Ziara 38 zilizofungulia Ruto ‘bedroom’ ya ODM

Ziara za mara kwa mara za Rais William Ruto katika eneo la Nyanza tangu ukuruba wake na marehemu Raila Odinga zimeanza kubadili mwelekeo wa kisiasa eneo hilo, huku viongozi wa ODM wakizikumbatia na kugeuza eneo lililokuwa na upinzani mkali kuwa jukwaa la ushirikiano.

Tangu muafaka huo ulipoanzishwa Julai 2024, Rais Ruto amefanya angalau ziara 38 katika eneo la Luo Nyanza pekee, ishara ya juhudi kubwa za kisiasa katika ngome iliyokuwa ikitawaliwa na Odinga kwa miongo kadhaa.

Kaunti ya Homa Bay imeibuka kuwa kitovu cha ziara hizo, chini ya Gavana Gladys Wanga ambaye pia ni mwenyekiti wa kitaifa wa ODM. Kati ya ziara hizo 38, 12 zimefanyika Homa Bay, zikifuatiwa na 10 katika kaunti ya Kisumu, tisa kaunti ya Migori na saba kaunti ya Siaya.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa mikakati ya Wanga—ikiwa ni pamoja na kuwarai viongozi na kupamba ziara hizo kama za maendeleo, imefanya Homa Bay kuwa lango kuu la ushawishi wa Rais Ruto Nyanza.

Kwa miaka mingi, Nyanza ilionekana kuwa ngome isiyopenyeka kwa marais waliokuwa nje ya ODM. Hata hivyo, hali ilianza kubadilika mwaka 2024 baada ya ushirikiano kati ya ODM na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).

Ziara ya kwanza kubwa ilikuwa Agosti 2024, ambapo Rais alizuru kaunti za Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori, akizindua miradi ya maendeleo na kuimarisha uhusiano wa kisiasa.

“Nitaenda kila kona ya nchi kuhakikisha hakuna eneo linaachwa nyuma kimaendeleo,” Rais Ruto amekuwa akisema mara kadhaa.

Hata hivyo, kauli zake zimekosolewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye amemlaumu kwa kupendelea Nyanza huku akipuuza eneo la Mlima Kenya.

Tofauti na tawala zilizopita, Rais Ruto ametumia mkakati wa ziara za mara kwa mara, akijihusisha moja kwa moja na viongozi wa eneo na masuala ya kijamii na kiuchumi.

Katika kaunti ya Homa Bay, ziara zake zimejumuisha uzinduzi wa miradi ya uchumi wa samaki, masoko ya kisasa na bandari ya Homa Bay. Kaunti hiyo pia iliandaa sherehe za Madaraka Day mwaka 2025 katika Uwanja wa Raila Odinga, hatua iliyotafsiriwa kama ishara ya mabadiliko kutoka upinzani hadi ushirikiano.

Katika kaunti ya Kisumu, miradi kama nyumba za bei nafuu na viwanda vya mchele imekuwa kiini cha ujumbe wa maendeleo. Katika Migori na Siaya, mkazo umewekwa katika unyunyuzaji, nyumba na miundombinu ya kidijitali.

Ziara ya siku nne ya Rais mwezi Machi 2026 iliyoanzia Kisumu hadi Siaya imetajwa kama mojawapo ya mikakati mikubwa zaidi ya kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo.

Viongozi wa ODM wakiongozwa na Oburu Oginga wamekuwa wakimuunga mkono Rais, wakisisitiza kuwa ziara hizo zinalenga maendeleo badala ya siasa.

Hata hivyo, si viongozi wote wanaoridhika. Gavana wa Siaya James Orengo ameonya kuwa ODM inapoteza umaarufu wake kwa kushirikiana sana na serikali.

Wakati huo huo, UDA inaendelea kujijenga kisiasa katika eneo hilo kupitia uchaguzi wa mashinani, hatua ambayo imeleta mvutano kuhusu pendekezo la kugawa maeneo ya kisiasa ili kuepusha ushindani.

Kwa Rais Ruto, mkakati huu ni jaribio la kupanua uungwaji mkono kuelekea uchaguzi wa 2027. Kwa ODM, ni fursa ya maendeleo lakini pia hatari ya kupoteza wafuasi wake wa jadi.

Wachambuzi wanasema mbinu ya Rais ni kuingiza ushawishi wake taratibu katika ngome za ODM kupitia maendeleo na ushirikiano.



from Taifa Leo https://ift.tt/oaLQNBj
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post