Wanasiasa, watetezi warushia Gen Z ndoana maandalizi ya kumbukumbu ya Juni, 25 yakishika kasi

MIAKA miwili tangu maandamano ya Gen Z yaliyotikisa nchi yafanyike, mvutano umeibuka kati ya wanasiasa wa upinzani na wanaharakati kuhusu nani anapaswa kuongoza maadhimisho ya maandamano hayo.
Huku maandalizi ya kumbukumbu ya Juni 25 yakizidi kushika kasi, imebainika kuwa baadhi ya wanasiasa wanataka maandamano ya siku tatu kuanzia Juni 24 hadi 26, kupinga kile wanachokiita utawala mbovu nchini.
Katika maandamano ya kihistoria ya kupinga Mswada wa Fedha wa Juni 25, 2024, Gen Z walijitokeza kama kundi lisilo na uongozi, lakini sasa wanasiasa wanataka kuingiza ushawishi wao na kuongoza mwelekeo wa harakati hizo kuelekea uchaguzi wa 2027.
Waandalizi wa maadhimisho hayo wanapanga “maandamano ya kumbukumbu” ya kuwaenzi waliouawa mnamo 2024, huku baadhi ya wanasiasa wakitaka kutumia tukio hilo kupata mtaji wa kisiasa.
“Tunalenga kufanya maandamano ya amani Juni 25 kuadhimisha miaka miwili ya maandamano ya 2024. Tunataka serikali iharakishe fidia na haki kwa wahanga,” alisema kiongozi wa vijana David Kimani, akisisitiza kuwa hawataki wanasiasa kuingilia mchakato huo.
Hata hivyo, maandamano hayo yameanza kuchochewa pia na malalamiko mapya kuhusu gharama ya maisha, kupanda kwa bei ya mafuta, ufisadi na madai ya utawala mbovu chini ya Rais William Ruto.
Wanaharakati wa haki za binadamu nao wanasema hali ya kutoshughulikiwa kwa kesi za ukatili wa polisi inaongeza hasira mpya miongoni mwa wananchi.
“Matukio ya hivi karibuni ya ukatili wa polisi na ongezeko la bei ya mafuta yamechochea hasira mpya,” alisema mwanaharakati David Kuria.
Mwanaharakati Boniface Mwangi alisema maandamano hayo yatatumika kudai mwisho wa ukatili wa polisi, akitaja matukio ya hivi majuzi yaliyosababisha vifo na majeruhi katika maandamano mbalimbali.
Alitaja tukio la Mei 18, 2026 ambapo watu waliokuwa wakipinga ongezeko la bei ya mafuta walipigwa risasi na wengine kuuawa au kujeruhiwa, akisema hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika. Pia alitaja vifo vilivyotokea katika maandamano ya kupinga ujenzi wa kituo cha karantini ya Ebola Nanyuki, Kaunti ya Laikipia. “Kwa haya yote, tuna haki ya kuungana na kujitokeza mitaani kudai mabadiliko,” alisema. Muungano wa Wahanga na Waathiriwa wa Ukatili wa Serikali pia umesema utashiriki maandamano hayo kudai fidia na haki kwa waathiriwa wa zamani. Katika barua yao kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, walisema wataandamana kudai ratiba ya wazi ya utekelezaji wa fidia na uwazi kuhusu fedha zilizotengwa na matumizi yake. “Tutatumia maandamano kushinikiza ratiba ya utekelezaji wa fidia na ufichuzi kamili wa fedha zote zilizotengwa,” ilisema barua hiyo.
Kwa upande wa kisiasa, makundi ya upinzani yakiwemo Linda Mwananchi la ODM, chama cha DCP kinachoongozwa na Rigathi Gachagua na Wiper cha Kalonzo Musyoka yamesema yataungana na Gen Z katika maadhimisho hayo.
Katibu wa mipango wa DCP, Dkt Peter Mbae alisema watawaunga mkono Gen Z, ingawa si lazima wawe barabarani moja kwa moja.
“Sisi tutakuwa pamoja na Gen Z wakati wa maadhimisho ya Juni 25. Huenda hatutakuwa barabarani moja kwa moja, lakini tutawaunga mkono,” alisema.
 Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kundi lake litashiriki moja kwa moja katika maadhimisho hayo.
“Linda Mwananchi itakuwa pamoja na Gen Z. Ni lazima tusimame na Wakenya pale ambapo kuna matumizi mabaya ya mamlaka,” alisema.
Wakati huo huo, Gavana wa Siaya James Orengo anasema maandamano yanaweza kuendelea kwa siku tatu, kupinga “utawala mbovu”.
Alisema upinzani utaendelea kushinikiza mabadiliko na hawataogopa serikali. Kwa mujibu wa wachambuzi, vijana wa Gen Z wanaonekana kuwa nguvu kubwa ya kisiasa kuelekea 2027, huku wakitarajiwa kuamua hatma ya washindi wa viti tofauti katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu, takriban watu 60 waliuawa katika maandamano ya 2024, huku wengine wakitoweka au kujeruhiwa.
Nairobi sasa iko katika hali ya tahadhari huku maadhimisho hayo yakikaribia, yakichanganya kumbukumbu, siasa na hasira za kijamii.


from Taifa Leo https://ift.tt/ej1r84w
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post