
VIONGOZI wa kisiasa na kijamii katika ukanda wa Mlima Kenya jana walipuuzilia mbali ombi la msamaha kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama tawala cha UDA, Bw Hassan Omar wakimtaka Rais William Ruto amtimue katika wadhifa huo.
Semi zake Bw Omar zinazofasiriwa kuwa za kikabila na chuki zimemueka Rais Ruto katika shinikizo za kutakiwa ajitenge na katibu huyo mkuu wa chama chake.
Mwingine ambaye amejipata katika shinikizo ni Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki ambaye anaulizwa inakuwaje amenyamaza ilhali mrengo wake wa kisiasa unaweka jamii anayotoka katika hatari ya ghasia.
Pia, washirika wa Rais Ruto katika Mlima Kenya wamejipata katika njia-panda, wengine kama Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru wakijitokeza kulia kwamba Bw Omar anatatiza husiano na serikali.
Bw Omar anahusishwa na nukuu za kueneza chuki na kupalilia uhasama alizozitoa katika ziara ya Rais Ruto katika eneo la Pwani mwishoni mwa wiki.
Bw Omar alidaiwa kutoa matamshi yaliyoashiria kupigia debe kutengwa na kudharauliwa kwa jamii za Mlima Kenya pamoja na kusingizia Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kama kiongozi asiyejali ambaye anamiliki mashamba mengi katika eneo la Pwani.
Akitumia lugha nzito na maneno yaliyojaa cheche, Bw Omar alisema Wapwani na Wakenya wanafaa kuungana dhidi ya madhalimu, mafisadi na wajeuri wanaodhania Kenya ni yao pekee yao.
Kinara wa chama cha DCP, Bw Rigathi Gachagua akiwa nchini Uingereza alidai Jumamosi kwamba Bw Omar alipendekezewa matamshi hayo na Rais Ruto.
"Mimi nilikuwa naibu wa Ruto kwa zaidi ya miezi 20. Nina ufahamu wa jinsi yeye hupanga watu wa kusema yaliyo moyoni mwake. Msione au mmsikie Bw Omar katika matamshi hayo ya kudunisha Mlima Kenya. Huyo ni Rais Ruto alikuwa anaongea kupitia kinywa cha Omar," akasema Gachagua.
Mambo yalipochacha huku Baraza Kuu ya muungano wa Jamii ya Agikuyu kupitia mwenyekiti Wachira Kiago likikemea matamshi ya Omar, jana chama cha UDA kupitia barua iliyotiwa saini na katibu mkuu huyo kiliomba msamaha.
Barua hiyo ilisema Bw Omar alinukuliwa visivyo wala hakuwa akinuia kudunisha au kukera jamii yoyote.
Lakini Bw Gachagua na Bw Kiago waliteta kuwa ombi hilo lilikuwa la ujeuri na utani wa kukera.
"Huwezi ukatekeleza utovu wa nidhamu kwa kiwango cha kuchochea chuki na kuhatarisha usalama kisha uandike waraka usioonyesha uzito wa kero lililopo," akasema Bw Kiago.
Aliongeza kwamba umekuwa mtindo wa Rais Ruto na washirika wake wa karibu kutumia semi za chuki, dharau na kupigia debe ghasia kisha kunazuka sarakasi za kusema pole.
Akiwa katika Kaunti ya Murang'a jana, kinara wa Wiper Patriotic Front, Bw Kalonzo Musyoka alisema kwamba ni dhahiri kwamba Rais Ruto anapania kutumia ghasia kujipa awamu ya pili mamlakani.
"Bw Omar ni kipaza sauti cha Rais Ruto. Usijisumbue kujua Bw Omar alikuwa akiyaangazia mawazo ya nani. Ukimsikia mbwa anabweka, usimtafute mfugaji wake mbali. Yuko hapo tu," akasema.
Bw Musyoka aliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) isiweke faili ya Rais Ruto mbali kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa atajipata amerejeshwa huko baada ya uchaguzi mkuu wa 2027.
"Ghasia za 2007/8 zilianza kwa mtindo sawa na huu tunaoona kutoka kwa serikali hii. Rais Ruto ndiye aliye katika shinikizo kuu la kuwajibikia umoja wa kitaifa la sivyo atachoma nchi na atabebeshwa huo msalaba," akasema.
Hata hivyo, Bw Omar alisema kwamba katika maisha yake yote hadi sasa amekuwa muadilifu kwa haki za Wakenya wote.
Alisema kwamba maongezi yake yaliyochukuliwa kuwa ya kikabila yalifaa kutafsiriwa kwa msingi wa haki za jamii za Pwani kuhusu umilki wa mashamba.
Hata hivyo, Bw Omar alishikilia kwamba alifurahishwa na hali ambapo baadhi ya watu wa Mlima Kenya walivyoupata ujumbe katika semi zake.
“Lakini kwa hao wote walionichukulia kama mbishi, najuta na ninawaomba msamaha," akasema.
Bw Kiago alisema kwamba msamaha huo hauna ladha ya ukweli na nia njema kwa kuwa unaashiria roho ya mtu anayefurahia vurugu na kisha kupuliza alikouma kwa njia ya unafiki.
Seneta wa Murang'a, Bw Joe Nyutu jana alimtaka Rais Ruto aombe msamaha mwenyewe kwa niaba ya serikali, chama tawala na katibu mkuu wake.
"Hadi itakapokuwa hivyo, sisi kama wadau wa Mlima Kenya tutazidi kushikilia kwamba serikali ya Rais Ruto akiwa yeye ndiye mhusika mkuu inapania kuchochea Wakenya wengine dhidi yetu kwa nia ya kutuingiza katika ghasia sawa na zile za 2007/08," akasema.
Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga alisema jinsi yeye alivyojiuzulu katika wadhifa wa naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) baada ya kuzungumza vibaya kuhusu marehemu Raila Odinga, ndivyo Hassan Omar aliye mbunge wa EALA, anafaa kujiuzulu katika wadhifa wa katibu mkuu wa UDA.
from Taifa Leo https://ift.tt/6a4xG5E
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS