Wanasiasa wanaocheza kamari hatari kuelekea 2027

UCHAGUZI mkuu wa mwaka wa 2027 unavyokaribia, siasa za Kenya zinashuhudia mwelekeo mpya ambapo baadhi ya viongozi waliochaguliwa wanaonekana kuwa tayari kuacha nyadhifa walizo nazo kwa sasa ili kutafuta kubwa na zenye mamlaka zaidi, ushawishi na umaarufu kitaifa.
Kuanzia kwa maseneta wanaolenga ugavana, wabunge wanaotaka kuwa magavana, hadi magavana na wabunge wanaomezea mate urais, hali hii imegeuza uchaguzi wa 2027 kuwa mchezo hatari wa kubadilishana nafasi za kisiasa.
Kwa baadhi ya viongozi, hatua hiyo ni ya kimkakati. Magavana wanaokamilisha mihula yao miwili hawana chaguo jingine isipokuwa kutafuta nafasi nyingine za kisiasa. Wengine wako tayari hata kuwania nyadhifa za chini ili waendelee kubaki katika uongozi.
Hata hivyo, kwa wabunge na maseneta wengine, uamuzi huo ni hatari zaidi. Mbunge anayedhibiti vizuri eneo alilochaguliwa anaamua kuacha kiti chake salama ili kuwania ugavana wa kaunti nzima, huku maseneta wakihatarisha nyadhifa zao kwa kuwania ugavana.
 Miongoni mwa viongozi maarufu waliotangaza au kuonyesha nia ya kuwania urais ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
Sifuna ameonyesha wazi kuwania urais kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi. Kwa upande wake, Orengo amesema yuko tayari kushindania tiketi ya urais ya vuguvugu hilo dhidi ya Sifuna au mgombea mwingine yeyote.
"Hakuna ubaya kuwa na viongozi wenye malengo tofauti ndani ya Linda Mwananchi au upinzani. Muhimu ni kuwa na mchakato wa haki wa uteuzi ili hatimaye tupate mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto," akasema Orengo.
Wachambuzi wa siasa wanasema kauli hiyo inaonesha changamoto inayokabili upinzani, yaani ikiwa viongozi wanaoshikilia nyadhifa muhimu wanapaswa kuhatarisha nafasi walizonazo kwa kuwania urais.
Mbali na urais, viongozi wengi nchini wanahama kutoka nyadhifa walizonazo kuelekea ugavana.
 Katika Kaunti ya Bungoma, Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi anajiandaa kuwania ugavana na anatarajiwa kukutana na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa katika kinyang'anyiro hicho. Barasa amemtaja Wanyonyi kama “mtalii wa kisiasa” kwa kubadilisha maeneo ya kuwania nyadhifa.
 Nairobi pia imekuwa kitovu cha ushindani mkali. Wabunge Babu Owino wa Embakasi Mashariki, James Gakuya wa Embakasi Kaskazini na Ronald Karauri wa Kasarani wanatajwa kuwa miongoni mwa wanaojipanga kugombea ugavana katika jiji kuu.
Hatua hiyo ni hatari kwa kuwa wanaacha maeneo yao ya uchaguzi yenye wapigakura wanaowafahamu na kuingia katika ushindani unaohusisha mamilioni ya wapigakura wa kaunti nzima.
Katika Kaunti ya Siaya, Mbunge wa Ugenya David Ochieng’ anataka kumrithi Orengo kama gavana. Kiongozi wa ODM Oburu Oginga tayari amemhimiza avunje chama chake cha Movement for Democracy and Growth na kujiunga na ODM ili kupata uungwaji mkono katika mbio hizo.
Kisumu nayo imekuwa na orodha ndefu ya wanaotazamia kurithi Gavana Anyang’ Nyong’o. Naibu Gavana Mathews Owili, Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron, Mbunge wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu, Mwakilishi wa Kike Ruth Odinga na Seneta Tom Ojienda wote wanatajwa kutamani ugavana.
Katika Kaunti ya Migori, Mbunge wa Uriri Mark Nyamita ameweka macho yake kwenye ugavana. Kisii, Seneta Richard Onyonka tayari ametangaza wazi kuwa atapambana na Gavana Simba Arati mwaka 2027. "Ninagombea ugavana wa Kisii mwaka wa 2027, hilo ni jambo la uhakika," akasema Onyonka.
Mwelekeo huo unaonekana pia Magharibi mwa Kenya ambapo Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale wanalenga ugavana wa kaunti zao.
Orodha ya maseneta wanaowania ugavana pia inajumuisha James Murango (Kirinyaga), Kanar Seki (Kajiado), James Lomenen (Turkana), Danson Mungatana (Tana River), Abass Sheikh (Wajir), Fatuma Dullo (Isiolo) na Enoch Wambua (Kitui).
Kwa mujibu wa wachambuzi, maseneta tayari wana mamlaka ya kisiasa yanayoenea katika kaunti nzima, lakini ili wawe magavana, lazima washinde tena kura za wananchi na wapitie changamoto za uteuzi wa vyama, siasa za kikabila, fedha za kampeni na ushindani kutoka kwa walio madarakani.
Swali kuu linaloibuka ni: kwa nini mwanasiasa aache kiti alicho nacho tayari?
Mchambuzi wa siasa Javas Bigambo anasema wanasiasa wana haki ya kikatiba kuwania nyadhifa wanazotaka.
 Akizungumzia azma ya urais ya Ndindi Nyoro, alisema hakuna mtu au kundi lenye mamlaka ya kuzuia wengine kutumia haki zao za kisiasa.
"Hakuna mtu mwenye haki ya kumiliki eneo au wadhifa kisiasa kana kwamba ni mali yake binafsi," anasema Bigambo.
 Kisa cha Nyoro kinaonyesha hatari kubwa inayowakabili wanasiasa wanaoondoka katika ngome zao za kisiasa. Akiwa amejiondoa UDA na kuanzisha chama cha People's Party of Kenya, Nyoro ameonyesha nia ya kuwania urais na hata kudai kuwa anaweza kumshinda Rais Ruto mwaka 2027. Wachambuzi wanaonya kuwa uchaguzi wa 2027 unaweza kuwaacha viongozi wengi mashuhuri bila nyadhifa.


from Taifa Leo https://ift.tt/S7DOhLv
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post