Changamoto mpya mirengo mitatu ikizuka katika upinzani

UPINZANI nchini unaonekana kukabiliwa na changamoto mpya huku viongozi wakipanga mikakati tofauti ya kumwondoa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi mkuu wa 2027.  Mikakati ya kiongozi wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, anayeongoza vuguvugu la Linda Mwananchi, inaonekana kuwa na uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa siasa za upinzani. Hata hivyo, ushirikiano huo unaweza kuimarisha umoja au kuchochea makundi pinzani yanayowania uongozi wa nchi.  Kwa sasa, upinzani unaonekana kuunda mirengo mitatu ya kisiasa huku viongozi wakitofautiana kuhusu wakati wa kumteua mgombea urais, namna ya kuendesha kampeni na chama kitakachotumiwa katika uchaguzi.  Mrengo wa kwanza unahusisha kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democratic Party of Kenya (DP) Justin Muturi na kiongozi wa Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa. Watatu hao wamekuwa wakifanya mikutano ya pamoja katika miezi ya hivi majuzi.  Mrengo wa pili unajumuisha kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wa People’s Party of Kenya (PPK) na kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) Martha Karua. Watatu hao wameanza kuonekana pamoja katika mikutano ya kisiasa, wakikosoa utawala wa Rais Ruto.  Hapo jana viongozi hao walikuwa Nakuru wakieneza ujumbe wa kupinga serikali ya Kenya Kwanza.  Kundi la tatu linaweza kuundwa na Gachagua na Sifuna, ambao wameanza mazungumzo kuhusu ushirikiano kuelekea uchaguzi wa mwaka ujao. Mnamo Jumanne, Sifuna alifanya ziara ya kushtukiza katika makazi ya Gachagua ya Wamunyoro, Nyeri, ambapo walijadili uwezekano wa kuunganisha nguvu zao.  “Tulikuwa na mazungumzo ya wazi na ya kujenga kuhusu ukombozi wa nchi yetu na kuunda utawala wa sita,” alisema Gachagua baada ya mkutano huo.  Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, mshirika wa karibu wa Sifuna, alisema mkutano huo ni ishara kuwa viongozi wa upinzani wanaweza kuungana.  “Njia pekee ya kushinda serikali hii ni umoja. Idadi ya wafuasi wanaoungwa mkono na viongozi hao wawili inaonyesha kuwa mshindi wa uchaguzi huu anaweza kupatikana katika duru ya kwanza,” alisema Natembeya, akiongeza kuwa mazungumzo yataendelea ili kutafuta uungwaji mkono kutoka maeneo mengine.  Hata hivyo, tofauti kuhusu jinsi ya kuchagua mgombea urais zimezua mashaka kuhusu uwezekano wa viongozi hao kukubaliana.  Kalonzo na Muturi wanataka mgombea atangazwe mapema ili upinzani uwe na muda wa kujiandaa. Kwa upande mwingine, Gachagua na Linda Mwananchi wanataka viongozi wajenge kwanza vuguvugu la kitaifa kwa kuunganisha misingi yao ya kisiasa.  Muturi alikiri kuwa kujenga muungano si jambo rahisi, lakini akasema viongozi wana nia ya kushinda changamoto zinazowakabili.  “Muungano wa kisiasa haujawahi kuwa rahisi popote, na hatutarajii kuwa jambo jepesi hapa Kenya. Tumejitolea kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza,” alisema.  Aliongeza kuwa lengo lao ni kumuondoa Ruto madarakani kwa njia ya kidemokrasia na kurejesha utawala unaoheshimu Katiba, utawala bora na sheria.  Nyoro pia alikanusha madai kuwa upinzani umegawanyika, akisema viongozi wanatumia njia tofauti kufikia lengo moja.  “Hatujagawanyika. Tumeungana kwa lengo la kumuondoa Rais Ruto mamlakani,” alisema.  Alisema hawatakimbilia kumtangaza mgombea urais kwa sababu mchakato huo unahitaji kuzingatia mambo mengi. Kwa maoni yake, upinzani ukiungana na kuwasilisha mgombea mmoja, utakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda.  Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mshirika wa Kalonzo, pia alipuuzilia mbali uwezekano wa makundi hayo kubaki yakiwa tofauti katika uchaguzi ujao. Alisema hivi karibuni Wakenya wataanza kuona mikutano itakayowaleta pamoja viongozi wa Wiper, DCP, Linda Mwananchi, DAP-K, DP na vyama vingine washirika.  Lakini Naibu Kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema ukosefu wa kuaminiana, kusalitiana na hila ni baadhi ya vikwazo vinavyoweza kuvuruga mipango ya upinzani.  Alisema baadhi ya viongozi wana uwezo wa kuvutia wapiga kura lakini hawana uungwaji mkono wa kutosha kuongoza nchi, huku wengine wakikabiliwa na tatizo la kukosa imani ya wananchi.  Mbali na tofauti za kitaifa, ushindani wa kupata ushawishi katika eneo la Mlima Kenya umeongeza mgawanyiko.  DCP, Jubilee, PLP, DP, Party of National Unity (PNU) inayoongozwa na Peter Munya na Devolution Empowerment Party (DEP) ya Lenny Kivuti ni miongoni mwa vyama vinavyowania uungwaji mkono katika eneo hilo lenye ushawishi mkubwa katika siasa za nchi.  Mvutano umeongezeka tangu Nyoro azindue PPK mnamo Agosti 17 na kuanza kampeni za kujijengea msingi wa kisiasa kote nchini, pamoja na Mlima Kenya.  Baadhi ya viongozi wa DCP wamemlaumu Nyoro kuwa “fuko”, madai ambayo yanalenga kuonyesha kuwa anatumiwa kuhujumu upinzani. Seneta wa Nyandarua John Methu hata amekiita chama cha Nyoro “wilibaro ya kijani”, akijaribu kukihusisha na UDA.  Nyoro amepuuzilia mbali madai hayo, akisema ni kampeni ya kumchafua yeye na chama chake.  “Hatuna muda wa kujibu mashambulizi na uongo wa kitoto. Anayetuma watu hao aseme moja kwa moja, nasi tutajibu ipasavyo,” alisema.  Akiwa Kajiado wiki iliyopita, Nyoro alisema wanaomshambulia wanahofia kuongezeka kwa ushawishi wake wa kisiasa. Ushirikiano wake wa hivi karibuni na Matiang’i katika mikutano ya pamoja umeongeza dhana kuwa wawili hao wanaunda mhimili tofauti ndani ya upinzani.  Ilivyo kwa sasa, changamoto kubwa inayowakabili viongozi wa upinzani si kupata tu mgombea anayeweza kumshinda Ruto, bali pia kukubaliana kuhusu mchakato wa uteuzi ambao utawafanya wagombea wengine kuunga mkono mshindi bila kuhisi wamesalitiwa au kushindwa kisiasa     

from Taifa Leo https://ift.tt/iAkgSuM
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post