
Washirika wa Rais William Ruto wanaonekana kuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kumuinua Naibu Rais Kithure Kindiki kuwa msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.
Hafla ya Jumamosi katika Uwanja wa Kirigiti, Kiambu, ilifichua vita vipya vya kutafuta ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na wazee kutoka jamii za Agikuyu, Embu na Meru ilimshuhudia Profesa Kindiki akivishwa mavazi ya kitamaduni na kutangazwa kuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya.
Wawakilishi wa mashirika sita ya wazee kutoka Mlima Kenya waliidhinisha uungaji mkono kwa Rais Ruto na Profesa Kindiki, huku wakipinga juhudi za kugawanya Mlima Kenya kisiasa.
Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika mjadala kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo, alitetea hafla hiyo.
Bw Ruku aliitaja kama tamko rasmi la wazee wa Mlima Kenya kumtambua Profesa Kindiki kuwa msemaji na anayeshikilia mustakabali za kisiasa za eneo hilo.
Hafla hiyo pia ilionekana kufunga mjadala wa Bw Ruku wa kugawanya Mlima Kenya Mashariki na Magharibi. Kwa wiki kadhaa, waziri huyo alikuwa akitumia shoka na msumeno kuashiria wazo la kugawanya maeneo hayo kisiasa.
Hata hivyo, hafla hiyo ilizua upinzani kutoka kwa baadhi ya wazee na wanasiasa ambao walipinga uhalali wake.
Mlezi wa Kiama Kia Ma, Kung’u Muigai, alipinga kutawazwa kwa Profesa Kindiki huku mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu, Wachira Kiago, akisema kundi lake halikushiriki hafla hiyo.
“Wakati mwingine inafikia mahali ambapo unapaswa kujiondoa na kuwa shahidi wa yanayotokea. Nadhani hiyo ilikuwa hafla ya Kiama Kia Ma na sisi hatukuhusika,” akasema Bw Muigai.
Bw Muigai alisema baadhi ya wazee waliohudhuria hafla hiyo waliwahi kumtembelea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro na kumtambua kama kiongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya.
Alisema ushiriki wao katika hafla ya Profesa Kindiki ulizua maswali iwapo walikuwa wakiendeleza maslahi ya kibinafsi.
Bw Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama cha DCP , alijitenga na hafla hiyo na kukana kuhusishwa na wazee walioiandaa.
Alidai baadhi ya waliohudhuria walilipwa Sh3,000 kila mmoja, ingawa madai hayajidhibitishwa.
“Hizi ni njama za kisiasa zinazolenga kuwapatia nafasi salama mawakala wawili wa kugawanya mlima ambao ni Profesa Kindiki na Bw Ruku, kwa niaba ya Rais Ruto. Lakini kwa pamoja wanapaswa kujua kuwa kura ya 2027 itakuwa wakati wa kuwawajibisha,” akasema akiwa Kansas, Amerika.
Profesa Kindiki aliteuliwa kuwa Naibu Rais Novemba 1, 2024 baada ya Bw Gachagua kuondolewa mamlakani.
Tangu wakati huo, amekuwa akijitokeza kama kiungo kati ya serikali ya Kenya Kwanza na jamii za Mlima Kenya, huku akisisitiza kuwa atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto 2027.
Hata hivyo, uongozi wake wa kisiasa katika eneo hilo unapingwa na Bw Gachagua, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Martha Karua na viongozi wengine wa kisiasa.
Mbunge wa Juja, George Koimburi na mwenzake wa Ndia, George Kariuki, pia walizua maswali kuhusu kutawazwa kwa Profesa Kindiki, wakisema hafla hiyo haikuwa halali.
from Taifa Leo https://ift.tt/m1yiVlF
via
IFTTT