Wageni waingiwa na taharuki tele kutokana na agizo la Rais Ruto

MAMIA ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini jana waligubikwa na taharuki na wasiwasi baada ya Rais William Ruto kuamuru msako dhidi yao hasa wale wanaofanya biashara ndogondogo.

Amri hiyo iliyotolewa wiki jana Septemba 2 wakati wa mkutano na wafanyabiashara wadogo (MSME) ilisababisha pilkapilka za kukimbilia stakabadhi za kusafiri, baadhi ya biashara kufungwa na ripoti za vitisho na kuhangaishwa katika sehemu mbalimbali nchini.

Mtanziko huo ulitokana na kile wanachosema raia wa kigeni walielewa kama amri ya kuondoka na ufafanuzi uliofuata kutoka kwa serikali kwamba msako huo unalenga wale wanaoendesha shughuli kinyume cha masharti ya uhamiaji, kibali cha kazi na sheria nyinginezo.

Jijini Nairobi, raia wa Burundi waliojawa wasiwasi walipanga foleni nje ya ubalozi wao jana, baadhi wakisaka stakabadhi za dharura kusafiri kurejea makwao huku wengine wakitafuta msaada wa kuhalalisha biashara zao na kuendelea kuwepo nchini.

Matukio hayo yaliashiria suitafahamu iliyofuatia matamshi ya Rais huku raia wa kigeni wanaofanya biashara wakichanganyikiwa kuhusu iwapo waliagizwa kuondoka nchini au wanahitajika kuhalalisha biashara na hadhi yao ya uhamiaji.

Nchini kote, wasiwasi uligeuka hofu ikiripotiwa kuwa raia wa kigeni walichelea kufungua biashara zao, kuacha makao yao na katika baadhi ya maeneo madai ya kuhangaishwa na wizi.

Serikali, hata hivyo, inasisitiza msako huo si amri ya kuwafurusha raia wa kigeni nchini.

Maafisa wanasema wanaolengwa ni wale wanaoendesha biashara zao bila vibali vya kazi, leseni au hadhi ya uhamiaji inayohitajika, huku raia wa kigeni wafanyabiashara waliosajiliwa wakilindwa.

Jijini Nairobi, mamia ya raia wa Burundi walijitokeza katika ubalozi wao wakisaka stakabadhi za usafiri na msaada, huku baadhi wakisema wanajiandaa kurejea makwao kwa sababu hawahisi kuwa salama tena kenya.

Foleni ndefu zilipangwa nje ya balozi huku wafanyabiashara waliozongwa na wasiwasi wakiitisha ufafanuzi kuhusu hatima yao.

Katika Ubalozi wa Burundi, baadhi ya raia waliozungumza na vyombo vya habari walisema waliondoka nchi yao kusaka nafasi za kitega uchumi na waligeuza Kenya kuwa makao yao ya pili.

“Nchi yetu ni ndogo, tunakabiliwa na ukosefu wa ajira na hatuna shughuli nyingi zinazofanyika ndiposa tuling’ang’ana kuja Kenya kuyainua maisha yetu. Tumewajua Wakenya kama watu wa amani na taifa bora Afrika lakini sijakula kwa siku mbili nilipojua tunatimuliwa,” akasema Erick Bizimana, aliyekuja Kenya 2022.

Mjini Murang’a, Jean Niyonzima, 28, ambaye amechuuza kahawa na mandazi kwa miaka mitano alisema alisimamishwa na maafisa wawili wa polisi Septemba 6 akidai alilazimishwa kusalimisha Sh3,000.

Mfanyabiashara mwengine Esperance Ndayishimiye, 24, anayeuza mavazi ya wanawake Murang’a, alisema hali imevurugika.

Homa Bay, raia kadhaa wa kigeni waliripoti biashara zao kuvunjwa na mali ikiwemo vifaa vya simu, viatu na nguo kuibiwa.

Mfanyabiashara raia wa Rwanda Zarubbabel Rusesabagina alisema alipoteza sehemu kubwa ya mali yake ikiwemo pasipoti, kadi ya ATM, vitambulisho na Sh16,000 pesa taslimu.

Mjini Kisii, wafanyabiashara wengi raia wa Uganda, Burundi na Rwanda hawakufungua biashara zao jana wakihofia kukamatwa na mali yao kuporwa.

Miji ya Narok, Kericho, na Bomet, raia wa kigeni wachuuzi pia walijiepusha kwenda barabarani huku baadhi wakiripotiwa kusafiri Nairobi kuwasilisha malalamishi kwa serikali.

Jijini Mombasa, raia wengi wa kigeni ambao kwa kawaida huchuuza bidhaa au kufanya kazi katika vinyozi, hoteli na vituo vya kuoshea magari hawakuwepo pia.

Lakini mjini Nyahururu, baadhi ya wanafanyabiashara waliapa kuwalinda raia wa kigeni ambao wameishi nao kwa miaka mingi.

“Tumeishi nao kwa miongo mingi, watoto wetu wanasoma pamoja shuleni. Wengi wao walizaliwa na kulelewa hapa, ni nyumbani ya pekee wanayojua, amri ya rais haina uhalisia,” akasema mfanyabiashara Philip Kahome.

Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui alisema baadhi ya raia wa kigeni wanatumia vibaya hati za kusafiria na mipango ya kuingia nchini kwa kushiriki biashara wakiwa kwenye hadhi ya mwekezaji au mtalii bila vibali vya kazi vinavyohitajika.

Bw Kinyanjui alisema raia wa kigeni watakaopatikana wakikiuka masharti ya uhamiaji watapokonywa hati zao kulingana na sheria.

Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Abraham Korir Sing’oei vilevile aliwahakikishia raia wa kigeni kwamba matamshi ya Rais hayapaswi kufasiriwa kama amri ya jumla dhidi ya raia wote wa kigeni wafanyabiashara.

Alisema wafanyabiashara wadogo na wakubwa na waajiriwa wa mataifa yote walio na stakabadhi zinazohitajika, ikiwemo vibali vya kazi wamelindwa kisheria kuendesha shughuli zao Kenya.



from Taifa Leo https://ift.tt/p7WwQMr
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post