
RAIS William Ruto kwa mara ya pili ndani ya wiki moja amewataka vijana kuheshimu sheria, huku familia za waathiriwa wa maandamano ya Juni 25, 2024 zikiandaa maadhimisho ya miaka miwili wiki hii.
Kiongozi wa nchi alisema vijana wana uhuru wa kujieleza ila pia wanastahili kuheshimu sheria na kujizuia kuharibu mali ya watu wanapoandamana.
“Tuko katika taifa huru, mko huru kuzungumza na kufanya chochote ila lazima vitendo viandamane na majukumu na wajibu. Uhuru bila uwajibikaji haufai,” akasema Rais.
Alikuwa akizungumza wakati wa gwaride na ukaguzi wa 95 wa Shirika la St John Ambulance uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi.
Rais alisema kuwa nchi imekuwa ikiomboleza vifo vya vijana katika maeneo ambayo yalipaswa kuwa salama zaidi kwa watoto, akiwataka vijana kujifunza na kuweka maslahi ya taifa mbele.
Kauli ya Rais inakuja siku chache kabla ya taifa kuadhimisha mwaka wa pili tangu maandamano ya Juni 25, 2024 dhidi ya Mswada wa Fedha. Maandamano hayo yaligeuka kuwa ya vurugu na kusababisha vifo na majeraha ya watu wengi.
Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu Kenya (KNCHR), watu 60 waliuawa kati ya Juni 18 na Julai 16, 2024 wakati wa maandamano hayo. Wengine wengi walijeruhiwa japo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamedai kuwa idadi halisi ya waliofariki huenda ilikuwa kubwa zaidi.
from Taifa Leo https://ift.tt/QTlMb7P
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS