
VIONGOZI na wakazi wa Kaunti ya Lamu, wameeleza matarajio makubwa ya ukuaji wa kiuchumi kutokana na uamuzi wa mfanyabiashara mashuhuri kutoka Nigeria, Bw Aliko Dangote, kutaka kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi eneo hilo.
Jana, Rais William Ruto alimkabidhi Naibu Rais Kithure Kindiki jukumu la kuongoza kikosi cha serikali na sekta ya kibinafsi kitakachoratibu maandalizi ya uwekezaji katika kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta kitakachojengwa Kaunti ya Lamu.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi wakati wa kutia saini Sheria ya Hazina ya Utajiri wa Taifa 2026, Rais Ruto alisema serikali tayari imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo na tarehe ya uwekaji wa jiwe la msingi imepangwa.
"Tumepanga tarehe ya kuweka jiwe la msingi la mradi huu. Tunachukua hatua zitakazoifanya Kenya kuwa taifa la kiwango cha dunia ya kwanza," alisema Rais Ruto.
Hata hivyo, hakufichua tarehe rasmi ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda hicho.
Kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa, kiwanda hicho kitakachokuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki kitakuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku.
Kitasambaza bidhaa za petroli Kenya na kwa nchi jirani, hivyo kupunguza gharama za kununua bidha hiyo kutoka mataifa ya nje.
Kampuni ya Dangote Group awali mwaka huu ilikuwa imeonesha nia ya kuwekeza mradi huo Tanga, Tanzania kabla ya kubadili nia kutokana na uwezo mkubwa zaidi wa Kenya.
Ingawa eneo halisi ambako kiwanda hicho kitajengwa halijafahamika, wadau serikalini walidokeza kuwa huenda kikajengwa katika eneo la Magogoni, karibu na Bandari ya Lamu iliyo Kililana, Lamu Magharibi.
Bandari ya Lamu husifiwa kwa uwezo wake wa kupokea meli kubwa na matumizi ya teknolojia za kisasa, kuliko ilivyo Mombasa na bandari nyingine za nchi Jirani.
Naibu Gavana wa Lamu, Dkt Mbarak Salim, amesifu hatua hiyo na kusema serikali ya kaunti, viongozi na wakazi wako tayari kushirikiana na mwekezaji huyo kuhakikisha mradi utafaulu.
“Tutashirikiana kuzingatia masuala muhimu ya usalama wa mazingira, uchumi na kuinua watu wetu kwa nafasi zozote za uwekezaji zitakazoundwa kupitia mradi huo,” akasema Dkt Salim.
Meneja Mkuu wa Bandari ya Lamu, Bw Abdulaziz Mzee, alisema mpango huo ukifanikiwa, utapanua biashara bandarini Lamu.
“Twapokea mradi kwa mikono miwili. Utaongeza idadi ya meli zitakazotia nanga bandarini Lamu kufikisha, kushukisha na kupakia mapipa ya mafuta, hivyo kuinua mapato na biashara ya bandarini,” akasema BwMzee.
Wakazi wa Lamu pia walipokea vyema mpango huo, lakini walisisitiza haja ya mwekezaji kuwashirikisha kikamilifu.
Mbunge wa zamani wa Lamu Mashariki, Bw Mohamed Hashim, alisema wasingependa yale yaliyofanyika wakati bandari ya Lamu ilipoletwa yajirudie, ikizingatiwa kesi zilizowasilishwa mahakamani kuhusu haki za kijamii.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Meya wa zamani wa Manispaa ya Lamu, Bw Famau Ahmed aliyependekeza asilimia 70 ya ajira kwenye mradi huo endapo utatekelezwa ielekezewe vijana wenyeji wa Lamu.
“Hatutaki kulaza damu tena kama ilivyofanyika katika LAPSSET kisha jamii ikose sauti kwenye mradi,” akasema Bw Ahmed.
Mwanaharakati wa Mazingira na Afisa Mtendaji wa Muungano wa Lamu Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau, aliomba wote ambao ardhi zao zitatumiwa wafidiwe kikamilifu.
“Mradi ni wa maana. Ila lazima kuwepo na mikakati kabambe ya kuwafidia waathiriwa wote. Haki za kimazingira, kijamii na tamaduni zetu kama wakazi wa Lamu pia zisikiukwe wakati mradi unapotekelezwa,” akasema Bi Famau.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Abdulkdir alisisitiza haja ya mwekezaji kuzingatia utoaji huduma za jamii wakati mradi ukiendelezwa.
from Taifa Leo https://ift.tt/z5EqcWs
via IFTTT