
HAKIMU Dolphina Alego amekataa kujiondoa katika kesi ya ulaghai wa shamba la thamani ya Sh1.35bilioni dhidi ya aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa Mkoa wa Nairobi (DPC) Davis Nathan Chelogoi. Bi Alego alisema Chelogoi ameshindwa kuthibitisha madai kwamba amekua akimwonea wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo. Akikataa kusitisha kusikizwa kwa kesi hiyo na kuamuru isikizwe na hakimu mwingine, Bi Alego alisema Oktoba 31,2025 kwamba “malalamishi ya Chelogoi kwamba hatapata haki hayana mashiko kisheria.” Hakimu alisema tangu Chelogoi ashtakiwe Bw Chelogoi ameshtakiwe pamoja na aliyekuwa naibu mkurugenzi idara ya mipango wizara ya ardhi Bw Andrew Aseri Kirungu amekuwa akiwasilisha maombi ya kila aina. Hakimu alisema DPC huyo alikwepa kortini mwaka 2023 huku akiimbua kila sababu. “Chelogoi alikwepa kufika kortini kujibu mashtaka akisema ni mgojwa na amelazwa katika Nairobi Hospital,” Bi Alego alisema katika uamuzi aliokataa kujiondoa katika kesi hiyo. Hakimu huyo alisema inashangaza kwamba Chelogoi aliyeshtakiwa pamoja  na afisa wa zamani wa  idara ya ardhi Andrew Kirungu amewasilisha ombi hilo baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi na kuwekwa kizimbani kujitetea. Mnamo Julai 2025 Bi Alego alifikia uamuzi Chelpogoi na Kirungu wako na kesi ya kujibu. Chelogoi aliwekwa kizimbani kujitetea katika kesi hiyo ya kunyakua shamba lao wafanyabiashara Ashok Rupshi Shah na Hitenkumar Amritlal Raja. Shamba hilo liko eneo la Lower Kabete kaunti ya Nairobi. Bw Chelogoi anakabiliwa na mashtaka saba ya ulaghai na unyakuzi wa shamba hilo. Katika ombi la kutaka Bi Alego ajiondoe kwenye kesi hiyo Chelegoi alidai hakimu huyo anamwonea na kwamba ameamua atamfunga jela. Katika uamuzi wake Bi Alego alisema kuwa madai ya DPC huyo hayana msingi kisheria. “Kabla ya mlalamishi kudai Jaji au Hakimu hafai kusikiza kesi lazima ushahidi utolewe kuthibitisha kwamba yuko na upendeleo na ni muhusika mkuu katika kesi anayoisikiza,” Bi Alego alisema. Hakimu huyo pia alisema tume ya kuajiri watumishi katika idara ya mahakama (JSC) imeweka sheria zinazowathibiti majaji na mahikumu wanapotekeleza majukumu yao. Hakimu alisema Chelogoi hakuthibitisha kwa kuwasilisha ushahidi hatapata haki kesi hoyo ikiendelea na kuamuliwa naye. “Madai ya Chelogoi hayana mashiko kisheria. Ombi hili limetupiliwa mbali,” alisema Bi Alego. Hakimu aliagiza kesi hiyo iendelee. Kirungu alisema hana shida na Bi Alego akiendelea kusikiza kesi hiyo.
from Taifa Leo https://ift.tt/SNM5WzP
via 
IFTTT