
KIONGOZI wa DCP, Rigathi Gachagua, jana alirejea nchini kimya kimya baada ya ziara ya miezi miwili Amerika.
Katika mkutano wake wa kwanza wa hadhi ya juu baada ya kurejea, Bw Gachagua alikutana na mrengo wa Linda Mwananchi unaoongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, huku juhudi za kupata mgombea mmoja wa urais zikishika kasi.
Duru kutoka kwa kambi ya Bw Gachagua zilisema mkutano huo ulikuwa hatua ya makusudi ya kuonyesha umoja kati ya eneo la Mlima Kenya na mrengo wa Linda Mwananchi.
“Huu ni wa kwanza katika mfululizo wa mikutano na atakayefuata kukutana naye ni Kalonzo Musyoka, kisha wote watatu watahutubia mkutano wa pamoja wa kisiasa. Kuna jambo linaloendelea kwa makusudi, na yote ni katika juhudi za kuonyesha kuwa upinzani hauwezi kuendelea kukwepa suala la kuwa na mgombea mmoja wa urais,” duru hizo zikaarifu.
Bw Gachagua aliandika kwenye mitandao ya kijamii: “Karibuni katika makazi ya Wamunyoro, binamu zangu kutoka Linda Mwananchi. Tunapoungana, mambo makubwa lazima yatokee.”
“Jiandaeni kwa mshangao mkubwa kwa sababu mambo yanaendelea chini kwa chini. Hivi karibuni tutakuwa na mgombea mmoja, manifesto ya pamoja na mikakati ya pamoja ya kumkabili rais aliye mamlakani, ambaye ni lazima tumwondoe madarakani kwa njia ya kidemokrasia 2027, akasema Gavana wa Trans Nzoia, Bw George Natembeya kwenye mahojiano na
Taifa Leo.
Bw Sifuna aliandamana na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Pauline Njoroge, Faith Odhiambo, Reuben Ndolo miongoni mwa viongozi wengine
Bw Gachagua sasa atakumbatia jitihada za kuimarisha uungwaji mkono wake eneo la Mlima Kenya, kutatua migogoro ndani ya chama chake na kushawishi upinzani kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Gachagua aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mapema jana siku ya Mashujaa, kabla ya kuelekea moja kwa moja nyumbani kwake Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri.
Alirejea kimya kimya, tofauti na Agosti 2025, alipokabiliwa na vurugu wakati wa ziara yake ya awali kutoka Amerika. Makundi ya watu wenye silaha yalishambulia msafara wake kwa mawe kwenye Barabara ya Mombasa, na kujeruhi wafuasi wake na kumlazimisha kuahirisha mkutano wa Kamukunji.
Safari hii, hakukuwa na msafara mkubwa wala umati wa wafuasi, lakini changamoto za kisiasa zinazomsubiri ni kubwa.
Bw Gachagua alikatiza mkutano wa kisiasa wa siku 15 aliokuwa amepanga kufanya katika ranchi yake Texas, Amerika, baada ya siku 10.
Alisema wafuasi wake nchini walikuwa wamemhimiza kurejea na kuongoza kampeni za upinzani dhidi ya azma ya Rais William Ruto kuwania muhula wa pili.
Katibu Mkuu wa DCP, John Methu, alisema sasa watamakinikia kuimarisha chama, kuandaa wagombeaji wa uchaguzi wa 2027 na kujadiliana kuhusu mgombea mmoja wa urais.
from Taifa Leo https://ift.tt/4p8umBH
via
IFTTT