Wakulima wahimizwa kupanda miti zaidi ya matunda kukabili mabadiliko ya tabianchi

WAKULIMA nchini wamehimizwa kupanda miti zaidi, hasa ya matunda kama vile maparachichi au avokado, ili kuchangia kuongezeka kwa misitu huku wakijiongezea kipato kupitia mazao ya kibiashara. Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Ushirika Kenya (Co-operative Alliance of Kenya - CAK), Daniel Marube, anasema miti ya matunda ina faida maradufu katika kuongezea kiwango cha misitu na wakati huo huo kuwapa wakulima mapato kutokana na mauzo ya matunda. Akizungumza wakati wa shughuli ya upanzi wa miti iliyoandaliwa na Baraza la Kitaifa la Ushirika (National Ushirika Council), Muungano wa Vyama vya Ushirika Kenya (CAK), pamoja na wadau wengine mnamo Jumamosi, Juni 20, 2026 ASK Jamhuri Grounds, jijini Nairobi, Marube alisema sekta ya ushirika imejitolea kuunga mkono juhudi za serikali kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. “Wakulima wengi nchini ni wanachama wa vyama vya ushirika. Tunawahimiza wapande miti zaidi, hasa ile ya matunda kama vile maparachichi, kwa sababu ni miti inayochangia uhifadhi wa mazingira na pia ni chakula na chanzo cha mapato,” alisema. Aidha, himizo hilo linajiri wakati ambapo serikali inaendeleza kampeni ya upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032, ambayo ilizinduliwa na Rais William Ruto 2022. Marube alifichua kuwa karibu miti 5,000 ilipandwa katika hafla ya Jumamosi iliyofanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Kujenga Madaraja, Kuonyesha Ustahimilivu wa Ushirika”, ambayo inalenga kuangazia nafasi ya vyama vya ushirika katika kuimarisha umoja wa kitaifa, utangamano wa kijamii na utunzaji wa mazingira. [caption id="attachment_189373" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Ushirika Kenya (CAK), Daniel Marube, akizungumza na wanahabari katika hafla ya vyama vya ushirika nchini kuzindua maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Ushirika kupitia mpango wa kitaifa wa uhifadhi wa mazingira uitwao Siku ya Mazingira ya Ushirika (Ushirika Environmental Day) mnamo Juni 20, 2026. Hafla hiyo ilijumuisha upandaji miti katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo na Biashara, ASK Ground, Jamhuri, Nairobi, pamoja na shughuli nyingine za uhifadhi wa mazingira kote nchini. PICHA|EVANS HABIL|NATION[/caption] Kulingana na Marube, zaidi ya watu 5,000 walishiriki katika shughuli hiyo, huku kila mmoja akipanda kati ya mti mmoja na mitatu. “Wanafunzi kutoka Cooperative University of Kenya, pamoja na vijana wanaojihusisha na shughuli za ushirika walikuwa miongoni mwa waliosaidia kutekeleza zoezi la upanzi wa miti,” alidokeza. Alisema vyama vya ushirika (SACCO) vilijitolea mwaka 2015 kushiriki kikamilifu katika juhudi za kimataifa kuhifadhi mazingira, na shughuli ya sasa ni mwendelezo wa ahadi hiyo. Marube alieleza kuwa kwa karibu muongo mmoja sasa, wanachama wa vyama vya ushirika nchini wamekuwa wakipanda miti ASK Ground, hatua ambayo imebadili kwa kiasi kikubwa mandhari ya mazingira. Alikadiria kuwa zaidi ya miti 30,000 imepandwa tangu mpango huo ulipoanzishwa. ASK Ground, Nairobi, kila mwaka huandaa maonyesho ya kilimo na biashara. “Tunajivunia kuwa karibu asilimia 90 ya miti tuliyopanda imeendelea kukua. Hii ni kutokana na uwekezaji katika matunzo, umwagiliaji maji wakati wa kiangazi na usimamizi bora wa miti hiyo,” alisema. Aliongeza kuwa miti iliyopandwa miaka ya awali sasa imekomaa na kusaidia kuunda msitu wenye uoto wa kutosha. Katika mipango ya siku zijazo, Marube alisema vyama vya ushirika vinazungumza na serikali ili vipatiwe eneo kubwa zaidi, hasa katika eneo la Ngong Hills, kwa lengo la kuanzisha “Msitu wa Ushirika” ambao utakuwa kitovu cha shughuli za upandaji miti. Aidha, afisa huyo alielezea imani yake kwamba sekta ya ushirika inaweza kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha lengo la kitaifa la kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032. [caption id="attachment_189374" align="aligncenter" width="300"] Naibu Mwenyekiti wa Mhasibu Sacco Society Limited, CPA Joyce Githuo (kushoto), na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Unaitas Sacco, Michael Muriithi, wakipanda mti katika hafla ya vyama vya ushirika nchini kuzindua maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Ushirika kupitia mpango wa kitaifa wa uhifadhi wa mazingira uitwao Siku ya Mazingira ya Ushirika (Ushirika Environmental Day) mnamo Juni 20, 2026. Hafla hiyo ilijumuisha upandaji miti katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo na Biashara, ASK Ground, Jamhuri, Nairobi, pamoja na shughuli nyingine za uhifadhi wa mazingira kote nchini. PICHA|EVANS HABIL|NATION[/caption] Alisema vyama vya ushirika vina uwakilishi katika kila kaunti nchini na kwamba SACCO nyingi, pamoja na vyama vya ushirika tayari vimekusanya fedha za kugharamia shughuli za upandaji miti. Hata hivyo, Marangu hakufichua kiwango cha pesa wanachotumia kila mwaka. “Wanachama wengi wa vyama hivyo ni wakulima wa mashamba madogo ambao maisha yao yanategemea hali nzuri ya hewa. Hivyo, kupanda miti ni uwekezaji muhimu kwa ustawi wa sekta ya kilimo.” Wakati huo huo, Mkurugenzi anayesimamia Kitengo cha Masuala ya Ushirika katika Benki ya Co-operative, Vincent Marangu aliambia wanahabari kuwa harakati za ushirika zinaweza kuchangia angalau asilimia 20 ya lengo la kitaifa la miti bilioni 15, na huenda mchango huo ukafikia kati ya asilimia 40 na 45 kupitia vyama vya ushirika vya kilimo na wakulima wanaopanda miti ya kibiashara. Aidha, afisa huyo alishauri vyama vya ushirika kukaza kamba kampeni kuhakikisha lengo la upanzi miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032 linatimia. Vyama vya ushirika vinaendelea kushirikiana na maafisa wa nyanjani wa kilimo, pamoja na serikali za kaunti kuhamasisha wakulima kupanda mimea inayostahimili mabadiliko ya tabianchi na kuongeza idadi ya miti katika mashamba na makazi yao.  

from Taifa Leo https://ift.tt/3YLmGR1
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post