Viongozi wa DCP wawaka kuhusu kutawazwa kwa Kindiki Mlimani

VIONGOZI wa DCP wamepinga kutawazwa kwa Naibu Rais Prof Kithure Kindiki kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya, wakisisitiza kuwa uongozi wa kisiasa huamuliwa na wananchi wala si wazee.
Wakiongozwa na Seneta wa Nyandarua, John Methu, viongozi hao walifika Embu na kusema Kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, ndiye anayetambuliwa na wananchi wa eneo hilo kama kinara wao.
“Ni wakazi wa eneo hili wanaoamua nani awe kinara wao, wala si wazee.
“Kindiki anapaswa kuacha kufikiria kuwa yeye ndiye kinara wetu,” akasema Bw Methu akiwa Kianjokoma, Manyatta.
Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji alidai kuwa Sh60 bilioni zinatumika kugawanya Mlima Kenya kisiasa ili kura za eneo hilo zisiende ‘kapu’ moja kuelekea uchaguzi wa 2027.
 “Hatutaruhusu hili lifanyike. Eneo letu litaendelea kuwa kitu kimoja, iwe serikali ya Kenya Kwanza inapenda au la,” akasema Bw Mukunji.
Kauli zao zilijiri baada ya wazee kutoka jamii za Kikuyu, Embu, Mbeere na Meru kumuidhinisha Prof Kindiki kuwa msemaji wa eneo hilo katika hafla iliyofanyika Kirigiti, Kiambu mnamo Jumamosi. Wazee hao walimkabidhi Prof Kindiki mamlaka ya kuwakilisha maslahi ya jamii zote za Mlima Kenya na wakasisitiza umuhimu wa umoja wa eneo hilo.
Prof Kindiki aliwashukuru kwa kumuamini na kuahidi kutumikia jamii zote bila ubaguzi, huku akisema hataruhusu tofauti za kisiasa kugawanya eneo hilo.
Viongozi wa DCP pia walikosoa serikali kuhusu kuuawa kwa vijana wawili katika uwanja wa Nembure, Embu, wakati wa mkutano wa kisiasa uliohudhuriwa na Prof Kindiki na Gavana Cecily Mbarire.
 Bw Methu alitaka waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.


from Taifa Leo https://ift.tt/AFYScIL
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post