Bunge lakaribia kupatia NTSA nguvu kudhibiti nauli za matatu

BUNGE linakaribia kupitisha mswada utakaopatia Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) mamlaka ya kudhibiti na kuidhinisha nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa umma nchini. Mswada huo wa Marekebisho ya Sheria ya NTSA wa mwaka 2023, unaodhaminiwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, unalenga kurekebisha Sheria ya NTSA ya mwaka 2012 ili kuweka mwongozo wa kupanga na kudhibiti nauli zinazolipwa na abiria wa magari ya uchukuzi wa umma. Iwapo utapitishwa, utamaliza uhuru ambao wamiliki wa matatu wamekuwa nao kwa miaka mingi wa kupanga na kubadilisha nauli watakavyo. Kwa sasa, nauli huamuliwa na nguvu za soko, jambo ambalo limekuwa likisababisha ongezeko la bei bila utaratibu maalumu. Mswada huo unapendekeza NTSA iwe na mamlaka ya kuidhinisha nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa umma na kuwapa abiria njia rasmi ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya wanaotoza nauli kupita kiasi. Kenya itajiunga na nchi kama Ghana, Rwanda, Tanzania, Cameroon, Ivory Coast, Fiji na Ujerumani ambazo serikali hudhibiti kiwango cha chini cha nauli za usafiri wa umma. Wakati wa mjadala wa mswada huo, wabunge wengi waliunga mkono pendekezo hilo wakisema ni wakati wa kuleta utaratibu katika sekta ya matatu na kukomesha unyonyaji wa abiria kupitia nauli zisizotabirika. Bw Barasa alisema haiwezekani Kenya kuendelea kuwa nchi ambayo nauli hubadilishwa kulingana na hali ya hewa au idadi ya abiria waliopo katika vituo. “Hatuwezi kuwa na nchi ambayo leo ubao unaonyesha nauli ya Sh300, halafu mvua ikinyesha unawekwa mwingine unaosomeka Sh500. Hatuwezi kuwaacha Wakenya mikononi mwa magenge ya matatu,” alisema. Aliongeza kuwa kama serikali inavyodhibiti bei ya miwa, mafuta na bidhaa nyingine muhimu, pia inapaswa kuwalinda wananchi dhidi ya sekta ya uchukuzi. “Mkenya anapotoka nyumbani akiwa na Sh100 ya nauli hajui atatozwa kiasi gani jioni. Mswada huu utaleta usawa na kuwasaidia wananchi kupanga matumizi yao,” alisema. Mbunge wa Kesses Julius Ruto alisema kudhibiti sekta ya uchukuzi ni suala la maslahi ya umma ambalo Bunge haliwezi kulipuuza. Kwa upande wake, Mbunge wa Tigania West John Mutunga alisema imekuwa kawaida nauli kupanda bei ya mafuta inapoongezeka lakini zinakosa kushuka mafuta yanapopungua. “Hatuwezi kuruhusu matatu kubadilisha nauli watakavyo. Lazima kuwe na mfumo wa kupitia upya nauli kulingana na hali halisi,” alisema. Mbunge wa Dagoretti North Beatrice Elachi alisema kizazi kijacho kinastahili mfumo wa uchukuzi ulio na utaratibu. “Lazima tuweke sheria zitakazoongoza sekta hii hata kama wahudumu wa matatu ni wapiga kura wetu. Tunahitaji mfumo wenye nidhamu,” alisema. Pia alipendekeza kanuni hizo ziwahusu makanga wanaowanyanyasa abiria. Mbunge Maalum Sabina Chege alisema ni wajibu wa Bunge kuwalinda watumiaji wa huduma za uchukuzi dhidi ya kutozwa nauli kiholela. Hata hivyo, mswada huo umepingwa na Kamati ya Bunge ya Uchukuzi na pia aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen. Murkomen aliambia kamati ya Bunge mwaka 2023 kuwa kabla ya serikali kuanza kudhibiti nauli, lazima ifanye utafiti wa kina na mashauriano na wadau wote ili kubaini iwapo mfumo huo unaweza kutekelezwa bila kukiuka sheria na mikataba ya kimataifa. Mwaka 2018, Bunge lilikataa pendekezo kama hilo la Wizara ya Uchukuzi la kumpa Waziri mamlaka ya kudhibiti nauli za matatu. Pia Chama cha Wamiliki wa Matatu kilipinga pendekezo hilo mwaka 2020.

from Taifa Leo https://ift.tt/IklfSBg
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post