
MBUNGE wa Saboti, Caleb Amisi amedai ametengwa ndani ya Chama cha ODM, akifichua kuwa aliondolewa kwenye kundi la WhatsApp la chama na sasa hapati taarifa kuhusu shughuli wala mikutano yake.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumatano, Juni 10, 2026, Amisi alisema amewekwa gizani kuhusu masuala ya chama baada ya kuondolewa kwenye jukwaa hilo la mawasiliano na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed.
“Sijui kinachoendelea. Walitufungia mlango. Mimi hata sipo kwenye kundi la WhatsApp la wanachama wa ODM,” alisema.
Anadai ndiye mwanachama pekee aliyeondolewa kwenye kundi hilo huku viongozi wengine wa ODM akiwemo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wakiendelea kuwa wanachama wa kundi hilo.
Alipoulizwa kwa nini anaamini alilengwa peke yake, Amisi alitania akisema huenda ni kwa sababu alikuwa “anapiga kelele nyingi” na kusababisha misukosuko ndani ya chama.
Mbunge huyo alisema sasa hafahamishwi kuhusu mikutano wala maamuzi ya chama licha ya kuendelea kuchangia fedha kila mwezi kupitia makato ya mshahara wake.
“Nimewekwa gizani. Sijui wanakutana lini, lakini kila mwezi nakatwa Sh20,000 kutoka kwa mshahara wangu ada ya chama,” alisema.
Aliongeza kuwa fedha hizo hufadhili shughuli mbalimbali za ODM, ikiwemo mikutano ya hadhara inayofanyika sehemu tofauti nchini.
Awali, Amisi alishutumu ODM kwa kumuondoa kama Naibu Katibu wa Uratibu kupitia ujumbe wa WhatsApp, hatua aliyoitaja kuwa “mapinduzi” ndani ya chama.
from Taifa Leo https://ift.tt/Hhdmn3z
via
IFTTT