
RAIS William Ruto Ijumaa alizindua rasmi awamu ya pili ya mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara vijana (NYOTA), katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mawaziri na maafisa wengine wakuu.
Hatua hiyo ilionyesha mkakati mpya wa serikali wa kutumia mawaziri kufikisha sera na mipango yake moja kwa moja kwa wananchi huku ikipanua utekelezaji wa mpango huo wa kuwawezesha vijana.
Rais Ruto aliongoza uzinduzi katika Uwanja wa Michezo wa Ulinzi jijini Nairobi, huku Naibu Rais Kithure Kindiki akiongoza shughuli za kaunti za Nakuru, Baringo na Nyandarua mjini Nakuru.
Mkuu wa Mawaziri Waziri, Musalia Mudavadi aliongoza uzinduzi eneo la Magharibi uliohusisha Kakamega, Vihiga, Busia na Bungoma katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.
Naye Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, aliongoza uzinduzi Meru, Embu na Tharaka Nithi mjini Chuka, huku Waziri wa Ardhi, Alice Wahome, akiongoza shughuli za kaunti za Nyeri, Kirinyaga na Murang'a.
Waziri wa Kazi, Alfred Mutua alisimamia uzinduzi Machakos, Makueni na Kitui mjini Kitui.
Shughuli kama hizo zilifanyika pia Nanyuki, Kapenguria, Eldoret, Bomet, Malindi, Mombasa, Kisumu, Kisii pamoja na Mandera, Wajir, Garissa na Marsabit.
Ingawa alikuwa Nairobi, Rais Ruto alihutubia taifa kupitia matangazo ya moja kwa moja yaliyotangazwa katika vituo vyote vya uzinduzi, jambo lililoruhusu mawaziri na viongozi wengine kuwasilisha ujumbe mmoja wa kitaifa kwa wakati mmoja.
Mpango huo unaolenga kuwawezesha vijana unatoa mtaji wa kuanzisha biashara, mafunzo ya ujasiriamali pamoja na ushauri wa kitaalamu ili kuwasaidia vijana kuanzisha na kukuza biashara zinazoweza kuzalisha ajira.
Zaidi ya vijana 14,000 kutoka Nairobi, Kiambu na Kajiado walihudhuria uzinduzi huo jijini Nairobi, huku uzinduzi wa wakati mmoja ukiwawezesha vijana kutoka kaunti zote 47 kushiriki bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Serikali ilitenga Sh5.5 bilioni kufadhili vijana 110,000 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 29 katika awamu ya kwanza ya mpango huo.
Kwa jumla, NYOTA inatarajiwa kuwafikia takriban vijana 820,000 kupitia ufadhili wa biashara, ukuzaji wa ujuzi na fursa za ajira.
“Tunataka kuhakikisha hakuna Mkenya anayeachwa nyuma. Zamani baadhi ya maeneo na wananchi walibaki nyuma, lakini sasa tumedhamiria kila Mkenya ajivunie nchi yake. Ndiyo maana mpango huu unatekelezwa katika wadi zote 1,450 nchini,” alisema Rais Ruto.
Alisema mpango huo umeundwa ili kuwapa vijana nafasi ya kushiriki katika ukuaji wa uchumi bila kujali kiwango cha elimu, hali ya kijamii au mwelekeo wao wa kisiasa.
“Nataka kuwaambia vijana kuwa huu ni mpango wa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 29. Umeundwa kwa ajili ya vijana wa Kenya,” alisema.
Rais alisema walengwa wakuu ni vijana ambao kwa muda mrefu wamekosa mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokana na ukosefu wa dhamana, mtaji au mitandao ya kibiashara.
Alisisitiza kuwa uteuzi wa wanufaika utaongozwa na uwazi na uwajibikaji, wala si upendeleo wa kisiasa.
"Hauhitaji kuwa gavana, chifu au mtu maarufu ili kufaidika. Mpango huu ni wa uwazi na uwajibikaji, na hautaendeshwa kwa misingi ya upendeleo," alisema.
Aliwataka wanufaika kuripoti mtu yeyote atakayewaitisha fedha au kuwaelekeza kuunga mkono chama fulani cha kisiasa ili wapate nafasi katika mpango huo.
"Huu si mpango wa kisiasa. Ni mpango wa biashara unaolenga kuwawezesha vijana," alisisitiza.
Rais pia alisema hata vijana ambao hawakumaliza masomo ya sekondari au waliosoma hadi darasa la nane watapewa nafasi sawa.
"Vijana wote ni Wakenya na serikali yetu ina wajibu wa kuwajali," alisema.
Mbali na mtaji, wanufaika watapatiwa mafunzo ya biashara, ushauri na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha biashara zao zinakuwa endelevu.
Hatutawapa fedha pekee. Tutawafunza, tutawashauri na tutatembea nanyi hadi mfanikiwe," alisema Rais.
Kwa baadhi ya wanufaika, mpango huo tayari umeanza kubadili maisha yao.
Kaunti ya Bungoma, Musembe alitumia fedha hizo kufungua duka la vifaa vya kielektroniki baada ya miaka mingi ya kukosa mtaji wa kununua bidhaa.
Katika Kakamega, Sonya Wembo aliwekeza fedha hizo katika ufugaji wa kuku, akisema sasa ana nafasi ya kujenga biashara itakayomwezesha kujitegemea.
Huko Kitui, Masoso Kituti alifungua bucha na anasema mtaji huo umempa fursa ya kujenga chanzo cha kudumu cha mapato.
Garissa, Najma alipanua biashara yake kwa kuongeza bidhaa dukani, huku Kiprono wa Eldoret akiwekeza katika kilimo cha parachichi akisema ni uwekezaji wa muda mrefu utakaomletea kipato cha baadaye.
Mbali na uzinduzi wa NYOTA, shughuli za Ijumaa zilionyesha jinsi serikali ya Kenya Kwanza inavyozidi kutumia mawaziri kueneza sera zake kote nchini kwa wakati mmoja badala ya kutegemea ziara za Rais pekee.
from Taifa Leo https://ift.tt/R3NAD61
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS