Mgogoro: Ajabu wakifariki saa 3 baada kuoana

WALIANZA maisha yao ya ndoa saa 10 jioni Agosti 9, 2026, lakini kufikia saa moja na nusu usiku siku hiyo wote walikuwa wamefariki.
Patrick Mwangi, 28, na Jackline Wambui, 25, walikuwa wameanza maisha yao ya ndoa katika Kijiji cha Nyerere, Murang’a, lakini ikawa ndoa ya muda mfupi zaidi kuwahi kushuhudiwa na baadhi ya wakazi.
Polisi wanachunguza vifo hivyo, ambavyo mwanzoni vilionekana kuwa mauaji yaliyotekelezwa na mmoja wao kisha akajiua.
Inadaiwa Mwangi alimnyonga Wambui kwa kamba alipokuwa amelala, kabla ya kutoka nje ya nyumba iliyokuwa imekusudiwa kuwa makazi yao mapya na kujinyonga.
Wapenzi hao walikuwa wamechumbiana kwa takriban miaka mitatu, kipindi kilichojaa migogoro kiasi kwamba wazazi wao walilazimika kuingilia kati mara kadhaa kuwapatanisha.
Mwangi alikuwa mwendesha bodaboda, huku Wambui akifanya kazi za vibarua mara kwa mara.
Mama ya Mwangi, Bilha Wangare, alisema bado hawezi kuelewa uhusiano wa wawili hao.
“Ulikuwa upendo ulioonekana kama uchawi. Wote walikuwa na mapenzi makali ambayo ilikuwa vigumu kuelewa. Nilishiriki katika mikutano mingi ya kuwapatanisha ili wasameheane. Nadhani neno linalowafaa ni wapenzi wapumbavu,” alisema.
Kwa mujibu wake, waligombana kwa sababu ya mambo mbalimbali, ikiwemo simu, pesa na burudani.
Wambui aliwahi kulalamika kwamba Mwangi hakumpeleka kujivinjari mara kwa mara kama alivyotaka. Mwangi naye alimshutumu kwa kuiba Sh100,000 kutoka kwake.
Wambui pia alilalamika kwamba Mwangi alikuwa akiwasaidia wazazi wake kifedha kupita kiasi, akitaka familia yake ipewe kipaumbele.
Mwaka huu, alianza kumtaka Mwangi amkabidhi cheti cha umiliki cha pikipiki yake na hati miliki ya shamba la ekari 0.1 alilonunua Makuyu, Maragua.
Wakati huo hawakuwa wakiishi pamoja, lakini mara kwa mara Wambui angelala katika nyumba ndogo ya Mwangi.
Katika juhudi za kuwapatanisha, Bi Wangare aliwaita kwenye kikao Agosti 4 na kupendekeza waanze kuishi pamoja.
Mwangi alitaka Wambui kwanza azae mtoto wake, huku Wambui akitaka cheti cha pikipiki na hati ya kumiliki shamba.
Hatimaye walikubaliana kwamba Mwangi angemfungulia biashara katika soko la Irembu, naye akakubali kwamba angepata mimba haraka iwezekanavyo.
Baada ya Wambui kuondoka, Mwangi alimkabidhi mama yake hati hizo akisema hamwamini.
Mnamo Agosti 6, Wambui alimpigia simu Bi Wangare na kumwambia alikuwa ameamua kuolewa na Mwangi na angehamia kwake Agosti 9.
Saa 10 jioni siku hiyo, Wambui alifika na kumkuta Mwangi akimsubiri.
Baada ya muda mfupi, Mwangi alimbeba kwa kwenye pikipiki na wakaondoka.
Walirejea karibu saa moja jioni. Bi Wangare alisema Wambui alionekana mchovu, mwenye usingizi na kama aliyelewa.
Muda mfupi baadaye, Mwangi aliingia nyumbani kwa wazazi wake na kuzungumza nao.
Alisalimia kila mmoja na kuwaaga.
Kabla ya kuondoka, alimwambia mama yake kwamba Wambui alikuwa ameweka picha ya mwanaume mwingine kwenye mitandao ya kijamii na pia kumtumia picha hiyo.
Alidai Wambui alikuwa amemwambia kwamba asipomtunza vizuri, angemwacha aende kwa mwanaume huyo.
Baada ya Mwangi kuondoka, Bi Wangare alisema alipata hisia za ajabu.
Alichukua tochi na kumtafuta mwanawe.Alimwita Wambui pia, lakini hakukuwa na jibu.
Mlango wa nyumba ya Mwangi ulikuwa wazi. Alimulika nyuma ya nyumba na kumwona mwanawe akiwa amejinyonga.
Alipiga mayowe, na mumewe Samuel Kimani pamoja na majirani wakafika.
Walipoingia ndani ya nyumba, walimkuta Wambui pia amefariki.
Miili hiyo ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Maragua Level Four.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Murang’a Cleti Kimaiyo alisema vifo hivyo vinachunguzwa, ingawa kwa mtazamo wa awali vilionekana kuwa mauaji yaliyofuatwa na kujiua.
Alisema polisi wako tayari kufuatilia mwelekeo mwingine iwapo ushahidi mpya utaibuka.
Shangazi ya Wambui, Tabitha Njoki, alisema kifo hicho kimeacha familia katika mshangao.
Wambui alikuwa mama wa mtoto wa kike wa miaka mitano.
“Aliniambia kwamba alikuwa akihamia( kwa Mwangi) kuolewa. Sikujua kwamba angekuwa katika ndoa kwa zaidi ya saa tatu tu. Mungu atuhurumie,” alisema.


from Taifa Leo https://ift.tt/rX3qxtp
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post