
MAONI ya umma katika mitandao ya kijamii kuhusu Mswada wa Fedha 2026 umekuwa hasi kwa kiwango kikubwa, huku mijadala mingi ikitawaliwa na alama ya #RejectFinanceBill2026, kwa mujibu wa uchambuzi wa machapisho 3,000 kwenye X yaliyochapishwa kati ya Mei 2 na Mei 26.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wametaja mswada huo kama unaolenga kuwakandamiza wananchi, na kuongeza mzigo wa kiuchumi.
Ni sehemu ndogo tu ya machapisho yaliyoonyesha mswada huo unaungwa mkono, huku hata mijadala isiyo na msimamo ikijikita zaidi katika kuhoji vifungu au kufanya uhakiki wa taarifa badala ya kuunga mkono sheria hiyo.
Masuala matatu yameibuka kuwa chanzo kikuu cha hasira mtandaoni: kuongezwa kwa mamlaka ya Mamlaka KRA, mapendekezo ya kutoza kodi kwenye majukwaa ya malipo ya kidijitali, na mkanganyiko kuhusu ushuru wa simu za kisasa.
Katika suala la KRA, pendekezo linaloruhusu mamlaka hiyo kutumia taarifa zilizokusanywa kutoka kwa taasisi za kifedha na makampuni ya mawasiliano kukadiria mapato ya walipa ushuru limeibua hofu kubwa.
Wataalamu wa ushuru wanasema hatua hiyo inaweza kuhamisha mzigo wa kwa mlipa ushuru, ambapo mtu atapaswa kuthibitisha kuwa makadirio ya KRA si sahihi badala ya KRA kueleza jinsi ilivyofikia hesabu hizo.
Wataalamu pia wameeleza wasiwasi kuhusu ukosefu wa uwazi katika mfumo huo.
Suala jingine linalojadiliwa kwa mapana ni pendekezo la kutoza ushuru wa ongezeko la thamani (VAT) wa asilimia 16 kwa majukwaa ya malipo ya kidijitali kama M-Pesa, Airtel Money na Pesapal.
Wizara ya Fedha imetetea pendekezo hilo ikisema VAT inapaswa kutozwa kwa watoa huduma za ICT wanaowezesha miamala.
Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa gharama hizo zinaweza kuhamishiwa kwa watumiaji kupitia ada za juu za miamala, jambo litakalowaathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea huduma hizo.
Mswada huo pia umeleta mkanganyiko kuhusu mabadiliko ya ushuru wa simu za kisasa.
Waziri John Mbadi amesema serikali inalenga kupunguza mzigo wa ushuru kwa simu kutoka asilimia 55 hadi asilimia 25 kupitia kuunganisha uliopo kwa sasa.
Hata hivyo, wananchi wengi mitandaoni bado hawajaridhika, wakisema maelezo ya serikali si wazi na yanaweza kupotosha kuhusu gharama halisi za simu sokoni.
Mbali na hoja za sera, mtandao umegeuka uwanja wa mapambano ya taarifa sahihi na potofu.
Baadhi ya mitandao imeeneza madai ya uongo kwamba mswada huo unaanzisha ushuru mpya kwa bidhaa za msingi kama mkate, madai ambayo hayamo kwenye sheria hiyo.
Kukabiliana na hilo, baadhi ya watumiaji wameanzisha kampeni za kurekebisha taarifa hizo na kuhimiza uhakiki wa taarifa kabla ya kusambazwa.
Alama ya reli ya #FB2026Facts imeibuka kama juhudi ya kupinga upotoshaji, huku zaidi ya machapisho 170 yakitumiwa kubaini na kupinga taarifa zisizo sahihi.
Wakati huo huo, kampeni nyingine ya kuunga mkono mswada ambapo zaidi ya machapisho 1,400 yanaonekana kusambaza ujumbe unaofanana, hali inayoashiria kampeni iliyoratibiwa badala ya mazungumzo ya kawaida ya wananchi.
Kwa ujumla, Mswada wa Fedha 2026 umeibua si tu upinzani mkubwa mtandaoni, bali pia mazingira ya taarifa ambapo hoja za wananchi, propaganda na upotoshaji vinachangia kwa kiasi kikubwa kuunda mtazamo wa umma kwa wakati halisi.
from Taifa Leo https://ift.tt/V4dTNko
via
IFTTT