Gachagua atoa ishara huenda ni Kalonzo atabeba bendera ya Upinzani 2027

KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ametoa ishara za wazi zaidi kwamba kiongozi wa chama cha Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka anaweza kuwa mgombea rais wa Muungano wa Upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Bw Gachagua, ambaye awali alikuwa akisisitiza kwamba yeye ndiye chaguo bora la kumshinda Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, alionekana kubadilika kidogo alipotembelea Ukambani jana kwenye ziara ya siku tano ya Muungano wa Upinzani.

Bw Gachagua alisema kiongozi huyo wa kisiasa wa Ukambani ana sifa zote za kuwa Rais wa Kenya.

“Jamii ya Wakamba ndiyo itakayookota Kenya kutoka kwa utawala wa sasa kwa sababu kura zenu ndizo zinazotegemewa zaidi na thabiti nchini Kenya. Kura za Wakamba ni kura unazoweza kuamini,” alisema Bw Gachagua katika mji wa Tawa, Kaunti ya Makueni.

Bw Gachagua alisema ziara hiyo katika eneo ambalo limekuwa upinzani kwa muda mrefu ilichochewa na kutambua kwamba Rais Ruto bado ana umaarufu katika eneo hilo.

Alisisitiza kwamba jamii ya Wakamba, inayoishi Kaunti za Kitui, Machakos na Makueni, lazima isajili angalau kura 4 milioni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 ikiwa Muungano wa Upinzani unataka kufanikisha dhamira yake ya kumzuia Rais Ruto kupata muhula wa pili.

“Ninajua mara mtakapojisajili, tutakuwa tayari na kura 4 milioni pamoja na kura yangu moja hata kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 haujaanza,” alisema.

Hii inamaanisha ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na kura milioni 1.7 ambazo eneo hilo lilikuwa nazo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Pia alitangaza vita dhidi ya wafuasi wa Rais Ruto katika Ukambani aliotaja kama wasaliti.

“Mnahitaji kukataa Madiwani na Wabunge wanaomdhihaki Bw Musyoka wakitekeleza maagizo ya Rais Ruto. Kalonzo anawezaje kufanikiwa endapo wasaliti wa jamii wanatembea kwa uhuru?” alihoji Bw Gachagua.

Bw Musyoka aliongoza viongozi wengine wa upinzani katika kulaani Rais Ruto na utawala wake, huku Gavana wa Makueni, Mutula Kilonzo Junior, akiwataka wananchi wa Ukambani kuchangamkia usajili wa wapigakura unaoendelea ili kuongeza idadi ya wapiga kura katika eneo hilo.

Bw Musyoka alilaumu Rais kwa utawala mbaya na kuahidi kuunganisha taifa kumpeleka nyumbani.

“Tunashuku miili iliyopatikana katika makaburi ya pamoja Kaunti ya Kericho ni ya vijana waliouawa na utawala wa sasa. Utafiti wa kina unahitajika,” alisema.

Mgombea rais wa Jubilee, Fred Matiang’i, aliepuka kujadili suala la mgombea rasmi wa Muungano wa Upinzani. Hata hivyo, alihimiza wananchi wa Ukambani kuunga mkono upinzani.

Gavana wa Machakos, Wavinya Ndeti, aliwahimiza viongozi kumi wa Muungano wa Upinzani kutotengana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 akionya itakuwa vigumu kumshinda Rais Ruto wakigawanyika.



from Taifa Leo https://ift.tt/g7fz1n0
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post