
JUHUDI za kufuta kituo cha kitaifa cha kujumlishia kura kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027 zimepata upinzani mkali kutoka kwa wabunge na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), hali inayoibua mvutano wa kisheria kuhusu namna matokeo ya urais yanavyotangazwa.
Wabunge na maseneta wameutetea mfumo wa sasa wa kisheria, huku IEBC ikisisitiza kuwa mfumo huo ni halali, muhimu kwa uhakiki wa matokeo, na uko wazi kwa uchunguzi wa mahakama.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah pamoja na viongozi wa upinzani inapinga Kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi na kanuni zinazohusiana na ujumlishaji wa kura za urais.
Kesi hiyo pia inalenga kudadisi kuanzishwa kwa kituo cha kitaifa cha kujumlishia kura pamoja na majukumu ya wasimamizi wa uchaguzi wa kaunti na mwenyekiti wa IEBC.
Walalamishi wanahoji kuwa matokeo ya kura za urais katika maeneobunge yanapaswa kuwa ya mwisho hayapaswi kupelekwa tena katika kituo cha kitaifa kwa uhakiki au kuhesabiwa upya.
Seneta Omtatah anasema Katiba inaweka wazi kuwa vituo vya kupigia kura na maeneobunge ndiyo ngazi ya mwisho ya kuhesabu na kutangaza matokeo ya urais.
Anasisitiza kuwa mwenyekiti wa IEBC ana jukumu la kiutawala tu la kukusanya na kutangaza mshindi bila kubadilisha matokeo.
[caption id="attachment_187055" align="alignnone" width="2000"]
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alipomtangaza William Ruto kuwa mshindi wa urais 2022. Picha|Maktaba[/caption]
Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amekataa madai hayo akisema kituo cha kitaifa kinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na maamuzi ya awali ya mahakama.
Anasema kituo hicho hakibadili wala kuharibu matokeo, bali hukagua Fomu 34A na 34B ili kuhakikisha usahihi kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa.
“Hatua hii huongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuwa umma unaweza kuona fomu kupitia mtandao,” amesema Ethekon katika kiapo cha mahakama.
Bunge nalo limejitokeza kutetea mfumo huo, likisema Kifungu cha 39 kinatoa utaratibu wa uwazi na uthabiti katika uwasilishaji wa matokeo.
Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge anasema masuala yaliyowasilishwa tayari yanashughulikiwa na Bunge kupitia Mswada wa Marekebisho ya Uchaguzi wa 2024, hivyo kuingilia kwa mahakama sasa kunaweza kuvuruga mchakato wa kutunga sheria.
Seneti kupitia Karani Jeremiah Nyegenye pia imeunga mkono msimamo huo, ikisema hoja nyingi zinaweza kushughulikiwa kupitia bunge badala ya mahakama.
Kesi hiyo itatajwa kusikilizwa rasmi tarehe 1 Julai 2026.
from Taifa Leo https://ift.tt/mr7ibZk
via IFTTT