Matumaini tele baada ya maambukizi mapya ya HIV Kenya kushuka kwa asilimia 56

KENYA imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya virusi vya Ukimwi baada ya maambukizi mapya kushuka kwa asilimia 56 katika kipindi cha miaka sita iliyopita, kulingana na takwimu mpya za baraza la kitaifa la kudhibiti ugonjwa huo.

Ripoti ya tathmini ya pamoja ya mpango wa kupiga vita Ukimwi inaonyesha kuwa maambukizi mapya yalipungua kutoka visa 32,027 mwaka 2020, hadi visa 13,936 mwaka 2026.

Kwa sasa, watu 1,481,853 wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini, huku takriban milioni 1.4 wakipokea dawa za kupunguza makali ya virusi (ARV).

Vifo vinavyohusishwa na Ukimwi pia vimepungua kutoka 21,007 mwaka 2024 hadi 19,434 mwaka 2026.

Kiwango cha maambukizi kitaifa ni asilimia 3.22, ingawa ugonjwa huo bado umejikita zaidi katika baadhi ya kaunti.

Ripoti inaonyesha kuwa wanawake na vijana wanaendelea kuathirika zaidi.

Asilimia 41 ya maambukizi mapya kwa watu wazima yalirekodiwa miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24, wengi wao wakiwa vijana wa kike.

Kaunti 10 zinabeba mzigo mkubwa wa maambukizi nchini, zikijumuisha Nairobi, Homa Bay, Kisumu, Siaya, Migori, Busia, Kakamega, Mombasa, Kiambu na Nakuru.

Takwimu zinaonyesha kuwa kundi la vijana na wanaobalehe lilishuhudia upungufu mkubwa zaidi wa maambukizi kwa asilimia 61.5 kati ya mwaka 2021 na 2026.

Hata hivyo, watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 14 walirekodi upungufu mdogo zaidi wa asilimia 34.7.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 38 ya maambukizi kwa watoto yanatokana na mapungufu katika huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto.

Pia, kiwango cha vifo vinavyohusiana na Ukimwi kilikuwa juu zaidi miongoni mwa watoto, ambapo watoto 33 kati ya kila 1,000 walifariki ikilinganishwa na watu wazima 12 kwa kila 1,000.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kukabiliana na Ukimwi na magonjwa yanayohusiana nao, Douglas Bosire, alisema takwimu hizo zinaonyesha mafanikio makubwa lakini pia changamoto zinazohitaji kushughulikiwa haraka.

“Nairobi iliongoza kwa maambukizi mapya 1,516, ikifuatiwa na Kisumu 1,057, Homa Bay 985 na Migori 970. Takwimu hizi zinaonyesha mafanikio lakini pia dharura ya kuchukua hatua zaidi,” alisema.

Sekta hiyo pia imekumbwa na changamoto za ufadhili baada ya kusitishwa kwa msaada wa Pepfar na USAid mwaka 2025, hatua iliyotatiza huduma katika vituo 2,127 vya afya.

Waziri wa Afya, Bw Aden Duale, alisema kuunganishwa kwa huduma za HIV, kifua kikuu na malaria hakumaanishi kupuuzwa kwa mapambano dhidi ya HIV, huku magavana wakitaka serikali kuhakikisha mpango huo unafadhiliwa kikamilifu.



from Taifa Leo https://ift.tt/3W84U5i
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post