
Kujitokeza hadharani kwa Bw Muhoho Kenyatta katika jukwaa la kisiasa wiki hii kumezua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa siasa za chama cha Jubilee na nafasi ya familia ya Kenyatta kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Bw Muhoho, kaka mdogo wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, alionekana bega kwa bega na mgombea urais wa Jubilee, Dkt Fred Matiang’i, katika mkutano mkubwa wa wajumbe wa jamii ya Maa uliofanyika Kaunti ya Narok Ijumaa hatua ambayo wengi wanaona kama ishara ya kurudi kwa nguvu kwa familia hiyo katika siasa za chama.
Kwa miaka mingi, Muhoho amesalia nyuma ya pazia, akitambulika zaidi kama mfanyabiashara na mshauri wa karibu wa Uhuru, badala ya kuwa mwanasiasa wa jukwaani. Hata hivyo, kuibuka kwake sasa—na hasa katika jukwaa rasmi la chama—kumechukuliwa na wachambuzi kama mabadiliko ya kimkakati.
Mchanganuzi wa siasa Dkt Mike Walia anasema kwamba hatua hiyo inaonyesha Jubilee inajaribu kujipanga upya na kurejesha mshikamano wake baada ya kipindi cha misukosuko ya kisiasa. “Muhoho si mtu wa kubashiri lakini kujitokeza katika mkutano wa chama kunamfanya kuwa kiungo muhimu katika Jubilee. Pia kunaweza kuwa ujumbe kuhusu 2027,” anasema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya wa chama cha DAP Kenya na Peter Munya wa PNU. Ingawa Munya ametangaza kuunga Matiang’i, kuhudhuria kwa Bw Natembeya kulizua maswali.
Kulingana na Dkt Walia, kujitokeza kwa Muhoho si tukio la kawaida bali ni ujumbe wa kisiasa uliopangwa kwa makini. “Hii si bahati mbaya. Ni ishara kwamba familia ya Kenyatta bado ina nia ya kuwa na ushawishi katika siasa za taifa. Wanajaribu kuhakikisha kuwa hawatoweki katika ramani ya siasa za Kenya,” anasema.
Wachambuzi pia wanaona uwepo wa Muhoho kama kupiga jeki kampeni ya urais ya Dkt Matiang’i, ambaye anahitaji mtandao imara wa kisiasa na kifedha ili kujenga ushindani kitaifa.
Hata hivyo, wengine wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuzua upya mjadala kuhusu siasa za kifamilia na ushawishi wake katika demokrasia ya Kenya. “Swali litakaloulizwa ni: Je, hii ni kuimarisha taasisi za chama au ni kurejesha siasa za nasaba?” anauliza mchambuzi wa siasa Peter Katana.
Hata hivyo anasema Muhoho na mtu mwingine wa familia ya Kenyatta ana haki ya kuamua chama na mustakabali wake kisiasa.
Duru za kisiasa zinaashiria kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anaweza kuachia rasmi uongozi wa Jubilee kabla ya 2027 na analenga kuhakikisha chama kimejipanga vyema chini ya uongozi mpya wa Dkt Matiang’i.
Kulingana na wanaofahamu mipango iliyosukwa, Uhuru atamkabidhi Matiang’i uongozi wa chama na anahakikisha kuna watu wake wa karibu ndani kuwakilisha maslahi yake.
“Usisahau kuna tetesi kwamba mfadhili wa kampeni za urais za Matiang’i ni Uhuru na hivyo sio rahisi kwake kuachilia chama kabisa bila kudumisha mizizi yake. Hii ndio sababu tunaona Muhoho akijitokeza.
Muhoho amekuwa akitajwa katika kampeni za chaguzi za awali akicheza nyuma ya pazia na kujitokeza kwake katika chama cha Jubilee kunasawiriwa kama mabadiliko makubwa ingawa hajatangaza kuwania wadhifa wowote chamani au katika uchaguzi mkuu ujao.
Kumekuwa na minong’ono kuwa analenga kiti cha ubunge lakini kufikia sasa hajatangaza azima hiyo.
“Kwa sasa, kinachoonekana wazi ni kwamba hatua ya Muhoho imeingiza uhai mpya katika mjadala wa siasa za upinzani na kufungua ukurasa mpya kuhusu nafasi ya familia ya Kenyatta katika siasa za baada ya Uhuru,” asema Dkt Walia.
from Taifa Leo https://ift.tt/yu8Hhtv
via IFTTT