
KUMBUKUMBU ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga ilikumbwa na suintofahamu Alhamisi baada ya baadhi ya vigogo wa chama hicho na Rais William Ruto kukosa kuhudhuria hafla iliyofanyika Migwena, Bondo, kaunti ya Siaya.
Kutohudhuria kwa viongozi hao kulizua maswali kuhusu mgawanyiko ndani ya ODM na uhusiano wake na serikali jumuishi ya Rais Ruto, huku mirengo pinzani ikizozana kuhusu urithi wa kisiasa wa Raila na mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, naibu kiongozi wa chama Abdulsamad Nassir na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed walikuwa miongoni mwa viongozi wakuu waliokosekana katika hafla hiyo.
Vyanzo vya ndani ya chama vilisema baadhi ya maafisa hawakufurahishwa na mpangilio wa sherehe, ambao waliamini uliwapa nafasi kubwa viongozi wa upinzani, wakiwemo wale wanaohusishwa na kundi la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Rais Ruto naye hakuhudhuria hafla hiyo, licha ya serikali yake kusaidia mazishi ya kitaifa ya Raila na ujenzi wa kaburi lake Kang’o Ka Jaramogi.
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pia hakuhudhuria hafla hiyo.
Vyanzo vya serikali vilisema Rais alijiondoa baada ya kubainika kuwa viongozi wa upinzani wangekuwa na nafasi kubwa katika sherehe hizo.
Kutokuwepo kwa vigogo hao kulijiri huku mjane wa Raila, Mama Ida Odinga, akiwakaribisha viongozi wa upinzani katika shamba la familia la Opoda kabla ya kuelekea Migwena.
Linda Mwananchi ilipokelewa Opoda, hatua iliyozidisha mjadala kuhusu iwapo kumbukumbu ya Raila ilipaswa kuwa hafla ya ODM pekee au jukwaa la kuwakutanisha viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa.
“Siasa ni ushawishi, si udikteta kama tunavyoshuhudia hapa. Raila alitufundisha kuweka maisha ya wananchi mbele tunapofanya maamuzi,” alisema Sifuna.
Bw Orengo alisema upinzani utaungana nyuma ya mgombea mmoja ili kumshinda Rais Ruto, akitaja ukosefu wa ajira kuwa mojawapo ya changamoto zinazowakabili Wakenya
Mama Ida alitetea uamuzi wa kuwapokea viongozi kutoka mirengo yote, akisema Raila alikuwa wa Wakenya wote na urithi wake haupaswi kufungwa ndani ya chama kimoja.
Mvutano huo ulijitokeza wazi uwanjani, ambapo wafuasi wa mirengo tofauti walizozana na baadhi ya vijana kujaa katika hema la wageni waalikwa. Hali hiyo ilivuruga baadhi ya shughuli za hafla.
Huku viongozi wanaounga mkono ushirikiano na serikali wakitetea mwelekeo huo, wanasiasa wa upinzani walisisitiza kuwa njia bora ya kumuenzi Raila ni kuunganisha nguvu na kumwondoa Rais Ruto madarakani mwaka 2027.
Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati aliwaambia wanaofikiria kuondoka chama hicho kuwa wako huru kufanya hivyo, akisisitiza kuwa ODM bado ina nguvu katika Nyanza.
Huku baadhi ya viongozi wakisisitiza kuwa urithi wa Raila unapaswa kulindwa ndani ya ODM na kwa kushirikiana na serikali, wengine walisema njia bora ya kumuenzi ni kuunganisha upinzani na kumuondoa Rais Ruto madarakani mwaka ujao.
Mvutano huo ulijitokeza wiki kadhaa kabla ya sherehe hizo, huku familia ikiunda kamati ya kitaifa ya kuratibu kumbukumbu za Raila, iliyoongozwa na Profesa Adams Oloo na kusaidiwa na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, ODM ilianzisha sherehe za mwezi mzima za Mwezi wa Baba.
Miongoni mwa viongozi wa upinzani waliohudhuria ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Seneta Godfrey Osotsi na kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi.
Kutokuwepo kwa baadhi ya vigogo na mvutano uliojitokeza vilifanya kumbukumbu hiyo kuwa zaidi ya hafla ya maombolezo, huku maswali kuhusu umoja wa ODM na urithi wa Raila yakitawala mazungumzo kuelekea uchaguzi wa 2027.
from Taifa Leo https://ift.tt/OsEfPnZ
via IFTTT