Wapwani walalamikia ongezeko la vijana kutekwa na kupatikana Nairobi

VIONGOZI na wakazi wa Mombasa wameelezea wasiwasi kuhusu visa vya vijana kupotea, huku baadhi yao baadaye wakipatikana Nairobi na katika viunga vya jiji hilo.

Tukio la hivi majuzi lilihusisha wasichana wawili wenye umri wa miaka 16 na 17 ambao waliokolewa wikendi baada ya kudaiwa kuzuiliwa kwa zaidi ya wiki moja.

Wapelelezi kutoka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) sasa wanategemea ushahidi wa kieletroniki katika kesi ambapo mwanaharakati Caleb Ngwena anachunguzwa kwa madai ya ubakaji na ulanguzi wa watoto kuhusu kisa hicho.

Wasichana hao wawili waliokolewa katika eneo la Kasarani, Nairobi baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja.

Ngwena alifikishwa katika Mahakama ya Shanzu, iliyowaruhusu wapelelezi kumzuilia kwa wiki mbili ili kukamilisha uchunguzi wao.

Mahakama iliagiza azuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Mjambere, baada ya kukubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kwamba waathiriwa hao ni watu walio katika mazingira hatari na kwamba kumwachilia Ngwena kwa sasa kunaweza kuhatarisha ushahidi na kuingilia kati uchunguzi.

“Mahakama imeridhika kwamba polisi wamewasilisha sababu nzito na za msingi za kumzuia Ngwena ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi wao. Ombi hilo limekubaliwa na atazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mjambere kwa muda wa siku 14,” mahakama iliamua.

Wasichana hao ni wanafunzi wa Kidato cha Tatu na majirani katika mtaa wa Red Estate, Kiembeni.

Walitoweka usiku wa Agosti 25 na kusababisha mama zao kupiga ripoti katika Kituo cha Polisi cha Kiembeni siku iliyofuata.

Ngwena alikamatwa nyumbani kwake Kiembeni Septemba 2 na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Mjambere.

Polisi walisema alisafiri hadi Nairobi akiwa ameandamana na maafisa wa DCI Kisauni mnamo Septemba 3 katika juhudi za kuwatafuta wasichana hao.

Wasichana hao waliokolewa siku iliyofuata katika eneo la Kasarani, huku wachunguzi wakisema Ngwena alisaidia katika kuwapatia mahali walikokuwa.

Wasichana hao waliwaeleza wachunguzi kwamba walichukuliwa kwa nguvu na Ngwena pamoja na mwanamume mwingine usiku walipotoweka.

Walisema walilazimishwa kuingia katika gari ambalo hawakulitambua na kusafirishwa kutoka Kiembeni hadi Nairobi, kabla ya kupelekwa Kaunti ya Kiambu.

Inadaiwa walifungiwa katika chumba kimoja na kubakwa.

Wachunguzi sasa wanafuatilia mawasiliano na ushahidi wa kifedha uliofanyika kabla na baada ya wasichana hao kutoweka.

Polisi walisema kulikuwa na mawasiliano mengi pamoja na fedha zilizotumwa kwenda kwenye simu za wasichana hao.

Laini za simu walizotumia zilisajiliwa kwa majina ya mama zao.

Polisi wanataka kupata taarifa kutoka Safaricom kuhusu akaunti tano za M-Pesa kwa kipindi cha Julai 20 hadi Septemba 6.

Taarifa hizo zinajumuisha stakabadhi zilizotumika kufungua akaunti, taarifa za M-Pesa na rekodi za matumizi ya simu.

Pia, wanachunguza taarifa za akaunti tatu za Airtel Money pamoja na rekodi zinazohusiana na matumizi ya simu kwa kipindi hicho.

Mahakama iliwaruhusu wapelelezi kuchunguza simu nne zilizopatikana, ambazo ni Oppo A9 2020, Samsung Galaxy A04e, Calus W999 na simu ya Nokia.

Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) kimeruhusiwa kufikia simu hizo, kuchunguza yaliyomo na kutoa faili pamoja na programu zilizohifadhiwa kwenye vifaa hivyo.

Mpelelezi wa kesi hiyo John Andama, alisema muda wa ziada wa kumzuilia Ngwena ulihitajika ili kupata ripoti za kitabibu za wasichana hao, kuchanganua rekodi za simu na rekodi za fedha, kutoa taarifa kutoka kwenye simu hizo na kurekodi taarifa za mashahidi wengine.

Polisi pia walisema Ngwena anawasaidia katika juhudi za kuwakamata washukiwa wengine wanaohusishwa na kisa hicho.
Kupitia wakili wake, Ngwena alipinga kuzuiliwa kwake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Upande wa utetezi ulipinga ombi la polisi, ukilitaja kuwa na kasoro za kisheria, huku ukipinga maelezo ya polisi kuhusu safari zake na kukana madai kwamba ndiye aliyewaongoza maafisa hadi Nairobi.

“Ni polisi waliompeleka mshtakiwa Nairobi; si kwamba yeye ndiye aliyewaongoza hadi huko,” wakili huyo aliambia mahakama.

Hakimu alisema polisi wana wajibu wa kutoa sababu za msingi za kuendelea kumzuilia mshukiwa baada ya muda uliowekwa na Katiba.

Hata hivyo, mahakama ilisema polisi wamewasilisha sababu za msingi za kuendelea kumzuilia Ngwena, ikizingatia mazingira ya waathiriwa na umuhimu wa kulinda ushahidi.

Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Mombasa, Bi Zamzam Mohamed, alisema karibu visa 13 vya matineja kupotea vimeripotiwa tangu Agosti.

Aliwataka wazazi kuwa waangalifu na kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuzuia visa kama hivyo.

“Mambo si mazuri huku nje. Vijana wengi wanapotea, kwa hivyo ninawahimiza wazazi kuwachunga watoto wao kwa makini. Kaeni pamoja na watoto wenu, zungumzeni nao, eleweni changamoto zao,” alisema mwishoni mwa wiki iliyopita.

Waathiriwa wote wamepelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na ushauri nasaha, huku taarifa zikiwa zimechukuliwa kutoka kwa familia zao.



from Taifa Leo https://ift.tt/4VpJCwM
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post