Ripoti yafichua ufisadi wa ngono umeongezeka

MWAKA wa 2014, Mary* alikuwa akitafuta kazi miaka mitatu baada ya kuhitimu shahada ya Mawasiliano na Uanahabari katika Chuo Kikuu cha Egerton. Wakati huo, alikuwa akifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea, lakini malipo yalikuwa kidogo na hayakukidhi mahitaji yake. “Nilikuwa nimefika mahali pa kukata tamaa baada ya kujaribu bila mafanikio kupata ajira ya kudumu,” anasema. Baadaye aliona tangazo la kazi katika moja ya mabunge ya kaunti eneo la South Rift kwa nafasi ya mwandishi wa kumbukumbu za Bunge hilo. Aliamua kumtafuta karani aliyewahi kufahamiana naye ili amsaidie kupata kazi hiyo. Hata hivyo, yaliyofuata yalimshangaza. “Aliniambia tukutane klabuni usiku, na akaweka wazi kwamba baadaye tunaweza kuwa na muda pamoja. Hapo ndipo nilijua alitaka tufanye mapenzi. Niliondoka na sikuendelea na hilo suala kabisa ,” anasema. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inataja matukio kama hayo ambapo mtu anaombwa ngono ili kupata huduma au ajira, kama aina hatari ya ufisadi wa kijinsia licha ya kukosekana kwa sheria mahususi ya kuushughulikia. Katika ripoti yake ya kwanza kabisa iliyotoa takwimu za ufisadi kulingana na jinsia, mnamo Alhamisi jijini Nairobi, tume ya EACC inaonyesha kuwa ufisadi wa kijinsia umeenea katika sekta ya umma na binafsi. Utafiti huo unaonyesha kuwa wanawake wanaotafuta huduma kwa maafisa wa umma wana uwezekano mara mbili zaidi ya wanaume kuombwa ngono. Asilimia 82 ya wanawake waliripoti kuombwa ngono angalau mara moja katika miezi 12 iliyopita, huku asilimia 73 wakisema waliombwa zaidi ya mara tatu. Kwa wanaume, asilimia 18 waliripoti kuombwa ngono mara moja, na asilimia 27 walisema walikumbana na hali hiyo mara tatu au zaidi. Aidha, asilimia 80 ya maafisa wanaodai ngono ni wanaume. EACC sasa inataka sheria za kupambana na ufisadi zibadilishwe ili kutambua wazi ufisadi wa ngono kama kosa la jinai. Hapo awali, Kenya ilijaribu kushughulikia suala hili kupitia Sheria ya Makosa ya Kijinsia ya 2006, lakini bado kuna mapengo katika kulifafanua kama ufisadi. Mnamo 2024, Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Esther Passaris aliwasilisha ombi bungeni kutaka sheria ifanyiwe marekebisho ili kutambua ufisadi wa ngono kuweka adhabu na kusaidia waathiriwa. Hata hivyo, Kamati ya Malalamishi ya Umma ilikataa ombi hilo, ikisema sheria zilizopo tayari zinatosha. Lakini wataalamu wanapinga msimamo huo. Kaimu Katibu wa Tume ya Marekebisho ya Sheria, Peter Musyimi, aliwaambia wabunge kuwa ufisadi wa ngono huathiri zaidi wanawake na wasichana wanaotafuta huduma za msingi kama vitambulisho, elimu, maji au ajira. Mifano ni pamoja na “ngono kwa samaki” katika maeneo ya Pwani, wanawake kulazimishwa kufanya ngono ili kupata maji mitaani, na wafanyabiashara wanawake kunyanyaswa sokoni. Kwa mujibu wa wakili wa Mahakama Kuu Vivian Mwende, ufisadi wa ngono ni aina ya ulaghai yenye mwelekeo wa ngono ambapo mtu hulazimishwa kutoa ngono ili kupata huduma au kuepuka madhara. “Ni hali ya kulazimishwa kukubali ngono kupata kitu fulani na ukikataa, haupati ,” anasema. Anashauri waathiriwa kuhifadhi ushahidi kama ujumbe, picha na rekodi za mawasiliano, na kuripoti kwa polisi, hasa kitengo cha uhalifu wa mtandao. Tofauti na Kenya, baadhi ya nchi kama India zimeweka sheria maalum dhidi ya ufisadi wa aina hii na adhabu kali ya kifungo na faini. Bila sheria wazi, wataalamu wanaonya kuwa Wakenya wengi wataendelea kuwa katika hatari ya kujipata katika dhuluma hii.    

from Taifa Leo https://ift.tt/X7dAU9R
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post