
KIKOSI cha mwisho cha maafisa 150 wa polisi wa Kenya waliokuwa wakihudumu nchini Haiti kilirejea nchini Jumanne na kufunga rasmi operesheni chini ya mpango wa kimataifa uliolenga kukabili magenge katika nchi hiyo.
Maafisa hao waliondoka Port-au-Prince wakiwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Naibu wake Eliud Lagat, walikutana na maafisa wa juu na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa kabla ya kurejea nyumbani.
Hata hivyo, huku familia nyingi zikisherehekea kurejea kwa wapendwa wao, familia ya afisa mmoja bado imegubikwa na sintofahamu.
Zaidi ya mwaka mmoja tangu atoweke, hatima ya Benedict Kabiru Kuria bado haijulikani.
Afisa huyo alitoweka Machi 25, 2025 kufuatia shambulio la genge katika eneo la Pont-Sonde, Artibonite, na tangu wakati huo juhudi za kumtafuta hazijafua dafu.
Kwa familia yake, kurejea kwa kila kikosi kumekuwa chanzo cha maumivu badala ya furaha.
Kila kundi la maafisa liliporejea, walitamani awe mmoja wao.
Mnamo Jumanne, matumaini hayo yaliendelea kuwepo, japokuwa dalili zilionyesha vingine.
Ndugu zake wanasema kimya kutoka kwa serikali kimekuwa kizito sawa na tukio lenyewe.
Wanalalamikia simu zisizojibiwa na maelezo yanayobadilika, wakihisi kwamba jamaa yao amesahaulika.
“Hatuombi mengi, tuambieni alipo na kilichompata,” alisema ndugu yake Philip Kamau, akiongeza kuwa wamekutana mara kadhaa na maafisa wa polisi lakini hawajapata majibu ya kuridhisha.
Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa afisa huyo bado “hajulikani aliko,” huku ujumbe wa rambirambi kutoka serikali ya Haiti ukizua mkanganyiko zaidi kuhusu iwapo alifariki au la.
Hali hii imelazimu familia kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya maafisa wa serikali, akiwemo Waziri Murkomen, Bw Kanja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, wakitaka ufafanuzi rasmi.
Wakati huo huo, Kenya imekabidhi uongozi wa operesheni hiyo kwa kikosi kingine.
cha kukandamiza magenge, huku kurejea kwa askari hao kukifuatia madai mapya ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya baadhi ya wanajeshi wa MSS.
Kenya imekanusha madai hayo vikali mbele ya Umoja wa Mataifa huku Balozi Erastus Lokaale akisisitiza kuwa operesheni hiyo ilifuata viwango vya juu vya taaluma, uwajibikaji na uwazi.
Hata hivyo, kwa familia ya Kuria, mjadala huo wote hauna maana bila majibu.
Hadi watakapojua ukweli, maisha yao yatasalia yamesimama kati ya matumaini na hofu.
from Taifa Leo https://ift.tt/nPJGkzW
via IFTTT