
RAIS William Ruto ameanzisha kampeni za kuimarisha uungwaji mkono wake katika Bonde la Ufa, akilenga kuongeza idadi ya wapiga kura kutoka 5.4 milioni waliojisajili mwaka 2022 hadi zaidi ya milioni saba kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na malalamishi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kwamba Rais amewapuuza kwa miaka minne na sasa amerejelea akitafuta uungwaji mkono kwa muhula wa pili.
Washirika wake wanahofia kuwa kutoridhika kwa wapiga kura kunaweza kusababisha wengi kukosa kujitokeza kupiga kura, hali inayoweza kuathiri juhudi zake za kuchaguliwa tena.
Rais pia anakabiliwa na kupungua kwa uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya, ambalo lilichangia pakubwa ushindi wake wa 2022. Wakati huohuo, anatafuta kuimarisha uhusiano na maeneo yaliyokuwa ngome za aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, yakiwemo Nyanza, Magharibi, Pwani na Nairobi.
Wabunge wanasema zaidi ya wakazi 1.8 milioni wa Bonde la Ufa hawajajisajili kupiga kura, huku wengi wakikosa vitambulisho vya taifa.
“Urais hushindaniwa kwa kura. Tuna uwezo wa kusajili wapiga kura zaidi ya milioni saba. Tafadhali pateni vitambulisho na mjisajili kupiga kura,” alisema Rais alipokuwa Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.
Hii ni mara ya pili ndani ya mwaka mmoja kwa Rais kuwataka wakazi wa Bonde la Ufa kupata vitambulisho na kujisajili. Awali alitoa ombi hilo katika kaunti za Bomet na Narok.
Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei, amesema uchaguzi wa 2027 utakuwa na ushindani mkubwa, akiwataka wafuasi wa Rais kuhakikisha wanajiandaa mapema.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, amesema chama cha UDA kinahamasisha wakazi wote wanaostahili kujiandikisha ili washiriki uchaguzi.
Katika uchaguzi wa 2022, Bonde la Ufa lilikuwa na wapiga kura 5.34 milioni waliojisajili. Ruto alipata kura milioni 2.6, huku Raila akipata takriban 1.1 milioni, hasa kutoka Narok, Kajiado na Turkana.
Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinaonyesha kuwa wapiga kura wapya 671,958 walikuwa wamejisajili katika eneo hilo wakati wa zoezi la mwaka huu. Bonde la Ufa liliongoza kwa idadi ya waliojisajili, likifuatiwa na Mlima Kenya lililokuwa na wapiga kura wapya 399,220.
Katika ziara yake ya siku 10 Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Rais amekuwa akizindua na kutangaza miradi ya barabara, afya, umeme, masoko na nyumba za gharama nafuu, huku akiwaomba wakazi kumuunga mkono kwa muhula wa pili.
Hata hivyo, chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kinaimarisha shughuli zake katika baadhi ya maeneo, yakiwemo Nakuru na Narok. Seneta wa Kajiado Samuel Seki na Mbunge wa Kajiado Kaskazini Onesmus Ngogoyo ni miongoni mwa viongozi waliojiunga na Gachagua.
Vincent Rotich, kiongozi wa DCP eneo la Emurua Dikirr, anasema ushindi wa chama hicho katika kiti cha uwakilishi wadi cha Narok Town na kupata zaidi ya kura 10,000 katika uchaguzi mdogo wa Emurua Dikirr kumezua wasiwasi serikalini.
Mchambuzi wa siasa Profesa Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana anasema wito wa Rais kwa wakazi kupata vitambulisho na kujisajili kupiga kura ni sehemu ya maandalizi ya mapema ya uchaguzi.
Anasema ushindani unaanza kutoka matamshi ya kisiasa hadi mikakati ya kusajili na kuhamasisha wapiga kura.
Ruto pia analenga maeneo yanayozungumza lugha ya Maa na Turkana, ambayo yalimuunga mkono Raila katika chaguzi zilizopita. Amechukua hatua kama kukabidhi usimamizi wa Hifadhi ya Wanyamapori ya Amboseli kwa Kaunti ya Kajiado na hati ya umiliki wa Msitu wa South West Mau kwa Kaunti ya Narok.
Hata hivyo, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, wakiwemo Seneta Seki na Mbunge Ngogoyo, wanaohusishwa na Gachagua.
Katika Kaunti ya Baringo, mvutano kati ya Rais na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi pia unaongeza changamoto za kisiasa kwa UDA.
Hivyo, kurejea kwa Ruto Bonde la Ufa kunahusu zaidi ya kutangaza miradi ya maendeleo. Ni juhudi za kuimarisha ngome yake ya kisiasa, kuongeza idadi ya wapiga kura waliojisajili na kukabiliana na upinzani unaojaribu kujipenyeza katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome yake.
from Taifa Leo https://ift.tt/WE4tOYl
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS