Serikali yatumia miradi kuvutia UDA kura Ol Kalou

CHAMA cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto kinafanya juu chini kuhakikisha kinashinda uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou ikiwemo kutumia miradi kuwavutia wapigakura. Uchaguzi mdogo utafanyika mnamo Julai 16 na maafisa wa ngazi ya juu serikalini, makatibu wa wizara na viongozi wengine katika utawala wa sasa wamekuwa wakizindua miradi ya maendeleo. Tabia hii inaonekana kama njama ya kuwashawishi wapigakura kumchagua mgombea wa UDA. Matokeo ya uchaguzi huo ni muhimu kwa Rais Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pande zote mbili zikisaka uungwaji mkono Mlima Kenya kuelekea uchaguzi wa 2027. Waziri wa Ardhi, Alice Wahome na mwenzake wa Utalii, Rebecca Miano ni kati ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini ambao wamezuru Ol Kalou kuzindua miradi ya maendeleo. Waziri wa zamani, Moses Kuria pia amekita kambi Ol Kalou wakati wa kuzindua miradi ya maendeleo. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki hajaonekana sana Ol Kalou akishiriki kampeni jinsi alivyofanya Mbeere Kaskazini. Wikendi iliyopita, Bi Wahome aliwaongoza Bi Miano, Bw Kuria, Katibu wa Wizara ya Ardhi Nixon Korir, Gavana wa Nyandarua, Kiarie Badilisha na Katibu wa Wizara ya Barabara, Joseph Mbua kufungua afisi ya ardhi Nyandarua. Wakuu hao wa serikali walitumia hafla hiyo kutoa vyeti vya ardhi kwa wenyeji huku Bi Wahome akitaja tukio hilo kama la kihistoria. “Tumetoa vyeti 2700 kwa wanaotoka vijiji vya kikoloni na sasa ardhi walikokuwa wakiishia kama maskwota ni zao,” akasema. “Kati ya rekodi na stakabadhi za ardhi 400,000, stakabadhi 296,000 zimehamishwa kutoka Nyahururu hadi Ol Kalou na kuleta huduma karibu na mwananchi,” akaongeza. Bi Miano alisema kufunguliwa kwa afisi hiyo ya ardhi kutawaepushia wakazi kazi ngumu ya kusafiri hadi Nyandarua wakisaka hudumu katika sajili ya ardhi . Mnamo Juni 2, Bi Miano alikuwa katika eneobunge hilo kufungua kituo cha reli cha Ol Kalou katika kile kilichoonekana kama mikakati ya kuwavutia wapigakura. Mbunge wa Gatanga, Edward Muriu, mwandani wa Bw Gachagua amepuuza UDA akisema kuwa wenyeji hawatashawishiwa na miradi kumchagua mgombeaji wa UDA. “Miradi gani unazungumzia? Magodoro, blanketi na Sh500? Watu wa Mlima wanathamini staha kuliko kitu chochote kile,” akasema Bw Muriu. “Hata ujenge barabara za dhahabu, mfereji wa maziwa na umewasaliti, umewaua watoto wao, ukawaibia na kuua ndoto za watoto wao, watachukua pesa na miradi kisha wampigie kura mwaniaji wao,” akaongeza. Ushindani mkali kwenye uchaguzi huo mdogo unaonekana kuwa kati ya Kamau Ngotho wa DCP na Samuel Muchina wa UDA.

from Taifa Leo https://ift.tt/2G4WAJh
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post