
IMEBAINIKA kuwa uamuzi wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kujifungia katika kijiji chake cha Wamunyoro kwa siku 45 katika kile alichokiita “mchakato mpana wa mashauriano” na washirika wake wa kisiasa, kwa hakika ni mpango wa kudhibiti mgogoro wa kisiasa unaomkabili.
Bw Gachagua alianza “mikutano yake ya siri” Juni 16 na anatarajiwa kurejea kwenye majukumu ya hadhara Julai 31, huku Rais William Ruto—ambaye anaonekana kuwa ajenda kuu ya mkutano huo wa Wamunyoro—akimuonya akisema “hujui unayeshughulika naye” na “nitahakikisha hautakuwa chochote katika nchi hii”.
Bw Gachagua, ambaye alitimuliwa kwa njia ya kumwondoa madarakani mwaka 2024 baada ya kuhudumu kwa miaka miwili kama Naibu Rais, amekuwa akipambana na misukosuko minne mikuu ya kisiasa: kesi ya kuondolewa kwake madarakani, ushindani na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu uongozi wa eneo la Mlima Kenya, mrithi wake Profesa Kithure Kindiki kuvutia Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto kwa uchaguzi wa 2027, na pia fuko ambao wako tayari ndani ya kambi yake.
Amepoteza kesi Mahakama Kuu aliyopinga kuondolewa kwake mamkakani, kukabiliana na mgombea anayependelewa na Bw Kenyatta, Dkt Fred Matiang’i, pamoja na mikakati ya wafuasi wa Prof Kindiki ya kugawanya Mlima Kenya kuwa kanda za Mashariki na Magharibi. Aidha, anakumbana na uasi kutoka ndani ya chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP).
Mlima Kenya pia unakumbwa na changamoto ya wanasiasa maarufu kama aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, ambao kwa kiasi kikubwa hawajaegemea upande wowote lakini wana uwezo wa kugawa kura iwapo wataamua kwenda kinyume na mwelekeo wa Bw Gachagua.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei amewahi kusema: “Tutahakikisha tunapata wagombea wanaomuunga mkono Rais Ruto kushindana katika maeneo ya Mlima Kenya huku wakishirikiana na vyama vya upinzani.”
Kauli hiyo imewafanya viongozi kama Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata kuonya kuwa inazidi kuwa wazi kwamba wapiga kura wa Mlima Kenya wanataka viongozi wenye msimamo ulio wazi, hasa wanaomuunga mkono Bw Gachagua na chama chake cha DCP.
Ni katika mazingira hayo ndipo inadaiwa Bw Gachagua aliamua kusitisha mikutano yake ya hadhara na kurejea Wamunyonyoro kwa mazungumzo ya karibu na jamii yake, kabla ya kuanza majadiliano na washirika wengine wa kisiasa kuhusu kuunda muungano na hatimaye kumpata mgombea mmoja wa urais atakayekabiliana na Rais Ruto.
Kwa mujibu wa Bw Maina Kamanda, mwenyekiti wa Baraza la Wazee katika DCP, mkutano huo wa Wamunyonyoro ni zoezi la kupanga upya uongozi wa jamii linalolenga kufikia msimamo mmoja kuhusu muundo wa miungano ya kisiasa kuelekea 2027.
“Masuala kadhaa yanahitaji makubaliano. La kwanza ni suala uongozi wa jamii, chama cha kisiasa cha jamii na masharti yasiyoweza kubadilika katika ujenzi wa miungano. Tunataka kukubaliana kwamba kituo chetu cha uongozi ni Wamunyonyoro, chama chetu ni DCP, na kuhakikisha makosa ya miungano ya 2022 hayajirudii,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo vilivyo karibu na “mapumziko” hayo ya kisiasa, Gachagua anatarajiwa kuimarisha DCP kuwa chaguo kuu la wagombea, kuandaa orodha ya masharti ya mazungumzo ya kisiasa, kufafanua jinsi Mlima Kenya utaingia kwenye muungano, na kuweka vipaumbele vitatu vya juu kwa tiketi ya urais.
Aidha, atabuni mbinu ya kuchagua mmoja kati ya wagombea watatu watakaopendekezwa, pamoja na mkakati iwapo tiketi hiyo haitamwendea mwanasiasa wa Mlima Kenya, na jinsi ya kuandaa makubaliano rasmi (MoU) na mgombea atakayekubaliwa.
Gachagua pia anatarajiwa kuwashawishi wafuasi wake kwamba ana uwezo wa kifedha kushindana na serikali iliyoko madarakani, pamoja na kuhakikisha uteuzi wa haki licha ya uwezekano wa kugawanywa kwa maeneo au uteuzi wa pamoja.
Pia anatarajiwa kueleza namna ya kupanua ushawishi wake katika maeneo ya Pwani, Bonde la Ufa na Nairobi, ambako DCP inaweza kulazimika kuingia katika miungano midogo ndani ya muungano mkubwa, pamoja na kuwahakikishia wafuasi wake kuhusu mgao wa madaraka baada ya uchaguzi.
Mlima Kenya unakabiliwa na changamoto ya kuamua nani wa kumuunga mkono ndani ya upinzani, ambapo vigogo wake ni Gachagua, Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Edwin Sifuna, Eugene Wamalwa na George Natembeya, huku Rais Ruto akijaribu kushawishi sehemu ya kura za eneo hilo ambalo lilimpa asilimia 87 ya kura mwaka 2022.
Gachagua ameonyesha kuwa kazi iliyo mbele yake Wamunyonyoro si rahisi, hasa kwa kuwa kesi yake bado inaendelea katika Mahakama ya Rufaa na huenda ikaenda hadi Mahakama ya Juu, jambo linaloweza kumzuia kushikilia wadhifa wa umma hadi 2035.
Anakabiliwa pia na jukumu la kuwashawishi wafuasi wake kwamba uongozi unaweza kuendelea hata nje ya mamlaka rasmi.
“Nina kesi mahakamani na kama itaenda kinyume changu, bado naweza kuongoza kutoka Wamunyonyoro kama Raila Odinga alivyofanya bila kuwa serikalini,” alisema.
Hata hivyo, Mbunge wa Kinangop Njuguna Njohi alisema ujumbe wao wa kwanza ulifika Wamunyonyoro Juni 16, ambapo walijadili mkakati wa 2027 na uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.
“Tulitoka tukijua tumekutana na kiongozi anayejitolea kwa maslahi ya taifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Wachira Kiago alisema jamii imeunga mkono ajenda hiyo ya umoja wa Mlima Kenya kuelekea 2027, akisisitiza lengo la kupata kura zaidi ya asilimia 95 kwa mgombea mmoja wa urais.
Hata hivyo, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri amekosoa mikakati hiyo akisema Gachagua bado hajapewa mamlaka ya kuongoza eneo hilo rasmi.
from Taifa Leo https://ift.tt/GT8Jl12
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS