Wetang’ula awataka Wakenya kukataa siasa za ukabila, uhuni

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewataka Wakenya kukataa siasa za ukabila na badala yake kuimarisha umoja wa kitaifa, akisema mustakabali wa nchi unategemea viongozi na wananchi kuweka maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kikabila na kisiasa. Akizungumza Likoni, Kaunti ya Mombasa, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa Shirika la Kijamii la Salute (CBO), Wetang’ula alisema maendeleo ya Kenya yatawezekana tu kupitia umoja, mshikamano na kuheshimu ushindani wa kidemokrasia. “Kenya ni kubwa kuliko mtu yeyote na uongozi hutoka kwa Mungu. Lazima tuunganishe taifa tunapoendelea kujenga nchi ya kisasa na yenye maendeleo,” alisema. Spika huyo alisisitiza kuwa jamii zote nchini zina haki sawa na hakuna kabila lililo kubwa au dogo kuliko jingine. “Hakuna kabila dogo wala kubwa nchini Kenya. Kila jamii ina haki ya kuongoza taifa hili. Tunapaswa kushindana kisiasa wakati wa uchaguzi, lakini baada ya matokeo kutangazwa tukumbatiane na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya nchi,” alisema. Wetang’ula pia alikosoa wanasiasa wanaodaiwa kufadhili magenge ya vijana kusababisha fujo na vurugu za kisiasa. “Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wanasiasa wakiajiri wahuni kuvuruga amani ambayo tumepigania kwa muda mrefu. Ikiwa wanataka wahuni, waajiri watoto wao wenyewe na si watoto wasio na hatia wa taifa hili,” alisema. Spika huyo alimpongeza aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kile alichokitaja kuwa kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. “Baada ya ushindani wa kisiasa wa mwaka 2022 kumalizika, Raila alionyesha kwamba Kenya ni kubwa kuliko mtu yeyote. Huo ndio moyo uliochangia kuzaliwa kwa serikali jumuishi inayowapa nafasi viongozi kutoka pande tofauti za kisiasa kuhudumia wananchi,” alisema. Kuhusu uchumi, Wetang’ula alisema ana matumaini kuwa Kenya iko kwenye mkondo wa ukuaji wa uchumi na ustawi. Alisema serikali ya Rais William Ruto imeweka msingi wa mageuzi ya kiuchumi huku taasisi za kidemokrasia zikiendelea kuimarika. Naye Spika wa Seneti Amason Kingi alisema eneo la Pwani halitaunga mkono siasa za ukabila kwa kuwa ni eneo lenye watu wa jamii mbalimbali. “Pwani ni eneo la watu wa tamaduni na makabila tofauti. Hatuwezi kurudi katika siasa za kugawanya Wakenya kwa misingi ya ukabila,” alisema. Waziri wa Madini Hassan Joho alimshukuru Rais Ruto kwa kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanapata nafasi sawa katika maendeleo. Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, ambaye alikuwa mwenyeji wa hafla hiyo, alimshukuru Wetang’ula kwa ushauri na mwongozo wake wa kisiasa, akisema viongozi wana wajibu wa kuunga mkono wale waliowasaidia kufikia nafasi walizo nazo.

from Taifa Leo https://ift.tt/nUpy9bl
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post