
KATIBU Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amesema kuwa Linda Mwananchi imevumbua mbinu za kujivumisha kwa raia kuelekea uchaguzi wa 2027.
Linda Mwananchi inalenga kuibuka na sera zinazowaridhisha wakazi wa kila eneo ambako watakuwa wakifika kujieleza kupitia mikutano nyanjani.
Mbinu hii ndiyo ilitumika kuelekea mkutano wa hadhara uwanja wa Tononoka ambao ulihudhuriwa na halaiki ya raia wikendi hii.
Wengi wa viongozi waliohutubu kwenye mkutano huo, walizungumzia dhuluma za kihistoria hasa unyakuzi wa mashamba.
Wanasiasa kutoka mrengo huo wanaonekana sasa kulenga changamoto za raia badala ya kuzungumzia mrengo wa Linda Ground unaoongozwa na Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga.
Tayari Linda Mwananchi imebuni kamati ya kutambua changamoto za kila eneo na kupendekeza suluhu, ambapo kamati hiyo itaongozwa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi.
Bw Osotsi Ijumaa iliyopita, alitimuliwa kama naibu kiongozi wa ODM wakati wa Kongamano la Chama hicho.
Tayari Linda Mwananchi imeandaa mikutano mikubwa Kitengela, Kaunti ya Kajiado, Kakamega, Narok na Mombasa.
“Watu wengi wameonyesha nia ya kushirikiana nasi huku wengi wakitaka kutuunga mkono kifedha na kwa njia nyinginezo.
Tumeona Bw Osotsi ana hekima na mawanda makubwa kisiasa ndiposa tumeamua awe mshirikishi wa shughuli zetu,” duru kutoka kundi hilo ziliambia Taifa Leo.
“Kibarua chake cha kwanza kilikuwa kuratibu na kuandaa mkutano wa Tononoka ambapo masuala yanayohusu ardhi za Wapwani ndiyo yalizungumziwa. Anatarajiwa kuratibu mikutano mingine na pia kongamano la viongozi,” duru hizo ziliongeza.
Wakati wa mkutano wa Tononoka, viongozi walimakinikia kuzungumzia masuala yanayohusu raia na Bw Sifuna akazua swali iwapo Rais William Ruto ana nia ya kutekeleza sera kuhusu umiliki wa ardhi.
“Ardhi ambazo zinamilikiwa na matajiri ndizo wakazi wanataka badala ya vyeti vya vipande vidogo vidogo. Tunahitaji ardhi hizo zipewe vijana,” akasema Bw Sifuna.
Mbunge wa Suba Kusini, Bw Caroli Omondi naye alisema kuwa Linda Mwananchi itahakikisha wakazi wa Pwani wananufaikia ardhi yao.
“Tutaondoa leseni zote haramu za uchimbaji madini eneo hili ili wakazi wanufaike,” akasema Bw Omondi.
Bw Osotsi alihusisha uungwaji mkono wa Linda Mwananchi na ule wa muungano wa NARC ulipata katika uchaguzi wa 2002.
“Tunaimarika katika kila mkutano na ujumbe wakati huu utakuwa tofauti hasa tukiangazia masuala yanayowahusu wananchi moja kwa moja,” akasema Bw Osotsi.
from Taifa Leo https://ift.tt/GfXvnRB
via IFTTT