Ruto ajikokota ukuaji uchumi katika miaka 3 ya kwanza ukiwa nyuma ya Kibaki na Uhuru

KUFIKIA mwisho wa miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Rais Mwai Kibaki, uchumi wa Kenya ulikuwa umeimarika kwa kasi, ukirekodi ongezeko maradufu la ukuaji na kuboresha maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa.

Katika kipindi hicho, Pato la Taifa (GDP) liliongezeka hadi asilimia 5.8 kutoka 2.9 mwaka wa 2003, huku uwezo wa ununuzi wa wananchi ukiongezeka kwa takriban Sh1,600 kwa mwezi.

Takwimu zinaonyesha kuwa mishahara halisi, inayozingatia mfumuko wa bei, iliongezeka kwa asilimia 12.5 kufikia mwaka 2005.

Hii inaashiria kuwa wafanyakazi walikuwa na fedha zaidi mikononi mwao hali iliyowawezesha kukabiliana vyema na gharama ya maisha.

Wafanyakazi wa sekta ya kibinafsi na wa umma walinufaika kwa pamoja na ukuaji huo wa uchumi.

Miaka 20 baadaye, Ripoti ya Hali ya Kiuchumi ya 2026 inaonyesha picha tofauti kwa utawala wa Rais William Ruto, ambaye ameongoza kwa miaka mitatu sasa.

Ingawa uchumi umeendelea kukua, kasi yake imekuwa ya chini zaidi katika kipindi hicho, ikishuka hadi asilimia 4.6 mwaka wa 2025 kutoka asilimia 5.7 katika mwaka wake wa kwanza kamili madarakani.

Hali hii inaonyesha changamoto ya kudumisha kasi ya ukuaji wa uchumi, hasa ikizingatiwa kuwa kiwango hicho ni cha chini zaidi tangu mwaka 2020 wakati wa janga la Covid-19.

Ukuaji huo pia uko chini ukilinganishwa na watangulizi wake, jambo linaloibua maswali kuhusu uthabiti wa sera za kiuchumi katika kipindi cha sasa.

Hata hivyo, kuna afueni kidogo kwa wananchi, kwani mishahara halisi imeongezeka kwa asilimia 1.7 katika miaka mitatu ya kwanza ya utawala wa Rais Ruto.

Wastani wa mshahara wa kila mwezi sasa ni Sh56,566, ikiwa ni ongezeko la takriban Sh959 kwa uwezo wa matumizi ya wananchi.

Ripoti ya Shirika la Takwimu Kenya (KNBS) inaonyesha kuwa sekta ya kibinafsi imekuwa nafuu zaidi, ikirekodi ongezeko la asilimia 3.9 ya mishahara ya kila mwaka hadi Sh716,100.

Kinyume chake, sekta ya umma imeshuhudia kushuka kwa asilimia 2.2, hali iliyopunguza mishahara halisi hadi Sh600,600 kwa mwaka.

Hii ina maana kuwa wafanyakazi wa sekta ya kibinafsi wameweza kukabiliana kwa kiasi fulani na kupanda kwa gharama ya maisha, huku wakiongeza uwezo wao wa matumizi kwa takriban Sh2,500 kwa mwezi.

Kwa upande mwingine, wafanyakazi wa serikali wamepoteza takriban Sh2,100 kwa mwezi kutokana na shinikizo la gharama ya maisha.

Katika miaka mitatu ya kwanza, utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulirekodi ukuaji mdogo zaidi wa mishahara halisi.

Mishahara iliongezeka kwa kiasi kidogo kutoka Sh30,722 mwaka 2013 hadi Sh30,864 mwaka 2015, huku wafanyakazi wa serikali wakipoteza uwezo wa matumizi kwa takriban Sh962 kwa mwezi.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, utawala wa Kibaki unabaki kuwa mfano bora zaidi.

Ndani ya miaka mitatu, uchumi uliongezeka kwa kasi kutoka asilimia 2.9 hadi 5.8, hali iliyochochewa na mageuzi ya kiuchumi, uwekezaji na mazingira bora ya biashara.

Chini ya utawala wa Rais Kenyatta, uchumi ulipitia vipindi vya kupanda na kushuka kati ya asilimia 5.4 na 5.9 katika miaka yake ya mwanzo, lakini bado ulikuwa juu kuliko kiwango cha sasa chini ya Rais Ruto.

Kulingana na takwimu halisi za pato la taifa, uchumi ulikuwa mkubwa zaidi kufikia mwisho wa mwaka wa tatu wa utawala wa Kenyatta, ambapo GDP ilifikia Sh6.28 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32 kutoka mwaka 2013.

Kwa sasa, uchumi wa Kenya unakadiriwa kufikia Sh17.58 trilioni, ongezeko la asilimia 16.9 kutoka mwaka 2023.

Katika suala la ajira, utawala wa Kenyatta ulifanya vyema zaidi katika miaka yake mitatu ya kwanza.

Idadi ya ajira mpya iliongezeka kwa asilimia 12.1 mwaka 2015 ikilinganishwa na mwaka 2013, huku ajira zikiongezeka kila mwaka katika kipindi hicho.

Kwa sasa, uchumi wa Kenya uliunda ajira mpya 822,100 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 kutoka mwaka uliotangulia.

Hata hivyo, idadi hii ni ya chini ikilinganishwa na ajira 848,100 zilizoundwa mwaka 2023, mwaka wa kwanza kamili wa utawala wa Rais Ruto.

Sekta isiyo rasmi inaendelea kuwa mhimili mkuu wa ajira nchini, ikichangia asilimia 83.8 ya wafanyakazi wote milioni 21.6.

Wengi wao wako katika sekta za biashara, hoteli na huduma dogo dogo.

Sekta ya ujenzi imeibuka kuwa miongoni mwa zinazokua kwa kasi zaidi, ikirekodi ukuaji wa asilimia 6.7.

Ukuaji huu umechochewa na uwekezaji katika mpango wa nyumba za bei nafuu pamoja na miradi ya miundombinu ya barabara.

Serikali ilikamilisha nyumba 6,738 mwaka jana, kutoka 1,655 mwaka uliotangulia.

Aidha, benki zimeongeza mikopo kwa sekta ya ujenzi kwa kiasi cha Sh70 bilioni, hatua inayochangia kupanuka kwa sekta hiyo.

Hata hivyo, sekta ya kilimo imeendelea kudorora, huku ukuaji ukishuka hadi asilimia 2.8 mwaka 2025 kutoka 4.3 mwaka uliotangulia.

Hali hii imechangiwa na uzalishaji hafifu wa mazao muhimu kama chai na sukari pamoja na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nje.

Katika sekta ya afya, matumizi ya serikali yameongezeka, huku serikali ya kitaifa ikitumia Sh150.9 bilioni na serikali za kaunti Sh133.4 bilioni ili kuboresha miundombinu na huduma za afya.

Sekta ya elimu pia inatarajiwa kunufaika na ongezeko la bajeti, ambapo matumizi yanakadiriwa kuongezeka kutoka Sh615.8 bilioni mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Sh702.1 bilioni mwaka 2025/2026, ikiwa ni pamoja na Sh30 bilioni za maendeleo.



from Taifa Leo https://ift.tt/lo1G3jX
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post