
MJADALA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027 umechukua mkondo mpya baada ya kauli za viongozi wa kisiasa kuashiria uwezekano wa kuibuka kwa muungano wa kisiasa kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Huku baadhi ya wadau wakichukulia ushirikiano huo kama silaha ya kumenyana na Rais William Ruto, wengine wanahisi unaweza kuwa chanzo cha migawanyiko mipya ndani ya upinzani.
Aliyekuwa Seneta wa kuteuliwa Gloria Orwoba ni mmoja wa waliozua mjadala huo baada ya kusema Wakenya wasipuuzilie mbali uwezekano wa Gachagua na Sifuna kujitokeza pamoja kwenye tiketi ya urais mwaka 2027.
Kwa mujibu wa Orwoba, Sifuna si mwanasiasa wa kawaida bali ni kiongozi anayeweza kuwa mgombea mkuu wa kiti hicho. Kauli hiyo imeongeza uzito kwa mjadala unaoendelea kuhusu nafasi ya Sifuna katika siasa za kitaifa huku uchaguzi ukikaribia.
Nyota ya Sifuna anayehusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi imekuwa iking’aa na kujijenga kama nguvu mpya ya kisiasa kuelekea 2027.
Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa ni chombo cha kisiasa atakachotumia kwa azma yake. Orwoba anadai kuwa Sifuna tayari ana chama lakini anatafuta namna ya kukipa sura mpya ili kivutie wafuasi wengi zaidi. Ndani ya vuguvugu la Linda Mwananchi, mjadala kuhusu chama bado unaendelea.
Lakini licha ya mjadala kuhusu vyama, Orwoba anaamini chama hakitakuwa kigezo kikuu kwa wapigakura. Kwa mtazamo wake, Wakenya wataangalia zaidi mgombea kuliko nembo ya chama.
Kauli hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa tiketi ya Gachagua na Sifuna. Kwa mara ya kwanza, viongozi wa upinzani wameanza kuzungumzia waziwazi uwezekano wa wawili hao kushirikiana katika kinyang’anyiro cha urais.
Kinachofanya mjadala huo kuwa wa kipekee ni kwamba Gachagua mwenyewe amewahi kusema hadharani kwamba yuko tayari kuwa mgombea mwenza wa Sifuna iwapo viongozi wa upinzani wataafikiana kuwa seneta huyo ndiye anayefaa kuongoza muungano huo. Aidha, amesema pia kwamba mpangilio wa kinyume unaweza kutokea ambapo yeye akiongoza tiketi na Sifuna kuwa mgombea mwenza.
Kauli hizo zimezua hisia mseto ndani ya upinzani. Wapo wanaoamini kuwa ushirikiano kati ya mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kiongozi anayevutia vijana na wakazi wa mijini unaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za taifa. Hata hivyo, wengine wanatahadharisha kuwa hatua hiyo inaweza kuibua malumbano mapya kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya upinzani.
Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ni mmoja wa watetezi wakuu wa muungano huo. Malala anaamini kwamba kuunganisha nguvu za Gachagua na Sifuna kutaunda kambi imara yenye uwezo wa kumpa Rais Ruto ushindani mkubwa.
Kwa mujibu wa Malala, hesabu za kisiasa zinaonyesha kwamba kuunganisha Mlima Kenya, Magharibi na jamii za Maa kunaweza kuunda msingi mkubwa wa kura. Ndiyo sababu ametangaza mpango wa kuanzisha vuguvugu la “Triple M” linalolenga kuleta pamoja watu wa Mrima, Mulembe na Maa.
Malala amekuwa akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Mlima Kenya na Magharibi mwa Kenya unaweza kuamua matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, siasa za upinzani bado zinaonekana kuwa katika hatua ya mazungumzo. Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kimeweka wazi kwamba kwa sasa hakitajiunga na Muungano wa Ukombozi (TUA).
Badala yake, kina nia ya kushirikiana kwanza na vuguvugu la Linda Mwananchi kabla ya kuingia katika mazungumzo ya kuunda muungano mpana wa upinzani.
Msimamo huo unaonyesha kuwa bado kuna tofauti za kimkakati kati ya vikundi mbalimbali vinavyolenga kumng’oa Rais Ruto mamlakani mwaka 2027.
Wakati Kalonzo Musyoka na washirika wake wakisisitiza umuhimu wa muungano mmoja wa upinzani, makundi mengine yanaonekana kutaka kujijenga kwanza kabla ya kuamua namna ya kushirikiana.
Kwa sasa, tiketi ya Gachagua na Sifuna bado ni wazo linalojadiliwa kisiasa na si makubaliano rasmi.
Hata hivyo, kauli za Orwoba, Malala na Gachagua mwenyewe zimeifanya kuwa mojawapo ya mada zinazovutia zaidi katika siasa za 2027.
Iwapo “ndoa” hiyo ya kisiasa itafungwa rasmi, inaweza kuimarisha upinzani au kuibua mvutano mpya ikizingatiwa kuwa Gachagua ni mmoja waliosuka muungano wa upinzani unaohusisha Kalonzo, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Fred Matiang’i, Justin Muturi miongoni mwa wengine ambao awali walionekana kuungana dhidi ya Rais Ruto.
Lakini jambo moja liko wazi: mjadala kuhusu Gachagua na Sifuna umeanza kuvuruga hesabu za upinzani na kufungua sura mpya ya siasa za uchaguzi
from Taifa Leo https://ift.tt/qK5OtT0
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS