Sifuna bado kikaangoni baada ya ODM kupewa ruhusa ya kumwadhibu

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na maamuzi muhimu ya kisiasa baada ya Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) kuruhusu chama cha ODM kuendelea na mchakato wa kinidhamu dhidi yake.
Uamuzi huo umeongeza presha kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye kwa sasa ni mmoja wa viongozi wa upinzani wanaovutia vijana wengi kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya serikali ya Rais William Ruto na baadhi ya viongozi wa ODM.
ODM imekuwa ikimlaumu Sifuna kwa kupinga hadharani msimamo wa chama kuhusu ushirikiano kati ya chama hicho na serikali. Chama kinadai amekuwa akikiuka misimamo ya chama, kuhudhuria shughuli za kisiasa ambazo hazijaidhinishwa na pia kukosa baadhi ya mikutano rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa ODM, Oduor Ong’wen, amesema uamuzi wa PPDT umeonyesha kuwa migogoro ya chama inapaswa kwanza kushughulikiwa kupitia mifumo ya ndani kabla ya kupelekwa nje.
Hata hivyo, kwa Sifuna, suala kubwa si tu mchakato wa kinidhamu bali mustakabali wake wa kisiasa.
Wachambuzi wa siasa wanasema sasa analazimika kuamua iwapo ataendelea kubaki katika ODM na kupigania nafasi yake ndani ya chama au aanze safari mpya ya kisiasa nje ya chama hicho.
Njia ya kwanza ni kubaki ODM na kupambana kutoka ndani. Mchambuzi Mark Bichachi anaamini kuondoka chama kwa sasa kunaweza kuwa hatari kwani kunaweza kusababisha uchaguzi mdogo wa useneta wa Nairobi.
Kwa maoni yake, kubaki ODM kunampa Sifuna muda wa kujijenga zaidi huku akiendelea kufaidika na mtandao na miundo ya chama hicho kikubwa.
Njia ya pili ni kutetea kiti chake cha Seneta wa Nairobi 2027 na kujitayarisha kwa nafasi kubwa zaidi 2032. Wachambuzi wengi wanaona hii kuwa njia salama zaidi kwake.


from Taifa Leo https://ift.tt/glap2PQ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post