Kazeni mshipi: Bei za mafuta zaongezeka tena

MAMLAKA ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) imeongeza bei ya bidhaa za mafuta katika hatua ambayo imeamsha hisia mseto na kuashiria siku ngumu zijazo kwa Wakenya. Kutokana na hatua hiyo, bei mpya mafuta ya Super Petroli sasa ni Sh226.96 kwa lita, Sh227.85 kwa dizeli na Sh219.87 kwa mafuta ya taa jijini Nairobi. Bei ya mafuta ya taa imeongezeka kwa Sh28.49 huku petroli ikipanda kwa Sh12.93 na dizeli kwa Sh9.90 kwa kila lita. Ongezeko hilo la bei ya bidhaa za mafuta limechangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo machafuko yanayoendelea Mashariki ya Kati kuhusiana na vita vya Israel na Amerika dhidi ya Iran, kulingana na Mkurugenzi wa EPRA, Edward Mwirigi. Aidha, uamuzi wa serikali kusitisha ruzuku ya mafuta umechangia ongezeko la bei. “Septemba imekuwa mwezi mbaya zaidi tangu vita vilipozuka,” alisema Bw Mwirigi akihutubia vyombo vya habari. Alifafanua kuwa hatua ya kupunguza ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 16 hadi nane itaendelea kutekelezwa hadi Januari 14 ili kuwalinda Wakenya dhidi ya gharama kubwa za mafuta. Hata hivyo, hatua hiyo huenda isitoshe kuzuia athari za kupanda kwa bei ya mafuta duniani, ambazo tayari zinatishia kuongeza gharama ya maisha nchini. Bei ya mafuta ghafi ya Brent ilipanda na kuvuka Dola 100 kwa pipa mwezi uliopita, huku ikiuzwa kwa Dola 105.98 Jumatano, kutokana na misukosuko iliyotokana na vita Mashariki ya Kati. Mapigano hayo yamevuruga usambazaji wa mafuta baada ya Iran kushambulia miundomsingi muhimu katika eneo la Ghuba, ikiwemo mitambo ya kusafisha mafuta na mabomba ya kusafirisha mafuta. Mafuta ghali yanatarajiwa kuongeza gharama za usafiri, kilimo na uzalishaji viwandani, huku wafanyabiashara na watoa huduma wakitarajiwa kuhamishia gharama hizo kwa wateja.  Dizeli ni muhimu katika kuendesha uchumi wa Kenya kwa kuwa hutumika katika magari ya uchukuzi wa umma, mitambo ya kilimo na viwanda. Wakati huo huo, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 6.8 mwezi uliopita, kiwango cha juu zaidi tangu Januari 2024, wakati ulipokuwa asilimia 6.9. Serikali pia imeonya kuwa hazina ya ruzuku ya mafuta imekuwa ikipungua kwa kasi kutokana na gharama kubwa ya kudhibiti bei. Ruzuku hiyo hugharimiwa kupitia Ushuru wa Ustawi wa Petroli, unaotozwa kwa bidhaa za mafuta. Hali hii inazua wasiwasi kuwa Wakenya huenda wakakabiliwa na ongezeko zaidi la bei za bidhaa muhimu na huduma katika siku zijazo

from Taifa Leo https://ift.tt/S59xqXj
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post