Afueni visa zaidi vya Ebola vikikosa kuripotiwa nchini

SERIKALI imesema hakuna kisa kipya cha Ebola kilichoripotiwa tangu kuthibitishwa kwa mgonjwa mmoja aliyekuwa ameambukizwa virusi vya ugonjwa huo kutoka nje ya nchi.

Watu 108 waliotangamana naye bado wamewekwa katika karantini na kufuatiliwa kwa karibu. Waziri wa Afya Aden Duale jana alisema kuwa hakuna hata mmoja kati ya watu hao aliyekuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo kufikia sasa.

Mgonjwa huyo, Mkenya aliyekuwa amesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Uganda, alipatikana na virusi hivyo, akawekwa katika kituo cha kutengwa Oktoba 5 na kufariki siku iliyofuatia.

Bw Duale alisema watu 122 waliokuwa na mtagusano na mgonjwa huyo wametambuliwa na kuthibitishwa. Kati yao, 108, sawa na asilimia 88.5, wako karantini na wanafuatiliwa kila siku huku serikali ikiendelea kuwatafuta wengine.

Alisema sampuli 293 zilizochukuliwa kutokana na tahadhari 289 za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa na ugonjwa huo zilipimwa, lakini ni sampuli moja pekee iliyothibitisha maambukizi.

Serikali pia imewapima wasafiri 667,675 katika vituo 26 vya kuingilia nchini, wakiwemo 2,345 katika muda wa saa 24 zilizotangulia.

Bw Duale alisema Kenya iliifahamisha Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kisa hicho ndani ya saa 24, huku vikosi vya kukabiliana na dharura vikiwa tayari kufanya kazi saa zote.

Maabara tano zilizoteuliwa zinapima sampuli, zikiwemo maabara mbili za kuhamishika katika vituo vya mipakani vya Lwakhakha na Busia.

Matokeo ya sampuli zilizothibitishwa yanaweza kupatikana ndani ya saa sita hadi 12. Serikali imetenga vitanda 241 vya kutenga wagonjwa katika hospitali tano jijini Nairobi, Eldoret na Mombasa. Aidha, wahudumu 4,917 wa afya wamepata mafunzo ya kukabiliana na Ebola, huku wataalamu 343 wakiwa tayari kwa dharura zozote.

Waziri huyo alisema hakuna marufuku ya safari, biashara, usafiri au mikusanyiko ya umma, na hakuna amri ya kutotoka nje iliyowekwa. Viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani vinaendelea kufanya kazi kawaida, ingawa uchunguzi wa afya umeimarishwa. Wakati huohuo, maafisa wa afya wameonya kuhusu hatari ya maambukizi katika miji inayohudumia madereva wa malori yanayosafiri kati ya Kenya, Uganda, DRC, Sudan Kusini na Rwanda.

Maeneo yanayofuatiliwa ni pamoja na Mai Mahiu, Naivasha, Gilgil, Salgaa, Molo, Londiani, Kericho, Narok na Bomet, pamoja na Timboroa, Eldoret na Kitale.

Afisa wa afya ya umma Dkt Reuben Osiemo alisema uchunguzi katika mpaka wa Kenya na Uganda unapaswa kuimarishwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Hata hivyo, maafisa wa afya Nakuru, Bomet na Kericho walisema kaunti zao zimeweka mikakati ya kukabiliana na dharura, ikiwemo kutenga vituo vya wagonjwa na kuwafunza wahudumu wa afya.



from Taifa Leo https://ift.tt/hAbmC3X
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post