Mpango wa Joho kujinasia wadhifa wa kitaifa wamleta katika vita na Mvurya

MGAWANYIKO wa kisiasa umelipuka upya katika eneo la Pwani, hali inayoweza kuathiri mafanikio ya muungano unaokusudiwa wa vyama vya ODM na UDA katika ukanda huo.

Kwa miezi kadha sasa, Waziri wa Madini, Uchumi wa Baharini na Ubaharia, Bw Hassan Joho, amekuwa akieleza hitaji la wanasiasa wa Pwani kuungana kumpigia debe Rais William Ruto kwa awamu ya pili ya uongozi.

Hata hivyo, matukio ya kisiasa wikendi iliyopita katika Kaunti za Kwale na Kilifi yaliashiria Bw Joho angali na kazi kubwa kuhakikisha kuna umoja kabla kampeni za 2027 zianze rasmi.

Katika Kaunti ya Kwale, ziara ambazo gavana huyo wa zamani wa Mombasa amekuwa akifanya sehemu tofauti za nchi zimeonekana kuzua tumbojoto kwa baadhi ya wanasiasa.

Hali hii imeonekana kufufua vita vya ubabe kati yake na Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana, Bw Salim Mvurya.

Akizungumza katika eneo la Lunga Lunga, Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, alipuuzilia mbali ziara ambazo Bw Joho amefanya kufikia sasa katika eneo hilo huku akisisitiza kwamba, yeye na wakazi wa Kwale wanamtambua tu Bw Mvurya kama kigogo wao wa kisiasa.

Chini ya wiki moja, Bw Joho amekuwa Kwale mara mbili ikiwemo Jumapili, akiandamana na Mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader, na wanasiasa wengine.

Bi Achani alisifu uongozi wa Bw Mvurya akisema wakati Waziri huyo alipokuwa gavana, alibadilisha sura ya Kwale na kufungua fursa kwa wakazi wengi wa kaunti hiyo, na anaendelea kufanya hivyo pia wakati huu akiwa katika serikali ya kitaifa.

Alionya pia kwamba viongozi wa Kwale hawatakubali kile alichokiita kutoheshimiwa kwa uongozi wa kaunti hiyo, akisisitiza kuwa wakazi wanatarajia viongozi waliotoa mchango katika maendeleo ya kaunti hiyo waheshimiwe.

“Kama mtu anajisikia kwamba ‘kingpin’ wake yuko Mombasa, avuke feri amfuate. Sisi mtu ambaye tunajua ametusaidia hii Kwale ni mheshimiwa Salim Mvurya. Hii Kwale imetambulika Kenya nzima kwa sababu Mvurya alitushika mkono. Tunataka aheshimiwe,” akasema.

Aliongeza kuwa, Naibu Rais Kithure Kindiki pia anastahili kuheshimiwa. Itakumbukwa kuwa, Bw Joho na wandani wake wamekuwa wakieleza nia kwamba awe mgombea mwenza wa Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu ujao, chini ya muafaka kati ya UDA na ODM.

Bw Joho, ambaye alikuwa katika eneobunge la Matuga, alijitenga na dhana kwamba anaingilia siasa za kaunti hiyo.

Hata hivyo, alishikilia msimamo wake kwamba analenga wadhifa mkubwa zaidi wa kitaifa.

“Nataka niwaambie watu wa Kwale, hii siasa yenu ya hapa mtapambana wenyewe. Kila mmoja ana uwezo wa kujitetea hapa Kwale kivyake. Mimi niko siasa ya kitaifa,” akasema.

“Safari hii watu wajue hii Pwani tutashikana na kama kuna mtu ana shauku tutazungumza naye aachane na hizo. Kuna safari ya muhimu hapo mbele,” aliongeza.

Katika Kaunti ya Kilifi, aliyekuwa Waziri wa jinsia, Bi Aisha Jumwa, ameibua mzozano na Gavana Gideon Mung’aro, akilenga kuwania kiti hicho 2027.

Wawili hao walitumia hafla za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kupimana nguvu, huku Bi Jumwa akionya viongozi wa UDA wasikubali kuachia ODM ugombeaji katika baadhi ya maeneo nchini bila kuwa na ushindani.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, amekuwa akisisitiza kuwa UDA itamuunga mkono Bw Mung’aro kwa ugavana.



from Taifa Leo https://ift.tt/DmJt9FI
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post