
KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, anatarajiwa kurejea nchini wiki ijayo baada ya ziara ya takriban miezi miwili Amerika, wakati ambapo anakabiliwa na changamoto zinazoweza kuathiri mwelekeo wa safari yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Gachagua aliondoka Kenya Agosti 26 na ametembelea majimbo mbalimbali yakiwemo Spokane, Portland, Kansas, Dallas na Boston.
Alimaliza mikutano yake na Wakenya wanaoishi ughaibuni Oktoba 9, kabla ya kutangaza kuwa angeendelea na mashauriano ya kisiasa kwa siku nyingine 15 katika shamba lake la kibinafsi Texas.
Alipoulizwa tarehe ya kurejea, alisema hakuwa ameamua siku kamili, ingawa alikuwa amefunga virago na Wakenya walikuwa wakimtaka aharakishe kurejea kwa sababu, kwa maoni yao, msukumo wa upinzani ulikuwa ukipungua.
Atakaporejea, atakuta serikali imeongeza shughuli zake za kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, ngome ambayo DCP inajaribu kupata uungwaji mkono mkubwa.
Mbunge wa Naivasha Jane Kihara, mshirika wa karibu wa Gachagua, anadai serikali ina mikakati mitano ya kupunguza ushawishi wake katika eneo hilo.
Mikakati hiyo, alisema, ni kugawanya umoja wa Mlima Kenya kupitia vyama na viongozi inaofadhili; kutoa zawadi au miradi ya kisiasa ili kupata uungwaji mkono; kutumia vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya kupinga kampeni za DCP; kuongeza shughuli za Naibu Rais Kithure Kindiki, hasa Mlima Kenya Magharibi; na kumjenga Mbunge George Kariuki katika siasa za eneo hilo.
Gachagua pia atarejea akikabiliwa na wito wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), iliyomtaka kufika mbele yake Agosti 27 kujibu madai ya matamshi ya chuki.
Kupitia kampuni ya mawakili ya Kiragu Wathuta, alikataa kufika, akisema alikuwa na safari ya nje iliyopangwa kuanzia Agosti 26 hadi Oktoba 20.
Tume hiyo ilitaja matamshi aliyotoa Februari 23 katika Uwanja wa Gusii, Kisii; Juni 12 Luanda, Kaunti ya Vihiga; na wakati wa ziara yake Meru kati ya Julai 25 na 28.
Bado haijulikani ikiwa Gachagua atafika mbele ya tume hiyo na hatua zitakazochukuliwa iwapo atakosa kufanya hivyo.
Changamoto nyingine ni mizozo ya ndani ya chama chake, ambapo hatua za kinidhamu na malalamishi kuhusu uteuzi zimeibua maswali kuhusu umoja wake.
Mwaniaji wa ubunge wa Gichugu Njeri Mbogo amesimamishwa kwa siku 180 kutokana na madai ya kuhusika katika tukio ambapo chupi za wanawake zilizokuwa na majina ya Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango na Mwakilishi wa Wanawake Njeri Maina zilionyeshwa na waandamanaji.
Maina alidai chupi hizo zililetwa kwa nia ya kumchafua kisiasa.
Mwenyekiti wa watu mashuhuri wa chama cha DCP, Maina Kamanda, alidai chama hicho kimeingiliwa na watu wanaofanya kazi kwa niaba ya serikali na akaonya kuwa hawatapewa tiketi za uteuzi.
Kiongozi wa vijana kaunti ya Kiambu Isaac Mungai pia alifukuzwa kwa sababu za kinidhamu baada ya kutofautiana na Seneta Karungo Thang’wa na kuonekana kumuunga mkono Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
Wakati huohuo, chama hicho kimemuonya Seneta wa Nakuru Tabitha Keroche dhidi ya kuendesha shughuli zake nje ya miundo ya chama baada ya kuondoka UDA Oktoba 9, 2026, akilenga kiti cha ugavana wa Nakuru.
Baadhi ya wanaowania nyadhifa wameibua malalamishi kuhusu haki katika uteuzi, wakidai viongozi wakuu wamekuwa wakionyesha upendeleo kwa wagombeaji fulani kabla ya mchakato rasmi.
Gachagua pia atalazimika kukabiliana na mjadala kuhusu kuunda muungano wa upinzani na wakati wa kutangaza mgombeaji mmoja wa urais.
Amesisitiza kuwa DCP inapaswa kwanza kujenga miundo yake katika kaunti, kuimarisha uanachama na kujitambulisha kabla ya kuingia katika muungano rasmi.
Pia amependekeza kuwa mgombeaji wa pamoja wa upinzani atangazwe Mei 2027, akisema tangazo la mapema litampa Rais William Ruto nafasi ya kumlenga na kudhoofisha kampeni zake.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani, akiwemo Kalonzo Musyoka, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi, wametaka jina hilo litangazwe mapema.
DCP pia inakabiliwa na mahitaji makubwa ya tiketi za uteuzi, huku kamati ya fedha ya chama ikisema inahitaji takriban Sh5 bilioni kwa bajeti yake.
Kaimu Katibu wa DCP John Methu hata hivyo amepuuzilia mbali hofu kuhusu changamoto hizo, akisema Gachagua ni mwanasiasa aliyejijenga na amewahi kukabiliana na changamoto kubwa, ikiwemo kuondolewa madarakani kama naibu rais.
Alisema Gachagua atarejea akiwa na nguvu mpya kuendeleza ajenda yake ya kisiasa na kushughulikia masuala yaliyoibuka akiwa ughaibuni.
from Taifa Leo https://ift.tt/NtqSVps
via
IFTTT