
KIONGOZI wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka ameonyesha kwa mara nyingine kuwa yuko tayari kuwania urais mwaka 2027 baada ya kuanza hatua rasmi za kujenga chapa yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi huo mkuu.
Bw Musyoka ameomba kusajili rasmi kauli mbiu “Kalonzo 2027” kama nembio, hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya wazi ya kampeni yake ya urais huku akijaribu kujiimarisha ndani ya muungano wa upinzani unaotafuta mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto.
Usajili wa chapa hiyo unaonyesha kuwa Kalonzo ameanza kuweka msingi wa kisiasa na kimkakati wa kampeni zake huku viongozi wa upinzani wakiendelea kujadiliana kuhusu nani atapeperusha bendera ya pamoja mwaka 2027.
Muungano huo wa upinzani unajumuisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Eugene Wamalwa wa DAP-K, Martha Karua wa People’s Liberation Party (PLP), Fred Matiang’i wa Jubilee pamoja na Justin Muturi wa Democratic Party (DP).
Mbali na Kalonzo, viongozi wengine waliotangaza wazi nia ya kuwania urais ni Gachagua, Martha Karua na Eugene Wamalwa, ingawa wote wameahidi kuwa tayari kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani atakayekubalika.
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amemuidhinisha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kama mgombea urais anayempendelea.
Akizungumza Ijumaa katika mazishi ya mama yake Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Martha Karua alisema viongozi wa upinzani wataendelea kujitambulisha kama wagombea wa urais lakini hatimaye wataungana nyuma ya mgombea mmoja.
“Tutaendelea kujitokeza kama wagombea wa urais mbele ya wananchi, lakini mwishowe tutaungana na kuwa na mgombea mmoja wa upinzani,” alisema Karua.Kwa mujibu wa kura ya maoni ya kampuni ya Trends and Insights for Africa (Tifa) iliyotolewa wiki hii, Kalonzo ndiye mgombea wa pili anayependwa zaidi na Wakenya kwa sasa baada ya Rais Ruto.
Katika kura hiyo, Rais Ruto alipata asilimia 24 huku Kalonzo akifuata kwa asilimia 19 na Dkt Matiang’i akiwa wa tatu kwa asilimia 14.
Mnamo Oktoba 2025, chama cha Wiper kilimuidhinisha rasmi Kalonzo kuwania urais katika mkutano wa wajumbe wa kitaifa uliofanyika Uhuru Park jijini Nairobi.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua, ambaye ni mshirika wa karibu wa Kalonzo, alisema mengi yanaendelea nyuma ya pazia tangu kiongozi huyo apewe idhini ya kuwania urais.
“Katika kiwango cha chama tayari ameteuliwa rasmi kuwania urais. Idhini hiyo imemruhusu kuanza maandalizi ikiwemo kuunda afisi ya kampeni,” alisema Wambua.
Aliongeza kuwa Kalonzo anaendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali ndani ya upinzani na kwamba wengi wanaona ndiye mgombea anayefaa zaidi kumzuia Rais Ruto kushinda muhula wa pili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika jarida la Taasisi ya Haki Miliki Kenya (Kipi), ombi la kusajili chapa ya “Kalonzo 2027” tayari limekubaliwa isipokuwa lipingwe ndani ya siku 60 zijazo.
Iwapo halitapingwa, Kalonzo atamiliki rasmi chapa hiyo kwa miaka 10 ijayo.Jarida hilo linaonyesha kuwa Kalonzo anataka matumizi ya kipekee ya maneno hayo katika matangazo ya kampeni na shughuli nyingine za kisiasa.
Nembo hiyo pia imeundwa kwa rangi ya bluu na nyekundu, jambo ambalo linaonekana kuashiria mwelekeo wa kampeni zake za kisiasa.
Katika mahojiano ya awali, Kalonzo alisema kuachana tena na azma yake ya urais mwaka 2027 kutamaanisha kustaafu siasa kutokana na umri wake wa miaka 72.
“Nikikosa kuwania urais mwaka 2027 basi nitakuwa ninaenda nyumbani kabisa. Hilo si jambo ambalo niko tayari kufanya,” alisema.
Kalonzo aliwania urais mwaka 2007 na baadaye akawa Makamu wa Rais katika serikali ya muungano ya marehemu Mwai Kibaki na Raila Odinga kati ya 2008 na 2013.
Katika uchaguzi wa 2013, 2017 na 2022 aliacha azma yake ya urais kumuunga mkono Raila Odinga.
Mwaka 2013 na 2017 alikuwa mgombea mwenza wa Raila lakini mwaka 2022 nafasi hiyo ilipewa Martha Karua.
Wachambuzi wa siasa wanasema nafasi ya Kalonzo katika siasa za upinzani bado ni kubwa lakini mustakabali wake utategemea sana hatua za Rigathi Gachagua.
Profesa David Monda alisema Kalonzo anaweza kuwa chaguo bora zaidi kwa upinzani iwapo viongozi wengine wataungana nyuma yake.
Hata hivyo, alisema vijana wengi wanaotarajiwa kuwa sehemu kubwa ya wapigakura mwaka 2027 wanaweza kutaka viongozi wapya badala ya kizazi cha zamani cha wanasiasa.
Naye Profesa Masibo Lumala alisema nafasi ya Kalonzo inaweza kuimarika iwapo Gachagua hataidhinishwa kugombea kutokana na changamoto zake za kisheria kufuatia kuondolewa mamlakani.
“Ikiwa Gachagua ataruhusiwa kugombea, hali ya kisiasa itabadilika kabisa. Lakini akiwa nje ya kinyang’anyiro, Kalonzo anaweza kuwa sura ya kuunganisha upinzani,” alisema Lumala.
from Taifa Leo https://ift.tt/q3LuYdZ
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS