Waathiriwa wa maandamano ya 2024 wataka KNCHR iweke wazi orodha ya watakaopata fidia

KENYA inapojiandaa kwa maadhimisho ya pili ya waliouawa wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z mnamo 2024, waathiriwa wanataka Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) iweke wazi orodha ya watakaonufaika.
Baadhi ya waathiriwa kutoka Nairobi wamesimulia makovu wanayoishi nayo tangu siku hiyo kutokana na madhila waliyotendewa.
Hawa Sheila, 26 kutoka Mathare, anakumbuka kwa uchungu siku hiyo ambayo ilibadilisha maisha yake milele. Sasa ni kipofu anayetegemea misaada ya wasamaria wema, na watoto wake wadogo.
Maandamano ya 2024 yalimsababishia upofu baada ya kugongwa usoni na kopo la gesi ya kutoza machozi lililolipuka.
Wakati taifa likielekeza macho yake kwenye orodha ya wanaotarajiwa kunufaika kwa fidia, ametamauka kwa sababu hawezi kuwaona wanawe tena.
“Sina pesa za matibabu japo namshukuru Mungu kwamba niko hai, lakini natamani kurejelea maisha yangu ya kawaida, niwatunze watoto wangu na kuwaona tena. Sasa nawategemea majirani hata kwa mambo madogo,” akasema Bi Hawa.
Ingawa hakuwa miongoni mwa waandamanaji, mama huyo wa watoto watatu anaishi na ulemavu wa kudumu.
Sasa anataka kujua ikiwa jina lake lipo kwenye orodha ya watakaopokea fidia.
Wiki jana, KNHCR ilitangaza kuwa imekamilisha mchakato wa kuwatambua waathiriwa watakaonufaika kwa Sh2 bilioni kutoka kwa serikali. “Ninataka pia kunufaika ili niwatunze watoto wangu na kujitunza mwenyewe,” akaongeza.
Alex Munyua, ambaye pia alipigwa risasi wakati wa maandamano katika mtaa wa Pipeline, Nairobi, alishangaa kwa nini tume hiyo imechukua muda mrefu kuchapisha orodha ya wanaolipwa fidia.
 “Nilipoteza kazi yangu baada ya kukaa hospitalini kwa wiki mbili. Niliwasilisha maelezo yangu kwa ajili ya fidia lakini bado sijajibiwa,” akasema.
Afisa wa Tume ya Kutetea Haki Kenya (KHRC), Ojiro Odhiambo, alisema Sh2 bilioni hazitoshi ikilinganishwa na idadi ya waliouawa, kujeruhiwa au kuathirika kisaikolojia.
Kulingana naye, waathiriwa wengi bado wanaendelea na matibabu na wanahitaji msaada badala ya malipo ya mara moja.
“Wana majeraha na wengi bado wanapitia ushauri nasaha. Wanapaswa kusaidiwa hadi wapone,” akasema.
Pia alikosoa mchakato uliotumika kuwateua waathiriwa wapatao 2,000, akisema wengi wao hawangeweza kutimiza masharti yaliyowekwa.
Aliongeza kuwa sharti la kuwasilisha nambari ya OB limewafungia nje waathiriwa wengi, hasa katika maeneo ambapo vituo vya polisi havikutoa usaidizi unaohitajika.
“Kuna masharti mengi ya kisheria ilhali ushahidi upo hadharani. Kwa nini KNCHR inategemea zaidi taasisi za serikali? Baadhi ya waathiriwa hawaamini rekodi za polisi kwa sababu baadhi ya matukio yalirekodiwa kimakosa kama ajali,” akasema.
KHRC pia inataka ujenzi wa minara ya kumbukumbu katika sehemu mbalimbali za nchi kuenzi waliopoteza maisha yao wakati wa maandamano hayo.
Mtaani Kitengela, Emily Ochieng, 24, anakumbuka jioni ya Juni 25, 2024, siku ambayo anasema ilibadili maisha yake milele wakati wa maandamano hayo yaliyageuka vurugu. Siku hiyo, mumewe Evan Odour, 27, alipigwa risasi na kuuawa saa 12 jioni mjini Kitengela.
Bi Ochieng alisema mumewe, aliyekuwa makanika katika Barabara ya Old Namanga, ndiye aliyekuwa tegemeo wa familia.
“Mume wangu aliondoka nyumbani kama kawaida. Sikujua kwamba hiyo ndiyo ingekuwa mara ya mwisho kumuona akiwa hai,” akasema.
 “Asubuhi nilikuwa na mume, kufikia jioni nilikuwa mjane.”
Aliongeza kuwa bado anahangaika kukabiliana na maumivu ya kutazama mwili wa mumewe kwenye mochari.
Tangu wakati huo, amesema imekuwa vigumu kuwalea watoto wake, akilazimika kumpa mamake watoto wawili mashambani naye akisalia na mmoja Kitengela.
“Siwezi kumudu nyumba nzuri wala chakula cha kutosha kwa ajili yangu na mtoto ninayeishi naye,” akasema
Mjane mwengine, Khadija Riami, 24, alisema maumivu ya kumpoteza mumewe Vincent Ayamo, 28, bado yamemlemea. Alisema mumewe, ambaye alikuwa mekanika mjini Kitengela, alipigwa risasi na kuuawa alipokuwa akirejea nyumbani. Kifo chake kimemuacha akitegemea vibarua kujikimu.
Ingawa hivyo, baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa kidini Kitengela wamepinga maadhimisho ya Juni 25 wakisema yanaweza kusababisha vurugu na kuvuruga shughuli za kiuchumi.


from Taifa Leo https://ift.tt/o5AJdpP
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post