
Ofisi ya Capitol Hill jijini Nairobi ilikuwa ikichangamka kila mara Raila Odinga alipoingia. Wanasiasa, wanadiplomasia, wafanyabiashara na Wakenya wa kawaida walikuwa wakimiminika humo kutafuta fursa ya kuonana na mtu waliyemuita Baba. Simu zililia bila kikomo, huku wafanyakazi wakiratibu mikutano na kupokea wageni.
Leo, hali imebadilika kabisa.“Ni kama mji uliokufa,” anasema Jack Nyamburi, aliyekuwa msaidizi wake wa karibu kwa miaka mingi. “Unaweza kukaa siku nzima bila mtu yeyote kuja.”
Kwa waliomhudumia Odinga kwa miaka mingi, baadhi kwa miongo kadhaa, ukimya huu si wa kawaida. Ni wa kihisia, kisiasa na binafsi.
Kwao, Odinga hakuwa tu mwajiri. Alikuwa mlezi, mkali lakini mwenye huruma, na wakati mwingine kiongozi asiyeeleweka kirahisi.
Nyamburi anakumbuka alikutana naye kwa mara ya kwanza nje ya Hoteli ya Serena mwaka 2005—mkutano ulioanza kwa makofi matatu lakini ukaishia kuwa mwanzo wa uhusiano wa muda mrefu. Kutoka hapo alipanda ngazi hadi kuwa msaidizi wake binafsi, akifanya kazi naye hadi nyakati za serikali ya muungano na baadaye.“Alikuwa mkali, lakini alijali,” asema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Florence Olang’, aliyekuwa msimamizi mkuu katika ofisi hiyo kwa miaka kumi. “Hakutuona kama wafanyakazi tu. Tulikuwa kama familia yake.”
Wafanyakazi wanamkumbuka kama mtu aliyesisitiza nidhamu lakini pia alikuwa mkarimu—mtu ambaye angegawa pesa kwa usawa au kuingilia kati kusaidia matatizo yao binafsi.
Sifa moja iliyojitokeza zaidi ni upatikanaji wake. Nyamburi anasema Odinga alikuwa na kanuni rahisi: hakukuwa na simu iliyopaswa kukosa kujibiwa.
“Ukimuita na asipokee, angekupigia baadaye. Hata kama hakujua nambari, angeuliza nani alipiga na kupiga tena,” anaeleza.
Utamaduni huo, wanasema, sasa umetoweka.
“Wabunge waliokuwa wakitupigia kila siku sasa hawapokei simu zetu,” anasema Nyamburi.
Siku zake za mwisho, kwa mujibu wa wasaidizi wake, zilikuwa za kawaida. Alitembelea ofisi Septemba 23, 2025, siku moja baada ya kuongoza mkutano wa wabunge wa ODM kaunti ya Machakos. Alifanya mikutano, akazungumza na wafanyakazi na, kama kawaida, akagawa pesa.
“Aliniambia nihakikishe kila mtu amepata kitu,” anakumbuka Nyamburi.
Jioni hiyo aliugua na kulazwa hospitalini. Hata akiwa hospitalini, aliendelea kuwasiliana na wafanyakazi wake kuhusu masuala ya kazi.
Florence anakumbuka siku hiyo kama ya kawaida: “Tulikuwa na mikutano, tulianza majadiliano lakini hatukumaliza. Alisema tutaendelea akirudi, lakini hakurudi.”
Baada ya kifo chake, mtandao mkubwa wa wafanyakazi aliokuwa ameunda ulianza kuyumba. Baadhi walikuwa wameajiriwa kupitia serikali, wengine kupitia chama cha ODM, na wengine walilipwa moja kwa moja na yeye.
Mfumo huu, ingawa ulikuwa thabiti alipokuwa hai, ulionekana dhaifu baada ya kuondoka kwake.
Baadhi ya wafanyakazi walifutwa kazi, huku wengine wakibaki gizani kuhusu hatima yao. Katika mkutano wa Machi 11, 2026, hali ilifikia kilele, wafanyakazi walilia walipoambiwa nafasi zao hazihitajiki tena.
Kwa baadhi, huo ulikuwa mwisho wa kazi za miaka mingi.
“Tunahitaji kusaidiwa kuingia katika utumishi wa umma kama alivyotamani Raila,” alisema Erick Ominde, dereva aliyemhudumia kwa miaka 25.
Wengine walionyesha kukata tamaa, si tu kwa kazi bali kwa kutambuliwa.
Katikati ya hali hiyo, Winnie Odinga aliingilia kati. Katika mkutano uliofanyika Jaramogi Oginga Odinga Foundation, alitoa dola 50,000 kusaidia wafanyakazi.
“Chumba kilijaa hisia,” anakumbuka Nyamburi.
Lakini kwa wengi, huo ndio ulikuwa msaada pekee waliopata.
Wakati huohuo, ODM imekumbwa na migawanyiko ya ndani baada ya kifo chake. Makundi mawili—Linda Ground na Linda Mwananchi—yameibuka, yakizozana kuhusu uongozi na mwelekeo wa chama.
Nyamburi anasema wazi: “Hii si hali ambayo Raila angetaka. Angeumia sana kuona haya.”
Mabadiliko katika Capitol Hill kutoka kitovu cha siasa hadi ofisi tulivu yanaakisi mabadiliko makubwa zaidi.
“Kabla ya kifo chake watu walikuwa wakimiminika, sasa hakuna kinachoendelea,” asema Florence.
Kwa wengi, Odinga alikuwa zaidi ya mwajiri—alikuwa mfumo wa msaada. Alitoa msaada wa kifedha, ushauri na fursa.
“Sasa sisi ni kama watoto waliopoteza baba,” asema.
Wafanyakazi wengine wanangoja kupelekwa katika utumishi wa umma, huku wengine wakijaribu kuanza maisha upya. Lakini kilicho chungu zaidi ni ukimya wa wale waliokuwa wakitegemea usaidizi wao.
“Tuliwasaidia kumfikia. Sasa hawapokei simu zetu,” asema Nyamburi.
Baadhi yao sasa wanamuomba Rais kuwasaidia, wakitaka aheshimu ahadi alizotoa wakati wa mazishi ya Odinga.
“Tunaomba tukumbukwe,” asema mmoja wao.
from Taifa Leo https://ift.tt/OW1IPYg
via IFTTT