mbolea imeshushwa kwa Sh500, kutoka Sh2,500 hadi Sh2,000.
“Kiini cha mpango huu ni kuhakikisha kwamba mkulima aliyepoteza zao kutokana na ukame hapotezi pia uwezo wa kupanda zao linalofuata kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za mbolea na mbegu,” alisema.
Hata hivyo, kwa wakulima wanaokabiliwa na madeni, gharama za kutayarisha mashamba na hali ya hewa isiyotabirika, bei ya mbolea pekee huenda isiwe kichocheo cha kutosha.
Hofu yao ni kwamba, kupanda tena bila uhakika wa mvua kunaweza kuwa mwanzo wa hasara nyingine.
Na ikiwa maelfu ya wakulima wataamua kusubiri hadi msimu ujao, athari zake zinaweza kwenda mbali zaidi ya mashamba yao.
Zinaweza kuathiri upatikanaji wa mahindi, bei ya chakula na usalama wa chakula nchini.
Kwa sasa, Kenya iko katika mashindano dhidi ya muda: Serikali inataka mashamba yarejee katika uzalishaji, lakini wakulima wanataka kwanza uhakika kwamba hawatapelekwa tena kwenye mzunguko wa madeni na hasara.


from Taifa Leo https://ift.tt/FGNHieR
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post