Walimu kuendelea kufurahia mitandao ya kijamii, TSC yapata pigo

WALIMU chini wataendelea kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii bila hofu ya kuadhibiwa baada ya korti kukataa ombi la Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) la kuondoa agizo lililosimamisha utekelezaji wa mwongozo wenye utata kuhusu machapisho yao mtandaoni.

Jaji Francis Kyambia alisema barua ya TSC haikufafanua wazi mienendo inayochukuliwa kuwa isiyo ya kitaaluma, hivyo kuwaweka walimu katika hatari ya kuadhibiwa kwa kutoa maoni kuhusu masuala ya umma.

“Barua hiyo haifafanui vya kutosha mienendo inayoweza kumfanya mwalimu kuchukuliwa hatua za kinidhamu,” akasema jaji huyo.

Mgogoro huo unatokana na barua ya Agosti 13, 2026, iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa TSC Evaleen Mitei, iliyowatahadharisha walimu dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni na tabia isiyo ya kitaaluma kwenye mitandao ya kijamii.

Mwalimu Fredrick Ochieng aliwasilisha kesi akisema mwongozo huo ulikuwa na lugha tata inayoweza kuingilia uhuru wa walimu kutoa maoni yao kuhusu sera za elimu, utawala na mazingira ya kazi.

Pia alilalamikia kutoshirikishwa kwa walimu na wadau wengine kabla ya kutolewa kwa ilani hiyo.

TSC ilisema waraka huo haukuanzisha makosa mapya bali uliwakumbusha walimu wajibu wao chini ya sheria na kanuni zilizopo.

Ilisema ilichukua hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa matumizi mabaya ya mitandao na kwamba haikulenga kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Hata hivyo, Jaji Kyambia alisema vikwazo vya uhuru wa kujieleza lazima viwe na msingi wa kisheria na vikidhi masharti ya Katiba.

Alisema TSC ilipaswa kushauriana na wadau na kutoa miongozo mahususi badala ya barua ya jumla. Aliongeza kuwa walimu wanaokiuka maadili wanapaswa kushughulikiwa mmoja mmoja chini ya kanuni zilizopo.

Agizo la kusimamisha barua hiyo litaendelea kutumika hadi kesi hiyo iamuliwe. Kesi hiyo itatajwa Februari 3, 2027.



from Taifa Leo https://ift.tt/f2JLIGz
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post