Wataalam waonya kuhusu maambukizi ya Kaswende jiji la Nairobi likiongoza

IDADI ya Wakenya wanaojitokeza kupimwa ugonjwa wa kaswende imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi majuzi, huku wataalamu wa afya wakionya kuwa watoto wengi bado wanazaliwa na maambukizi hayo kwa sababu mama zao hawakupimwa wala kutibiwa wakati wa ujauzito. Takwimu mpya kutoka Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Zinaa (NSDCC), zinaonyesha kuwa watu wengi zaidi sasa wanatafuta huduma za kupimwa kaswende katika vituo vya afya kote nchini. Visa vingi vimeripotiwa katika miji mikubwa, maeneo yenye shughuli nyingi za usafiri na vijiji vya mbali.Mwaka 2020, wahudumu wa afya walipima watu1.29 milioni. Kufikia mwaka 2025, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi watu 1.42 milioni. Kadri watu wengi walivyoendelea kupimwa, ilibainika kuwa ugonjwa huo ulikuwa tayari umeenea katika jamii lakini visa vingi havikuwa vimegunduliwa. Licha ya ongezeko la vipimo, idadi ya waliopatikana na maambukizi imepungua. Mwaka 2020, karibu Wakenya 16,000 walipatikana na kaswende. Kufikia mwaka 2025, idadi hiyo ilishuka hadi zaidi ya watu 9,000, sawa na kupungua kwa zaidi ya asilimia 40.Hata hivyo, kaunti 15 zilirekodi visa vya juu au vinavyoendelea kuongezeka. Wataalamu wanasema hali hiyo inachangiwa na ongezeko la uhamaji wa watu mijini, mifumo dhaifu ya ufuatiliaji wa magonjwa na ukosefu wa vifaa vya kupimia na kutibu ugonjwa huo. Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa vingi zaidi nchini. Mwaka 2023, visa 961 vilirekodiwa huku mwaka 2025 idadi hiyo ikiongezeka hadi 1,068 kati ya watu 161,020 waliopimwa. Ripoti ya NSDCC inaeleza kuwa Nairobi ni kitovu kikubwa cha usafiri na biashara ambapo maelfu ya watu huingia na kutoka kila siku, jambo linalorahisisha kusambaa kwa maambukizi. Ingawa Nairobi ina visa vingi zaidi, Kaunti ya Homa Bay ina kiwango kikubwa zaidi cha maambukizi. Mwaka 2025, watu 37,348 walipimwa na 508 kupatikana na ugonjwa huo, kiwango cha asilimia 1.4 ambacho ni mara mbili ya kile cha Nairobi. Kaunti za Uasin Gishu na Machakos pia zimeibua wasiwasi baada ya kurekodi ongezeko la ghafla la visa. Uasin Gishu ilikuwa na visa 152 mwaka 2024 na visa 489 mwaka 2025, huku Machakos ikiongeza visa kutoka 62 hadi 157 katika kipindi hicho. Wataalamu wa afya wanasema ongezeko hilo linaashiria kuwa ugonjwa huo ulikuwa ukisambaa kimyakimya katika jamii kabla ya kugunduliwa kupitia vipimo. Kaswende ni hatari zaidi kwa wanawake wajawazito kwani inaweza kuambukizwa mtoto akiwa tumboni. Ugonjwa huo unaweza kusababisha mimba kuharibika, mtoto kuzaliwa mfu, kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa au kupata ulemavu mkubwa. Katika Kaunti ya Nakuru, wanawake wajawazito 309 walipatikana na maambukizi ya kaswende mwaka 2024. Ingawa idadi hiyo ilipungua kutoka visa 474 mwaka uliotangulia, maafisa wa afya wanasema bado ni kiwango cha kutisha. Mkurugenzi Mkuu wa NSDCC, Dkt Douglas Bosire, alisema hatua kali za afya ya umma zinaweza kupunguza maambukizi kwa haraka.Alitaja Turkana kama mfano ambapo visa vilipungua kutoka 1,182 mwaka 2023 hadi 540 mwaka 2025 baada ya kampeni kali za upimaji, matibabu na elimu kwa jamii. Kaunti za Kakamega, Bungoma na Narok pia zimefanikiwa kupunguza visa vya ugonjwa huo kupitia juhudi za upimaji na matibabu ya mapema. Wizara ya Afya na NSDCC sasa zimezindua Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kudhibiti Magonjwa ambao unalenga kaswende, Ukimwi, Kifua Kikuu na homa ya ini chini ya mfumo mmoja. “Kenya inalenga kupunguza kiwango cha kaswende miongoni mwa wajawazito hadi chini ya asilimia moja kufikia mwaka 2030,” alisema Dkt Bosire. Aliongeza kuwa kaunti zote zimeagizwa kuhakikisha vipimo vya kaswende vinapatikana katika huduma za kawaida za afya, huku akiba ya vifaa vya kupimia na dawa ikidumishwa wakati wote.Wataalamu wanaamini kuwa kwa kuimarisha upimaji wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa, Kenya inaweza kudhibiti ugonjwa huo na kuzuia watoto wengi kuzaliwa wakiwa na maambukizi yanayoweza kuzuiliwa.  

from Taifa Leo https://ift.tt/R02NX1S
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post