
TAKRIBAN wiki tatu sasa tangu Rais William Ruto akutane na viongozi wa sekta ya uchukuzi katika Ikulu ya Mombasa, wamiliki wa matatu bado wanasubiri kuona ikiwa ahadi alizotoa zitatekelezwa au zitabaki kuwa maneno matupu. Hali hii imezua hofu ya kurejea kwa migomo na misukosuko ambayo ilisimamishwa baada ya serikali kuahidi kutoa nafuu kwa sekta hiyo.
Kiini cha matarajio yao ni ahadi ya kupunguza bei ya dizeli kwa angalau Sh10 kwa lita katika mzunguko wa bei wa Juni na Julai. Wamiliki wa matatu wanasema hatua hiyo ndiyo iliyowafanya waahirishe mgomo waliokuwa wamepanga, wakiamini kuwa serikali ilikuwa imejitolea kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji.
Sasa macho yote yameelekezwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA), inayotarajiwa kutangaza bei mpya za mafuta leo. Ikiwa ahadi hiyo haitatekelezwa, viongozi wa sekta hiyo wanaonya kuwa huenda hasira zilizokuwa zimetulia zikachipuka tena.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Albert Karakacha, amesema wanachosubiri kwa sasa ni kuona bei ya dizeli ikishuka kama walivyoahidiwa, huku masuala mengine yakisubiri mazungumzo ya baadaye.
Lakini changamoto za sekta hiyo haziishii kwenye mafuta pekee. Wamiliki wa matatu pia wanataka suluhu kuhusu ada kubwa za bima, mikopo ya magari na gharama nyingine za uendeshaji zinazozidi kupunguza faida zao. Rais Ruto aliagiza Wizara ya Uchukuzi na taasisi husika kuzungumza na benki ili kutafuta nafuu kwa wamiliki wa matatu wanaohangaika kulipa mikopo ya magari, lakini hadi sasa hakuna taarifa za wazi kuhusu maendeleo hayo.
Imebainika kuwa kamati inayojumuisha wawakilishi wa sekta ya matatu, taasisi za kifedha na maafisa wa wizara tayari imeundwa kujadili suluhu hizo. Hata hivyo, ukosefu wa ratiba na maelezo ya utekelezaji umeacha waendeshaji wengi wakiwa na mashaka.
Serikali pia iliahidi kuendelea kutumia Hazina ya Maendeleo ya Petroli pamoja kuwalinda wananchi dhidi ya kupanda kwa bei za mafuta duniani. Hata hivyo, wamiliki wa matatu wanasema kipimo halisi cha nia njema ya serikali ni kupunguzwa kwa bei ya dizeli.
Rais pia alielekeza Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) kuruhusu matatu kuendelea kuwa na michoro na mapambo ya kisanii mradi viwango vya usalama vizingatiwe.
Hata hivyo, dalili za kutoridhika tayari zimeanza kujitokeza. Mwenyekiti wa Forward Travellers Sacco, Paul Thiong’o, amesema baadhi ya viongozi waliowawakilisha kwenye mazungumzo walinufaisha nafsi zao badala ya kutetea maslahi ya sekta nzima. Aidha, alieleza kuwa suala la kuruhusu vioo vya giza si kipaumbele na linaweza hata kuhatarisha usalama barabarani.
Kwa upande wake, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi amesisitiza kuwa serikali imejizatiti kutekeleza agizo la Rais la kupunguza bei ya dizeli. Amesema mafuta hayo ni muhimu kwa sekta za usafiri, kilimo na viwanda na hivyo bei ikiwa ya chini itasaidia kupunguza gharama za maisha na uzalishaji.
Wandayi pia amehakikishia wananchi kuwa Kenya ina akiba ya kutosha ya mafuta hadi mwisho wa Julai na hakuna hatari ya upungufu wa bidhaa hiyo licha ya kuyumba kwa soko la kimataifa.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa sekta hiyo kama Wilfred Bosire wa Mass Mobility Operators Association wanaamini punguzo la zaidi ya Sh10 linawezekana, wakisema hali ya upatikanaji wa mafuta nchini haijatikiswa na misukosuko ya kimataifa.
from Taifa Leo https://ift.tt/w4925gV
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS