Ol Kalou: Gachagua ashutumu IEBC akisema imeshindwa kuzima serikali kuwahonga wapigakura

KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Bw Rigathi Gachagua, ameshambulia vikali Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiishutumu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba.
Bw Gachagua alidai kuwa tume hiyo inafumbia macho madai ya kuhonga wapigakura, vitisho vya kisiasa na maafisa wa serikali kuingilia uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou utakaofanyika Julai 16.
Akizungumza jana, siku moja kabla ya makamishna wa IEBC kutimiza mwaka mmoja afisini, Bw Gachagua alisema jinsi tume hiyo itakavyosimamia uchaguzi wa Ol Kalou, itakuwa kipimo cha iwapo inaweza kuaminiwa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Alitoa kauli hiyo chini ya saa 24 baada ya Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Edung Ethekon, kuonya kuwa tume inaweza kuahirisha au hata kufuta uchaguzi huo iwapo vitendo vya utoaji hongo, vurugu na makosa mengine ya uchaguzi vitaathiri uadilifu wa mchakato huo.
Hata hivyo, Bw Gachagua alisema badala ya kuonya kuhusu uwezekano wa kuahirisha uchaguzi, IEBC inapaswa kuwachukulia hatua wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivyo.
"Mwenyekiti wa IEBC anawezaje kutishia kufuta uchaguzi kwa sababu ya hongo ilhali Katiba na sheria zinampa mamlaka ya kukomesha vitendo hivyo?" alihoji.
Alidai kuwa vyombo vya habari vimeripoti visa vya utoaji hongo kila siku, huku mawaziri, makatibu na maafisa wengine wa serikali wakihusika waziwazi katika kampeni na kuwahonga wapigakura.
"Badala ya kuwachukulia hatua wanaohusika, IEBC inataka kuwaadhibu wananchi wa Ol Kalou kwa kufuta uchaguzi wao," alisema.
Bw Gachagua alinukuu Kifungu cha 81 cha Katiba kinachotaka uchaguzi uwe huru, wa haki na usio na vurugu, vitisho, ufisadi au ushawishi usiofaa. Pia, alirejelea Kifungu cha 38 kinachowapa Wakenya haki ya kushiriki katika uchaguzi wa mara kwa mara ulio huru na wa kuaminika.
Alisema tume hiyo imeshindwa kutekeleza masharti hayo ya kikatiba na hivyo kupoteza imani ya wananchi.
"Tumekuwa tukieleza kutoridhishwa kwetu na jinsi tume hii inavyofanya kazi. Katiba na imani ya wananchi ndiyo misingi ya uchaguzi wowote, na imani hiyo imeporomoka," alisema.
Pia, aliishutumu IEBC kwa kutumia viwango tofauti katika chaguzi dogo tofauti. Alidai tume hiyo haikuchukua hatua katika chaguzi za Mbeere North, Malava, Narok Township na Kasipul, ambako kuliripotiwa vurugu na madai ya hongo, lakini sasa imekuwa ikitoa matamshi makali kuhusu Ol Kalou.
"Kulikuwa na vurugu, vitisho na hata mauaji katika chaguzi zilizopita, lakini IEBC haikuwahi kuzungumzia kuahirisha uchaguzi. Kwa nini Ol Kalou iwe tofauti?" alihoji.
Bw Gachagua alidai eneo la Ol Kalou limekuwa tulivu isipokuwa visa vichache alivyodai vilihusisha maafisa wa serikali. Alirejelea tukio la Julai 1 katika Hoteli ya Royal Garden ambapo viongozi wa DCP walidai kushambuliwa na polisi pamoja na wafuasi wa chama cha UDA.
Aidha, aliwataka maafisa wa polisi waliovalia sare pekee kusimamia usalama siku ya uchaguzi, akidai maafisa waliovalia mavazi ya kiraia wamekuwa wakitumika kutisha wapigakura katika chaguzi zilizopita.
Alikosoa serikali kwa kile alichodai ni kupeleka idadi kubwa isiyo ya kawaida ya mawaziri, makatibu na wakuu wa mashirika ya umma kufanyia kampeni mgombeaji wa UDA.
Alitaja Waziri wa Ardhi Alice Wahome, Waziri wa ICT William Kabogo, Waziri wa Barabara Davis Chirchir, Waziri wa Utalii Rebecca Miano, Katibu wa Ulinzi Patrick Mariru, Katibu wa Nishati Alex Wachira na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Kenya Philip Mainga.
Kwa mujibu wake, viongozi hao wamekuwa wakizindua miradi ya maendeleo huku wakigawa fedha taslimu, godoro, mitungi ya gesi, matangi ya maji na bidhaa nyingine ili kuwashawishi wapigakura.
 "Ni kama miujiza kwamba miradi yote ya maendeleo ya serikali imehamia katika eneo moja wakati wa kampeni," alisema.
Alionya kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi wa Ol Kalou kutadhoofisha zaidi uaminifu wa IEBC na kuzua maswali kuhusu uwezo wake wa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.
 "Iwapo IEBC haiwezi kusimamia uchaguzi mmoja mdogo wa ubunge kwa sababu ya madai ya hongo na vurugu, itawezaje kuaminika kusimamia Uchaguzi Mkuu?" alihoji.


from Taifa Leo https://ift.tt/ARKjvUe
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post