
KUONEKANA kwa Gavana wa Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, katika mkutano wa umma wa vuguvugu la Linda Mwananchi mjini Thika siku ya Jumapili kumefanya aanze kumulikwa kisiasa.
Eneo la Mlima Kenya limeshuhudia mabadiliko makubwa kisiasa kuelekea 2027 na hatua ya Bw Kang’ata imezua maoni mseto.
Karata ya Bw Kang’ata inaonyesha wazi jinsi viongozi wa Mlima Kenya wanaendelea kusaka faraja, baada ya wengi wao kutalikiana na serikali.
Jana Gavana Kang’ata alizungumza na wapigakura wa Mlima Kenya katika mahojiano kwenye runinga ya Inooro, ambapo alifafanua kuwa hatua yake ya kuhudhuria mkutano wa hadhara wa Linda Mwananchi katika Kaunti ya Kiambu kulikuwa sehemu ya mikakati yake ya kisiasa.
“Licha ya kujiunga na Linda Mwananch nafahamu kwamba DCP ni chama maarufu zaidi katika Kaunti ya Murang’a na kwamba Rigathi Gachagua ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya,” akasema Bw Kang’ata.
Alikanusha madai kuwa anajiandaa kuwa kigogo wa siasa za Mlima Kenya, kugombea urais au nafasi ya naibu rais, ama kuanzisha chama.
Hata hivyo, mdadisi wa masuala ya kisiasa Stanley Wang’ombe alimshutumu Bw Kang’ata kwa kujaribu kuchukua hatua binafsi kuamua mwelekeo wa kisiasa wa Mlima Kenya kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Tungependa kushirikiana na watu wengi iwezekanavyo. Lakini Dkt Kang’ata anapaswa kujua kwamba tutafanya hivyo kwa mpangilio maalumu. Hapasi kutangulia,” akaeleza Bw Wang’ombe.
Gavana Kang’ata akitetea uamuzi wa kuingia Linda Mwananchi alisema lengo lilikuwa kuwakilisha maslahi ya Mlima Kenya.
Alisisitiza eneo hilo halipaswi kuachwa nje katika uwakilishi ndani ya vuguvugu hilo.
Pia alisisitiza kwamba hatua yake haipaswi kutafsiriwa kama kujiunga na ODM — ikizingatiwa kundi hilo ni mrengo wa waasi katika ODM.
Badala yake alisema vigogo wa vuguvugu hilo ambao pia ni wanachungwa; Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, huenda wakajiunga na muungano mpya wa kisiasa hivi karibuni.
Kauli za gavana huyo pia zimeongeza shinikizo kwa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, ambaye amekuwa mkosoaji wa serikali ila bado hajatangaza hadharani msimamo wake wa kisiasa kuelekea kura ya 2027.
Bw Kang’ata amejipata katika hali ngumu ya kisiasa miezi michache iliyopita baada ya kuasi serikali na pia kukosa kujitambulisha na mrengo wa Bw Gachagua.
Waziri wa Ardhi Alice Wahome amekuwa akifanya ziara Murang’a akimkosoa gavana huyo kwa kuhama mrengo wa serikali.
“Ni vyema ameondoka kujiunga na mirengo ya upinzani, lakini atajuta na atajua yeye si mbabe wa siasa za kaunti hii,” akahoji Bi Wahome.
Gavana Kang’ata alijibu kwa kumshutumu Waziri Wahome kwa kuweka mbele maslahi ya chama kuliko huduma kwa wananchi.
from Taifa Leo https://ift.tt/o9VtexR
via IFTTT