Wabunge 186 wahepa kikao cha Mswada wa Fedha

WABUNGE kadhaa akiwemo Ndindi Nyoro (Kiharu), Kareke Mbiuki (Maara), Julius Melly (Tinderet), George Kariuki (Ndia) na Sabina Chege ni miongoni mwa wabunge 186 wa Bunge la Kitaifa waliokosa kuhudhuria kikao muhimu kilichopitisha Mswada wa Fedha wa 2026.

Wakati hoja ya kusomwa kwa mara ya tatu na kupitishwa kwa mswada huo ilipowasilishwa bungeni, wabunge 162 kati ya 349 walikuwepo.

Hii ilikuwa hatua ya mwisho kabla ya mswada huo kuwasilishwa kwa Rais kutiwa saini kuwa sheria.

Katika kura hiyo iliyopigwa saa tatu na dakika 15 usiku Alhamisi, wabunge 122 waliunga mkono mswada huo huku 40 wakipinga.

Hakukuwa na waliokataa kupiga kura.Mswada huo unalenga kuongeza mapato ya ziada ya takriban Sh120 bilioni ili kufadhili bajeti ya Sh4.82 trilioni kwa mwaka wa kifedha 2026/27.

Hata hivyo, baada ya shinikizo kutoka kwa wananchi na wadau, Kamati ya Fedha na Mipango ilipendekeza marekebisho yaliyopunguza makadirio ya mapato hadi chini ya Sh70 bilioni.

Licha ya umuhimu wa mswada huo, baadhi ya wabunge hawakuhudhuria. Bw Nyoro alieleza kuwa alikuwa nje ya nchi wakati wa upigaji kura.

“Nimekuwa nje ya nchi tangu Jumatano jioni, ndiyo maana sikuwa bungeni,” alisema Bw Nyoro, akisisitiza kuwa alishiriki mijadala ya awali ya mswada huo.

Aliongeza: “Tumekuwa tukihudhuria na kutoa maoni yetu katika kamati na bungeni kwa lengo la kutoa mtazamo mbadala kuhusu uchumi.”

Wabunge wengine walioorodheshwa kuwa hawakuhudhuria ni pamoja na Didmus Barasa (Kimilili), Mary Wamaua (Maragwa), Innocent Mugabe (Likuyani), Alice Ng’ang’a (Thika Town), Doris Donya (Mbunge wa Kike Kisii) na John Njuguna maarufu Kawanjiku (Kiambaa).

Ingawa Katiba inahitaji angalau wabunge 50 ili kufanikisha shughuli za Bunge la Kitaifa, viongozi wa Bunge wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa uwepo wa wabunge hasa wakati wa maamuzi muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja.

Bw Mbiuki ni mwenyekiti wa Kamati ya Utalii, huku Bw Melly akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Elimu. Mabw Kariuki na Barasa ni viongozi katika Kamati ya Uchukuzi na Miundombinu.

Hata hivyo, imebainika kuwa baadhi ya wenyekiti wa kamati hawahudhurii mara kwa mara vikao vya Bunge, hali inayosababisha changamoto katika majukumu yao ya uongozi.

Kazi zao mara nyingi zimekuwa zikifanywa na wanachama wengine wa kamati zao.Kabla ya kura hiyo, Spika Moses Wetang’ula alionekana kukerwa na kutokuwepo kwa baadhi ya wenyekiti wa kamati waliopaswa kutoa majibu kwa hoja za wabunge, hali iliyomlazimu Mbunge wa Bureti, Kibet Komingoi kuingilia kati mara kadhaa.

Kiongozi wa Wachache, Junet Mohammed (Suna East), alisema baadhi ya viongozi wa kamati “hawafiki bungeni mara kwa mara,” akipendekeza hata marekebisho ya uongozi wa kamati hizo.

Baadhi ya wabunge waliokosa kupiga kura hawakupatikana kujibu maswali ya waandishi wa habari, huku wengine wakihusishwa na malengo ya kisiasa ya kugombea nyadhifa za ugavana katika uchaguzi wa 2027, hali inayowafanya kuwa na muda mdogo bungeni.

Mswada huo ulikuwa na mjadala mkali, baadhi ya wabunge wakipinga kile walichokiita mzigo wa ushuru kwa wananchi, huku wengine wakiuunga mkono kwa hoja kuwa unahitajika kufadhili bajeti ya taifa.Licha ya upinzani, mswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Rais William Ruto ili kuwa sheria rasmi.

 



from Taifa Leo https://ift.tt/HAlqRym
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post