Alhamisi ni siku ya kawaida ya kazi, Kindiki na Mwaura waonya upinzani kuhusu Juni 25

SERIKALI imewaonya viongozi wa upinzani dhidi ya kutumia maandamano ya Gen-Z hapo Alhamisi kujinufaisha kisiasa, ikisema watakabiliwa vikali kisheria.

Maandamano hayo yamepangwa kuandaliwa kuadhimisha miaka miwili tangu vijana wa Gen-Z wavamie jengo la bunge mnamo Juni 25 wakipinga Mswada wa Fedha 2024.

Takwimu za Tume ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR) zinaonyesha watu 60 waliaga dunia kwenye maandamano hayo ingawa mashirika mengine yamekuwa yakisisitiza idadi hiyo ni ya juu zaidi.

Msemaji wa polisi Isaac Mwaura jana alisema polisi watapambana na wale ambao wanapanga kushiriki ghasia.

“Wanasiasa wanaonywa wakome kutumia maandamano hayo kutoa matamshi ya uchochezi na kujinufaisha kisiasa,” akasema Bw Mwaura.

Alisema Kifungu cha 37 cha katiba kinasisitiza kuwa maandamano lazima yawe ya amani na wale ambao watakuwa barabarani wakiandamana, hawastahili kuvuruga shughuli za watu wengine.

“Mbona tuadhimishe mauti ya walioaga kwa kuharibu mali na kusaka umaarufu wa kisiasa? Mbona maandamano hayo yasiwe ya amani? Tunastahili kuweka wazi tofauti ya maandamano ya kawaida na uhuni,” akasema Bw Mwaura.

Aidha, alikanusha kuwa Juni 25 ni sikukuu ya kitaifa na akawataka Wakenya waje kazini na kusaka riziki kama kawaida.

Kuhusu fidia alisema tume ya KNCHR imenakili waathiriwa 1,500 ambao watanufaika akisema idadi hiyo inatarajiwa kupanda zaidi.

Wiki jana, Rais William Ruto alitangaza kuwa serikali imetenga jumla ya Sh2 bilioni ambazo zitatumika kulipa fidia kwa wahanga wa maandamano ya miaka ya nyuma ikiwemo ya Gen Z mnamo 2024.

Naibu Rais Prof Kithure Kindiki naye amesema serikali haitavumulia juhudi zozote za kutumia maandamano ya Gen Z kushiriki uporaji na uharibifu wa mali, akionya kuwa watakaofanya hivyo watakabiliwa kisheria.

Profesa Kindiki alisema Katiba inawalinda watakaoshiriki na wale ambao hawatashiriki maandamano kwa hivyo hakuna haja ya kuzua zahama na kutatiza shughuli za wengine.

“Hakuna yeyote atakayetutishia dhidi ya kuwalinda Wakenya ambao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida iwe wanasafiri au kuendeleza biashara zao kama kawaida,” akasema Profesa Kindiki.

Mnamo Jumapili, Profesa Kindiki alisema Katiba inaruhusu maandamano ila hakutakuwa na nafasi ya mtu yeyote kumvamia mwengine au kuharibu mali na kupora biashara wakati wa maandamano hayo.

“Anayeshiriki na asiyeshiriki wote watalindwa kwa mujibu wa sheria,” akaongeza.

Naibu Rais alikuwa akiongea katika eneobunge la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa ibada ya madhehebu mbalimbali, hafla ambayo pia ilikuwa ya kuchangishia makanisa 19.



from Taifa Leo https://ift.tt/quaHhnK
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post