
KWA maelfu ya vijana nchini, ndoto ya kujiunga na vyuo vikuu au taasisi za kiufundi hukwama kutokana na ukosefu wa karo.
Wengi hulazimika kuahirisha masomo, huku wengine wakichukua mikopo ambayo huanza kuwalemea hata kabla ya kupata ajira.
Ili kutatua hili, Global ISA Alliance, muungano wa mashirika kutoka nchi 24 duniani, umezindua mfumo wa ufadhili wa elimu unaozingatia matokeo ya wanafunzi.
Mfumo huo wa Income Share Agreements (ISAs) unatofautiana na mikopo ya kawaida ya masomo kwa kuwa mwanafunzi halipi 'deni' mapema.
Badala yake, huanza kuchangia sehemu ndogo ya mapato yake baada ya kupata kazi. Hakuna riba wala kushurutishwa kufanya malipo ikiwa mwanafunzi hajaajiriwa.
Hatua hii inakuja wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto ya maelfu ya wahitimu wanaoingia sokoni kila mwaka huku nafasi za ajira zikiwa chache.
Wataalamu wanasema hali hiyo imezua maswali kuhusu thamani ya elimu na namna ya kuhakikisha mafunzo yanawapa vijana ujuzi unaohitajika na waajiri.
Mkurugenzi Mkuu wa Chancen Kenya, Gladys Mutisya, alisema vijana wengi wenye uwezo wa kusoma hukosa nafasi kwa sababu ya gharama za elimu.
“Tunashuhudia vijana wengi wenye vipaji wakikosa nafasi za kubadilisha maisha yao kwa sababu hawawezi kumudu gharama za masomo. Mfumo huu unalenga kuwaondolea kikwazo hicho,” alisema.
Kwa mujibu wa Chancen International, zaidi ya vijana 10,000 nchini Kenya, Rwanda, Ghana na Afrika Kusini wamefadhiliwa kupitia mfumo huo.
Takribani asilimia 73 ya wahitimu hupata ajira ndani ya mwaka mmoja baada ya kukamilisha masomo yao.
from Taifa Leo https://ift.tt/Pefdkp7
via
IFTTT